SoC02 Tutengeneze safina

SoC02 Tutengeneze safina

Stories of Change - 2022 Competition

Captain Donor

Member
Joined
Jul 24, 2022
Posts
13
Reaction score
19
Maisha ni safari ndefu na kila hatua anayoipitia mwanadamu katika safari ya maisha ulimwenguni ina mazingatio makubwa sana. Kuzaliwa ndio pito namba moja la mwanadamu yeyote kuianza safari ya kuishi hapa duniani, lakini kabla ya kuzaliwa kuna mapito kadhaa ya kibayolojia mpaka kufanyika mtoto ndani ya tumbo la uzazi la mama hadi kufikia miezi tisa ya mama kujifungua. Uchovu na magumu anayopitia mama mjamzito kumleta kiumbe duniani unadhihirisha juu ya urefu wa safari ya maisha ya mwanadamu na huo ni utangulizi tu wa safari hii, kwani baada ya hapo hufuatia malezi ili kuhakikisha mtoto aliyezaliwa anakua hali yakuwa ana siha njema. Mpaka kufikia kiwango cha kujitambua na kujitegemea, mwanadamu hupitia mambo mengi ya kumjenga kifikra, kihisia na hata kiroho pia.

Kabla ya kuvumbuliwa kalenda yoyote katika historia ya maisha ya wanadamu ulimwenguni, yalitokea mambo mengi na baada ya kuvumbuliwa kalenda pia yametokea matukio mengi ya kihistoria ambayo mengine yamerekodiwa na wino wa historia na mengine yamebakia tu kwenye masimulizi kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Licha ya hivyo si matukio yote au mapito yote ya wanadamu ulimwenguni yanafahamika. Bila shaka umepata kusoma ama kusikia juu ya kisa cha Nabii Nuhu!.

Kama jibu ni ndiyo nikikuuliza unafahamu nini kuhusiana na kisa hicho bila ya shaka hauwezi kuacha kutaja habari za Safina. Tukirejea katika kamusi ya kiswahili sanifu neno Safina lina maana ya chombo cha kusafiria majini kinachosadikiwa kilitengenezwa na Mtume Nuhu kabla ya wakati wa gharika kama ilivyoelezwa katika baadhi ya vitabu vya dini ambavyo ni Kurani au Biblia. Je, ni mazingatio gani tunayoyapata na kujifunza kutokana na Safina ya Mtume Nuhu?

Ili kufikia malengo unayojiwekea katika maisha unahitaji kuwa na mpango mkakati uwe ni wa muda mfupi au mrefu pamoja na nyenzo maalumu kwaajili ya kutimiza malengo yako. Baada ya lengo la kuhubiriwa watu wa Nuhu kugonga ukuta ndipo Mungu alipomuamuru Nabii Nuhu kupanda mti na kuitengeneza safina kisha yeye na watu wake wachache waliomfuata pamoja na pea ya kila mnyama na ndege wapande safina muda wa gharika utakapowadia na hatimaye Mungu alitimiliza ahadi yake kama alivyomuambia Nuhu na watu wake.

Mungu ameweka kanuni za kimaumbile ambazo mtu akizizingatia basi atafanikiwa katika jambo lake analotaka kulifanya kama vile ukitaka kuvuna mazao ni sharti ulime kwanza, kisha upande mbegu na kumwagilia au kusubiri mvua inyeshe ndio mwisho wa siku utavuna mazao unayoyahitaji. Na si hivyo tu ni lazima upande mbegu ya mazao unayoyahitaji.

Safina ya Nuhu ilitengenezwa kwa lengo la kuwaokoa Nuhu na watu wake na pea ya kila kiumbe kutokana na adhabu ya gharika kubwa ya maji. Leo hii tupo karne ya ishirini na moja na vijana ulimwenguni kote tunakabiliwa na gharika ya ukosefu wa ajira!. Nafikiri pengine vijana tunahitaji safina kwaajili ya kujiokoa kutokana na gharika hiyo, je ni mambo gani tunahitaji kwaajili ya kuitengeneza safina kwa lengo la kujikwamua kutokana na ukosefu wa ajira?

Binafsi nina orodha ya mambo machache na ambayo unaweza kuhisi ni madogo sana kuyafanya ili kuondokana na mtazamo wa kutegemea kupata ajira na badala yake tuingize dhana ya uwepo wa kazi za kila namna zinazoweza kutukwamua kuondokana na utegemezi pamoja na umasikini;

1. Salimu watu
Salamu ni moja ya jambo muhimu sana katika mawasiliano na ndio mwanzo wa mazungumzo mazuri baina ya watu. Kusalimiana kunaunganisha watu na kuboresha mahusiano baina yao kwa kuwaleta karibu. "Habari yako" inaweza kutengeneza urafiki kati ya watu wawili wasiofahamiana kabisa. Salamu ni ufunguo wa mazungumzo na umuhimu wake una nguvu kiasi cha kuweka tabasamu kwenye uso wa mtu mwingine. Kusalimu watu ni moja ya sifa bora katika jamii na inaweza kukufungulia milango mingi ya mafanikio ikiwemo kupatiwa msaada pale utakapokuwa unahitajia msaada.

2. Amka mapema
Mojawapo ya siri ya mafanikio ya watu wengi wenye mafanikio makubwa duniani ni kuamka mapema. Zipo faida nyingi mtu anazozipata kutokana na utaratibu wa kuwahi kuamka mapema na faida kubwa mojawapo ni kujijengea nidhamu ambayo ndiyo hitaji namna moja la mtu anayetaka kufanikiwa. Kijana ukiwa na nidhamu ya kuamka asubuhi na mapema utaweza kupangilia vizuri mipango yako ya siku nzima iwaje jambo ambalo linachochoea ufanisi katika kuitekeleza mipango hiyo.

3. Fikiri tofauti
Mithali 23;07 inasema, "Maana aonavyo mtu nafsini mwake, ndivyo alivyo..". Fikra zako ndio mafanikio yako, ukiweza kuutawala vizuri mfumo wako wa kifikra basi utakuwa umefanikisha nusu ya kwanza ya safari yako ya kuyaelekea mafanikio. Kwasababu mfumo unaoendesha maisha yetu upo kwanza kwenye mawazo yetu, ni kipi tunafikiri na ni kipi tunachoendelea kukiwaza ndio kinachounda maisha yetu. Mfumo wa fikra unakupa kile ambacho unachokiwaza, kukiamini na kukizingatia akilini, kwahivyo kushindwa au kufaulu kunatengenezwa na mfumo huu ambao haudanganyi. Jifunze kuutumia vizuri ili ukupatie kile unachokihitaji. Kumbuka, fikra zako ndiyo mafanikio yako au kufeli kwako.

4. Insafu
Katika maisha ukifanya kila jambo hali yakuwa unamuogopa Mungu basi utakuwa mtu muadilifu na mwenye hamasa ya kutenda haki. Moja kati ya vitu ambavyo vinajenga chuki na kusababisha uvunjivu wa amani ni kukosekana uadilifu. Kuwepo kwa misingi imara ya kutenda haki katika jamii yoyote kuanzia ngazi ya kifamilia hadi taifa ni jambo muhimu sana linapaswa kuwekewa msisitizo haswa katika nchi nyingi za bara Afrika. Kuwatendea wengine kwa moyo safi na nia njema ni jambo bora sana, viongozi wenye mamlaka ndio wanapaswa zaidi kuwa na insafu.

5. Nena kweli
Hakuna mtu mwenye akili timamu anayependa kuongopewa, na kinyume chake ni ukweli kuwa kila mtu anapenda kuambiwa ukweli. Kwa hiyo ukiwa mwenye sifa ya kuwa mkweli watu wengi watakupenda japokuwa si watu wote wanataka kusikia ukweli, hivyo kwa kusema ukweli wapo ambao watakuchukia pia. Ukiwa mwenye sifa ya kunena yenye ukweli ni rahisi kuaminiwa na watu na uaminifu ni sifa inayoenziwa na wengi na ndio maana hata kwenye utumishi wa umma kipo kiapo cha uadilifu ambacho kinaendana na mtu kuwa mkweli, muaminifu, mtenda haki na mwenye kuwatumikia watu walio nyuma yake. Milango ya neema na fanaka huwafungukia wale wenye sifa ya ukweli na pia kuwa mkweli kunamuweka mtu karibu na watu wenye manufaa siku zote.

6. Anza sasa
"Mwaka mmoja baadae kutokea sasa utatamani ungeanza leo" ni nukuu maarufu kutoka kwenye lugha ya kiingereza inayohamasisha juu ya umuhimu wa kuanza kufanya mambo pasipo kuchelea. Pia ipo methali ya kiswahili isemayo, "liwezekanalo leo, lisingoje kesho". Mwanzo ni mgumu siku zote, na pengine muda ulio nao sasa ndio unaofaa zaidi kuanza kulifanya jambo lako kuliko muda mwingine wowote ule, kusanya rasilimali na nyenzo ulizo nazo, weka mkakati mzuri wa kulitekeleza hatua kwa hatua, kuwa jasiri na uanze sasa.

Hitimisho
Tukirejea katika vitabu vya dini (dini za kiabrahamiya) tunajifunza juu ya watu wa Nuhu na sababu iliyopelekea wakaokolewa baadhi na wengi wao wakaadhibiwa kwa gharika ya maji. Kutokana na hadithi ya Mtume Nuhu na watu wake binafsi nimejifunza jambo moja kubwa. Elimu ni wokovu kwa wale wenye kufikiri kwa kina, tafakuri ni aina ya ibada na mtu anayetumia muda wake kufikiri mambo kwa kina ni rahisi zaidi kuwa mchamungu. Kufikiri kabla ya kutenda kuna faida nyingi katika jamii na kinyume chake ni chanzo cha matatizo mengi yanayotokea kwenye jamii.

Ni maamrisho pamoja na maarifa aliyopewa Nuhu ya kupanda mti kwaajili ya kutengeneza safina ndiyo ilikuja kuwa sababu ya kuokolewa yeye, watu wake pamoja na pea za wanyama na ndege muda wa gharika ulipowadia. Nasi kama vijana wa karne ya ishirini na moja, licha ya mfumo wetu wa elimu kutokutuandaa kukabiliana na mazingira ya uchache wa ajira baada ya kuhitimu vyuoni yatupasa tutengeneze SAFINA(Salimu watu, Amka mapema, Fikiri tofauti, Insafu, Nena kweli, Anza sasa).
 
Upvote 1
Back
Top Bottom