habari toka :
Nifahamishe.com Habari za michezo za Tanzania
Simba yaangukia pua Tusker Cup, yatolewa nusu fainali
BAO la pili lililofungwa katika dakika ya 54 na Erick Obua wa Mamlaka ya Mapato Uganda (URA), lilitosha kuiwezesha timu hiyo kutinga fainali ya Kombe la Tusker na kuitupa Simba nje ya michuano hiyo.
Obua alifunga bao hilo la pili na hivyo kuifanya URA itoke uwanjani na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa jioni ya leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo ulianza kwa kasi, huku kila timu ikitafuta nafasi ya kufunga bao la haraka, lakini walikuwa Simba waliopata bao la mapema lililofungwa na kiungo Henry Joseph, katika dakika ya nne ya mchezo huo, baada ya kupokea pasi safi ya Ulimboka Mwakingwe.
Ikiwa imesalia dakika moja timu kwenda mapumziko, kosa lililofanywa na beki Ramadhan Wasso la kutoa pasi isiyokuwa na macho liliweza kuwapa bao la kusawazisha URA, lililofungwa na Mbiru Samson. Mpaka mapumziko timu hizo zilikuwa sawa kwa mabao 1-1.
URA itasubiri mshindi wa nusu fainali ya kesho itakayozikutanisha timu za Mtibwa Sugar ya Tanzania na Tusker ya Kenya.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Kocha wa Simba, Talib Hilal, alisema amekubali matokeo, lakini alilalamikia uamuzi wa mchezo wa leo kwa kusema haukuwa mzuri.
Endapo Tusker itashinda mchezo wa leo, timu hiyo na URA zitaweka rekodi ya kucheza fainali kwa mara ya pili ndani ya kipindi cha miezi mitano katika ardhi ya Tanzania. Tusker na URA zilicheza fainali ya Kombe la Kagame mwaka huu, ambako Tusker ilitwaa ubingwa.
Simba: Deogratius Bonaventure, Salum Kanoni, Ramadhan Wasso, Meshack Abel, Kelvin Yondan, Henry Joseph, Haruna Moshi ‘Boban', Mohamed Banka, Mussa Hassan ‘Mgosi', Emeh Izuchukwu na Ulimboka Mwakingwe.
URA: Dhamira Abel, Mbiru Samson, Kyombe David, Owino Joseph, Karangwa John, Maweejje Tommy, Ochan Patrick, Kigozi Ismail, Muwanga Martin na Obua Erick.
http://www.nifahamishe.com/NewsDetails.aspx?NewsID=591898&&Cat=6