SoC01 Tunaweza kuwa Taifa imara kama tutaamua kubadilisha Mfumo wa Elimu yetu

SoC01 Tunaweza kuwa Taifa imara kama tutaamua kubadilisha Mfumo wa Elimu yetu

Stories of Change - 2021 Competition

Mlalamikaji daily

JF-Expert Member
Joined
May 19, 2014
Posts
744
Reaction score
1,621
Wadau, hakika ili taifa liwe imara mfumo wa elimu yake lazima ubadilike, tuko hivi tulivyo kutokana na aina ya elimu yetu tunavyoitoa ikiwemo mitaala yetu! wakati nimeona hili shindano nikadhani ni bora nilete mjadala huu mpana katika nchi yetu namna ya kuleta elimu yenye tija! na yafuatayo ni mapendekezo yangu kwa kuanzia na madarasa ya awali na aina ya "maudhui" ambayo mwanafunzi anapaswa kuyapata

1. ELIMU YA AWALI IWE MIAKA MIWILI
Hapa mwanafunzi ajifunze lugha na utangulizi katika somo la hisabati, yaani mtoto ajue kusoma kwa ufasaha na kuhesabu na kufanya hesabu rahisi ili kumuandaliwa mazingira ya kuingia darasa la kwanza akiwa anajua kusoma vizuri, na mwishoni mwa darasa la awali kila mwanafunzi awe na ripoti yake ambayo mwalimu atakuwa amependekeza "kipaji na ujuzi mwingine ambao huyu mtoto anao mbali na hesabu na lugha ili sasa mwalimu wake wa darasa la kwanza aanze kumuangalia kwa undani.

2. DARASA LA KWANZA NA LA PILI
Hapa nashauri mwanafunzi asome masomo yale mawili kisha liongezwe somo la uzalendo ambalo itakuwa ni maalum kwa ajili ya kumuwezesha mtoto kuipenda nchi yake tangu akiwa mdogo, halafu hesabu na lugha iboreshwe zaidi ili kumfanya mtoto achangamke zaidi kwa maana hii darasa la kwanza na la pili watoto wasome masomo matatu tuu! lugha kidogo na hesabu sana.

3. DARASA LA TATU NA LA NNE
Hapa mwanafunzi asome hesabu, lugha, sayansi , uzalendo, na jeografia na somo la historia liwe la hiari kwa mwanafunzi , maudhui ya mtaala huu katika ngazi hii ilenge mwanafunzi kufanya, na sio kukariri na hivyo katika sayansi mtoto aanze kufanya majaribio madogo madogo na hapa nashauri angalau kila shule moja ya msingi iwe na chumba kimoja cha maabara ili kuwawezesha wanafunzi kufanya majaribio mbali mbali

4. DARASA LA TANO
Hapa mwanafunzi ataanza kuchagua masomo yake kwa kuwa tayari ndani ya miaka mitano tunaamini tumeshatengeneza msingi katika nyanja muhimu na hivyo mwanafunzi anaweza kuamua kusoma sayansi, ama Lugha ama hesabu au historia na jografia na hapa nashauri mwanafunzi asome masomo matatu tu kama ilivyo combination za masomo , kisha aongezewe na somo la uraia, ambalo ndani yake kutakuwa na mada za maadili na uzalendo


DARASA LA SITA NA SABA
Hapa ni kumjengea mwanafunzi uwezo wa kwenda kuendelea na masomo kwa hatua ya sekondari "upili" kwa yale mchepuo husika, ama kwenda kwenye vyuo vya ufundi stadi kama VeTa N.k
mwisho wa miaka hii miwili mwanafunzi afanye mtihani wa masomo yale manne.

KIDATO CHA KWANZA NA CHA PILI
Hapa mwanafunzi asome mchepuo wake kamili mfano CBG, HGL, PCM n.k na kisha somo la Civics liongezeke na kumfanya mwanafunzi kugundua na kuvumbua vitu kadhaa, na mwishoni mwa kidato cha pili mwanafunzi aliyechagua mchepuo wa sayansi anatakiwa kugundua ama kutengeneza kitu fulani katika kikundi cha wanafunzi wasiozidi watano kama kazi mradi yao ambayo itawapa alama katika mtihani wao wa mwisho, na wale watakao chagua mchepuo wa sanaa wanatakiwa kutunga kazi ya fasihi au kutunga mchezo wa sanaa, na hii haitakuwa kazi ngumu kwasababu mwanfunzi huyu amekaa miaka miwili akiwa na masomo manne tu!

KIDATO CHA TATU NA NNE
Hapa mwanafunzi aliyefaulu katika mtihani wa kidato cha pili ataanza kuchagua na kufanya umahiri katika fani mbali mbali, kuna ambae ataanza kujifunza fani mbali mbali kwa nadharia na vitendo kutokana na uchaguzi huo , na hapa italenga zaidi katika vitendo hususasani katika masomo ya sayansi na mwisho wa kidato cha nne mwanafunzi abuni au kutengeneza kitu cha kuendena na fani yake na hapa mwanafunzi ambaye hataendelea na kidato cha tano anaweza kujiunga na chuo katika fani mbali mbali na anaweza hata kujiajiri mwenyewe katika fani yake maana atakuwa ana umahiri katika hilo somo kwa miaka minne

KIDATO CHA TANO NA SITA
Hapa katika elimu ya juu mwanafunzi aendelee na masomo mawili tu na moja la maadili huku akikazana kufanya tafiti mbali mbali na wale watakaojikita katika sayansi waanze kuwezeshwa kwa kupewa mikopo na tafiti zao zilete manufaa kwa uma, mfano zile tafiti za panya kugundua mabomu n.k zinaweza kufanywa na mhitimu wa kidato cha sita tu, na sio profesa wa chuo kikuu kwakuwa tayari mhitimu ameiva katika fani husika na huyu anakuwa na thamani hata akirudi mtaani.

Mwisho wa kidato cha sita mhitimu atoe hitimisho katika utafiti aliokuwa anaufanyia kazi kwa miaka miwili na utafiti huo upimwe kwa asilimia alizofikisha na kama zitapungua basi mhitimu arudie tena mwaka unaofuata kuendeleza alipoishia , na hapa kila mhitimu alete utafiti wake na usiwe unaofanana na mwingine, hii italeta hali ya kutengeneza taifa lenye watu wanaotengeneza mambo na ugunduzi badala ya kukariri tuu

CHUO KIKUU
Hapa mhitimu wa kidato cha sita ataenda chuo kikuu kufanyia kazi zaidi ya utafiti wake kwa njia bora zaidi na hapa anaweza kuwa anasoma huku akiwa amefungua kampuni binafsi au shirika ambalo linafanya yenye kuzalisha kutokana na ule utafiti wake na sasa atakuwa hata anaweza kuajiri wafanyakazi kadhaa katika mradi huo huku yeye akiendelea kuongeza ujuzi zaidi katika eneo hilo,

Mhitimu wa chuo kikuu asipate shahada yake bila kuonyesha mradi ambao ni yeye aliuunda na unaendelea kutokana na kozi anayosomea, na sasa huyu mhitimu ni wazi kuwa hataingia katika janga la kukosa ajira na kutegemea kuajiriwa pekee , badala yake anaweza kuomba mkopo kwa kutumia vyeti vyake vya kidato cha sita na kuendeleza mradi wake kwa manufaa ya taifa,

MTAZAMO WANGU
Kama kila mwanafunzi atakuwa anajua kitu ambacho anasomea tangu akiwa mdogo hii italeta umahiri na kuongeza ufanisi, ni aibu sana mpaka mtu anamaliza kidato cha sita bado hajui anataka kuwa nani katika jamii! leo hii unaweza kufanya utafiti wako ndugu msomaji nenda kwenye shule zetu za sekondari halafu jaribu kuwauliza wanafunzi kuwa wanasoma ili wawe watu wa namna gani katika jamii! ni wachache sana watakuambia kitu cha kueleweka, lakini wengi watakuwambia hawajui, ama wanamuachia Mungu! na hivyo hivyo kwa wazazi! ni wachache sana ambao wanaona ndoto za watoto wao tangu wakiwa wadogo! na suala hili lipo katika nchi nyingi za kiafrika,

Ni wazi kuwa hakuna mzazi ambae atapenda mtoto wake arudi shuleni ama chuoni halafu aendelee kuwa mzigo pale nyumbani!

Na sisi kama wadau tunalo jukumu la kuhakikisha elimu yetu inakidhi vigezo! Rais mstaafu Kikwete alisema kunahitajika kuwa na mjadala wa kitaifa wa elimu nadhani alikua sahihi sana, hakuna maendeleo bila elimu, tutaenda mbele na kurudi nyuma lakini naona suala la elimu ni kipaumbele sana.

KWANINI TUKO HAPA LEO KWENYE ELIMU YETU?

Binafsi katika uchunguzi wangu nimebaini yafuatayo:

Kwanza, wanaosimamia mitaala na kuitunga mara nyingi sio wale wanaoingia darasani! na jambo baya zaidi wakati mwingine hata kile wanachokiweka kwenye mitaala hawana ujuzi nacho kabisa! niliwahi kuona mahali fulani muhtasari (syllabus) inamuelekeza mwalimu kufundisha vipindi 20 kuandaa hotuba kwa mwanafunzi wa kidato cha nne ! yaani mwalimu atumie zaidi ya dakika 790 kufundisha kuandaa hotuba? utaona hapa ni wazi huyu ambaye ameandaa hii hakuwahi kuingia huko darasani na kuona mazingira halisi ya ufundishaji!

Lakini vile vile jambo lingine ni kutanguliza siasa mbele, kama Nchi tungeweka maslahi mapana kuangalia zaidi namna ya kuboresha elimu yetu katika uwanda mpana zaidi wa kuangalia miaka 100 ijayo badala ya kuwekeza kwenye miaka michache tu!

HITIMISHO

Kama Taifa tukiamua kuwekeza katika elimu naamini miaka 20 ijayo tunaweza kuwa na vijana wetu wanaotengeneza na kugundua vitu mbali mbali vyenye manufaa kwa taifa tena wakiwa katika umri mdogo tu kwakuwa elimu imewawezesha!
lakini katika mchakato huu wote hauwezi kusogea na kufanikiwa endapo WALIMU wataachwa kando! Huwezi kutenganisha elimu na walimu na hivyo lazima mambo ya makusudi yafanywe kwa walimu ili kuweza kuendana na aina ya elimu husika, ikibidi mafunzo na semina elekezi zifanyike mara kwa mara ili waweze kuendana na mfumo tarajiwa

Ahsanteni kwa kunisoma karibuni kwa maoni
 
Upvote 11
Unaweza kusoma pia Hii habari kutoka jamiiforums...


NJOMBE: WALIOHITIMU CHUO WALAZIMIKA KUOLEWA ILI KUPUNGUZA UGUMU WA MAISHA

Kutokana na uhaba wa Ajira, Wadau wa #Elimu mkoani Njombe wameomba Mtaala ubadilishwe ili Elimu iendane na mazingira yaliyopo kwa Vijana kujiajiri

Soma > Njombe: Wahitimu wa vyuo walazimika kuolewa ili kuepuka ugumu wa maisha
#JFLeo
 
Back
Top Bottom