Tune Shaaban Salim: Mshindi wa Tuzo ya Nyerere ya Uandishi Bunifu Maktaba

Tune Shaaban Salim: Mshindi wa Tuzo ya Nyerere ya Uandishi Bunifu Maktaba

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
TUNE SHAABAN SALIM MWANDISHI NGULI NA MSHINDI WA TUZO YA NYERERE YA BURT AMEFIKA MAKTABA

Leo nimetembelewa Maktaba na mwandishi Bingwa na Mshindi wa Tuzo ya Nyerere ya Burt inayoshindaniwa na waandishi vijana kutoka Tanzania, Ethiopia, Kenya na Ghana.

Amekuja kunipa kitabu chake, ''Posa za Maana.''

Nimekipokea kwa furaha na nilisubiri anyanyue mguu tuu avuke kizingiti changu nikianze.

Aliponipa kisogo yeye na mumewe wanaingia kwenye gari haraka nimeingia ndani.

Mimi nimeumbwa na mshawasha wa vitabu.
Sina stahamala mbele ya kitabu.

Nikakianza.

Mashaallah ni kitabu cha mwendo kasi ni aina ya vile vitabu ambavyo kila ukurasa unakuita uufunue usome kuangalia kuna nini ndani yake?

Mama na baba wanapambana kuhusu posa ya binti mdogo hata masomo bado hajamaliza.

Mposaji anakimbilia utu uzima, anaogolea kwenye fedha na anaishi Ulaya na ana mitala.

Hapo nimekuonjesha kidogo.
Mama ana ndabi yaani mdomo baba mpole.

Sikutegemea hata siku moja kama mimi iko siku nitanyanyua kitabu kusoma na mwandishi awe ananifunza mimi Kiswahili.

Hii ni mara yangu ya kwanza kusoma kitabu nikakutana na maneno inabidi nifungue kamusi.

Ama kweli kila mjuzi kuna mjuzi kumpita.

Mwandishi Bi. Tune ni mwalimu na mwandishi wa vitabu vya shule vya kiada.

Nimepiga goti mbele ya mwalimu nimeamua kusomeshwa.

Ukiitaka elimu sharti upinde mgongo uinamishe kichwa mbele ya mwalimu uchote elimu.

Nafungua kurasa nasimeshwa.
Nimepigwa na mshtuko mkubwa.

Najiuliza huyu mwandishi anakifungua kitabu kwa staili gani?
Iweje aje na staili hii?

Mbona kama vile ananitayarisha kwa hatari inayonikabili katika kurasa za mbele?

Naam.
Sijakosea.

Ukianza kusoma ukurasa wa kwanza unakumbana na nyumba ya Bwana Khamisi na Bi. Salma iliyokuwa na mazingira yasiyopendeza tena kuna ukimya mkubwa ila kwa sauti za kuku.

Inakujia picha nyumba imehamwa haina wakazi.

Kuku wamezagaa kote wanachafua nyumba na kufanya kila aina ya vurugu.

Najiuliza.

Huu ukimya mbona unafanana na mwanzo wa utangulizi mfano wa ''Radi na kimulimuli,'' yaani "Thunder and lightning" katika mchezo wa William Shakespeare ''Mcbeth,'' kabla "Weird Sisters," hawajatokea katika jangwa?

Hawa "Weird Sisters," ni wanawake watatu wanga.

Hawa walikuwa washenga wa msiba.
Sasa hawa kuku wanaashiria kitu gani?

Hii fasihi ya Kiswahili.
Mbona akili yangu inanipeleka kwa Shakespeare?

Hili mwandishi kapanga kumtayarisha msomaji kwa makubwa au limejitokeza tu kwa bahati?

Vibweka vya kuku hawa sitakueleza.
Sitaki kukuondolea utamu.

Raha uvisome mwenyewe kitabuni.

Baada ya hapo sasa nafungua ukurasa naingia katika mazungumzo kati ya Bi. Salma, mke mwenye ndabi asiyechoka kusema na mumewe Bwana Khamisi mwanamme mpole maridhia.

Maisha yake yote Bwana Khamisi kakaliwa utosini na mkewe.
Hapa msomaji ndipo utakapostarehe na nafsi yako.

Hii ''dialogue,'' niwie radhi kwa kuandika Kiingereza.

Kuna maneno yanayo tafsiri ya Kiswahili lakini kwa mtu anaejua Kiingereza ukimtajia ''dialogue,'' anajua kwa hakika nini umekusidia.

Anatambua kuwa ni mazungumzo mazito baina ya pande mbili ya nipe nikupe.

Kitabu sijakimaliza lakini usisubiri nirejee hapa kukueleza kama jina la kitabu cha Shaaban Robert linavyosema, ''Ashiki Kitabu Hiki,'' kuwa mimi nikuambie wewe ukipende kitabu hiki.

Si kila siku utakutana na kitabu mfano wa hiki.
Amini kauli yangu na ashiki kitabu hiki.

1715805494690.jpeg

1715805534533.jpeg
 
Back
Top Bottom