SoC03 Tunu ya Mazingira

SoC03 Tunu ya Mazingira

Stories of Change - 2023 Competition

Baraka dyrocky

New Member
Joined
Aug 19, 2021
Posts
1
Reaction score
2
Wakati wote wa vipindi vya majira ya mwaka hali ya mazingira haikuwa na hiana kwani ilitulia tuli mithili ya maji yaliyomo ndani ya mtungi. Anga tulivu na angavu lenye rangi ya samawati lilizidisha uzuri wa mazingira.

Naam!hakuna ambaye angeliangalia bila kulimwagia sifa kedekede. Ndege nao hawakubaki nyuma,waliziachia nyimbo zao zenye sauti ya kusisimua kwa kila sikio la msikilizaji.

Mawimbi ya bahari yaliyotofautiana vimo hayakuacha kupiga pembezoni mwa fukwe, yalizidisha uzuri wa mazingira mithili ya mwanamwari kigoli mwenye kila aina ya pambo livutialo machoni mwa kila rijali. Giza nene la bahari lilitoa nafasi kwa samaki na wanyama wa majini kama pomboo, nyangumi, kombakoche, uduvi, taa, dagaa, taa, pweza,pamoja na kasa kuzaliana na kutengeneza ekolojia nzuri yenye mandhari ya kuvutia.

Misitu minene iliyoundwa kwa vichaka vya miiba na miti mikubwa kama misonobari, mikalatusi, minjane, mimalala,mipingo,mimbambakofi na mininga iliunda uoto wa asili. Wanyama wakali na wapole kama simba, nyoka mafasa, swala, paa, chui, tembo pamoja na sungura walionekana wakitalii vema katika baadhi ya maeneo. Wadudu kutoka jamii tofauti nao waliitumia fursa ipasavyo juu ya mazingira yale tulivu na kuyafanya yenye kuvutia zaidi. Nyuki waliweza kujipatia asali pamoja na kuchavusha maua akishirikiana na kipepeo. Siafu chini ya malkia wao walishindana kujenga vichuguu na kuipendezesha sakafu nzuri ya ardhi mithili ya zulia litandikwalo mwanzoni mwa lango la kuingia katika kasri la mfalme wa Wandiki.

Maeneo mengi ulimwenguni ikiwemo Tanzania yalibarikiwa kuwa na mazingira safi yaliyovutia. Udongo wenye rangi ya kipekee wenye rutuba uliweza kubeba mazao mbalimbali yakiwemo nafaka, matunda, mbogamboga, na viungo vya kupikia kama nanasi, ndizi, kauliflawa, mdalasini, mpunga, forosadi, karanga, mtama, mahindi, njegere na sukumawiki. Njaa haikuwa tishio tena kwa wakazi wa eneo husika. Maghala ya ukubwa tofauti yalitengenezwa kwa ajili ya kuhifadhi chakula cha akiba.

Kila lenye mwanzo halikosi mwisho na chovyachovya humaliza buyu la asali, hatimaye polepole tunu ya mazingira tulivu na yenye hewa safi ilianza kuharibiwa. Kadri muda ulivyozidi kwenda na miaka kusonga ndivyo hali ilivyobadilika. Mahitaji mbalimbali ya binadamu ambayo yaliongezeka kwa kasi kutokana na kasi ya kuzaliana yalisababisha uharibifu wa mandhari nzuri ya maeneo tofauti ulimwenguni hasahasa Afrika.

Lahaulaa! Taratibu ukame ulianza kuvamia baadhi ya maeneo mengi ulimwenguni. Na hii ni kutokana na ukataji miti katika misitu ambayo ilikuwa ndiyo chanzo kikubwa cha mvua. Ndege kama tai walianza kupotea kutokana na kuharibiwa kwa maskani zao.

Mkaa uliotengenezwa kwa miti iliyokatwa kutoka misituni uliweza kutengeneza hewa chafu ya kabonidioksaidi iliyosababisha mabadiliko makubwa ya hali ya hewa Afrika.

Shughuli za usafirishaji pamoja na viwanda zilichangia ongezeko la hewa chafu na nzito angani. Hewa kama chlorofluorocarboni (CFC’s) na kabonimonoksaidi zilichangia uharibifu wa tabaka la ozoni ambalo huzuia kasi ya miale ya jua kufika katika uso wa dunia. Magonjwa kama saratani ya ngozi yaliongezeka kwa kiwango cha juu na kusababisha vifo.

Uwindaji haramu wa wanyama pori kinyume na sheria kama ujangili dhidi ya meno ya tembo na uwindaji wa wanyama adimu ulisababisha kutoweka kwa viumbe hao. Pia matumizi ya mabomu na kemikali katika shughuli za uvuvi wa samaki baharini, kwenye mabwawa, mito na maziwa yaliharibu mazalia ya samaki na kupunguza uzalishaji wa samaki. Hakika hali ilibadilika.

La hasha! Udongo nao haukusalimika. Mbolea zisizorasmi pamoja na matumizi ya viuatilifu visivyokidhi ubora viliharibu na kupoteza rutuba na ubora wa udongo katika shughuli za kilimo. Shughuli za uchimbaji wa madini usiofuata kanuni za mazingira uliacha mashimo juu ya ardhi na kupoteza mvuto wake.

Bila shaka mazingira katika maeneo yote ya nchi kavu, majini, na angani yalikuwa yameharibiwa. Magonjwa yatokanayo na uvutaji wa hewa chafu, magonjwa ya macho, mmomonyoko wa udongo ulioweza kusababishwa na ufugaji wa wanyama wengi katika eneo dogo, mafuriko yaliyotokana na shughuli za kilimo pembezoni mwa vyanzo vya maji, utupaji wa taka ovyo uliosababisha magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, ongezeko la vifo vilivyosababishwa na utapiamlo kutokana na ukosefu wa lishe bora kwa watoto yalikuwa ni baadhi ya matokeo ya uharibifu wa mazingira.

Je, Ni nani asingependa kuishi katika mazingira tulivu na yenye amani yasiyo na chembe ya uharibifu?. Bila shaka kizuri chavutia. Uharibifu wa mazingira ni zaidi ya vita. Uharibifu wa mazingira hasa Afrika madhara yake ni makubwa na yamekuwa yakiongezeka kwa kasi hivi karibuni. Hali ya uchumi imezidi kuzorota kwa baadhi ya mataifa. Watu waishio chini ya dola moja kwa siku nao wameongezeka maradufu. Ni nani ajuaye kwamba Afrika mpaka kufikia 2050 itakuwa na mazingira mabaya yaliyoharibiwa au mazuri?

Licha ya jitihada mbalimbali juu ya utunzaji wa mazingira,bado uharibifu wa mazingira umekuwa ni tatizo licha ya Afrika kuchangia kwa kiwango kidogo katika uharibifu wa mazingira ukilinganisha na maeneo mengine ulimwenguni.

Utunzaji wa mazingira ni muhimu sana kwa maisha ya viumbe hai wote ulimwenguni. Uanzishaji wa kampeni za utunzaji wa mazingira zinazoendana na wakati kama zinazohusu upandaji wa miti, matumizi mbadala ya baadhi ya vitu kama vikapu badala ya mifuko ya plastiki, matumizi ya karatasi zilizotumika ili kupunguza karatasi zinazotupwa ovyo, uanzishaji wa klabu za mazingira katika taasisi mbalimbali kama mashuleni na vyuoni, utoaji wa elimu juu ya umuhimu wa mazingira kwa wanafunzi.

Vyote hivi vikisimamiwa ipasavyo tutaweza kuhakikisha tunapunguza na kuondoa kabisa shida ya uharibifu wa mazingira Afrika. Uwajibishwaji pamoja na uchukuaji wa hatua kali dhidi ya waharibifu wa mazingira bila kujali nani na anacheo gani ilimradi ameharibu mazingira itasaidia kupunguza kwa kiasi fulani athari za uharibifu wa mazingira.

Naam! Kwa hakika tukijitahidi kadri tuwezavyo kutengeneza mazingira na kuwa kama yalivyokuwa mwanzo kuanzia sasa mpaka kufikia 2050, hewa safi, majani yenye rangi nzuri ya kijani kibichi pamoja na ndege wazuri mithili ya hariri iliyonakshiwa kwa lulu na dhahabu watarejea tena kwa shangwe na bashasha Afrika na kuifanya kuwa yenye mazingira asili, safi na yenye muonekano unaovutia.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom