BAO pekee la Zahor Pazi wa Mtibwa Sugar jioni hii lilitosha kuitoa Yanga kichwa chini katika michuano ya Kombe la Tusker na sasa timu hiyo haijuwi hatima yake iwapo imefuzu Nusu Fainali au la mpaka itakaposubiri kura hapo kesho asubuhi..
Pazi ambaye ni mtoto wa kipa wa zamani wa Simba na timu ya Taifa, Idd Pazi Father, alifunga bao hilo katika dakika ya nane ya mchezo huo baada ya kuinasa kona iliyochongwa na Rashid Gumbo.
Mtibwa leo jioni iliwakilishwa na Shaaban Kado, Obadia Mwangusa, Idrissa Rajab, Chacha Marwa, Salum Sued, Shaaban Nditi, Zahor Pazi, Rashid Gumbo, Abdallah Juma, Uhuru Suleiman na David Mwantobe.
Yanga: Juma Kaseja, Shedrack Nsajigwa, Abdul Mtiro, Nadir Haroub Cannavaro, George Owino, Geofrey Bonny/Gaudence Mwaikimba, Shamte Ally, Nurdin Bakar, Jerry Tegete, Abdi Kassim na Mrisho Ngassa.
Kwa matokeo hayo, Yanga, Mtibwa na Mamlaka ya Mapato Uganda (URA) kesho asubuhi zitapigiwa kura kujua timu zitakazoingia nusu fainali za michuano hiyo. Timu zote zina pointi tatu na bao moja la kufunga na kufungwa.