Lady of Excellence
Member
- Jul 22, 2022
- 6
- 7
TUWALINDE WATOTO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA.
Utangulizi
Ni dhahiri kwamba ukatili wa kijinsia kwa watoto nchini ni tatizo linaloumiza hisia za wengi hasa kwa kuzingatia ongezeko la taarifa kuhusu visa vya namna hii kwenye vyombo vya habari na jamii kwa ujumla ambapo tunasikia ukatili wa kingono wanaofanyiwa watoto wadogo sana kuanzia mwaka mmoja hadi 13. Naandika andiko hili kwa lengo la kukumbushana wajibu wetu kila mmoja dhidi ya janga hili, ili kujenga watoto wenye afya njema kimwili, kiakili na kihisia.
Kwa ufupi, Mtoto ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18. Hivyo basi, Ukatili wa kijinsia naweza kusema ni vitendo anavyofanyiwa mtoto vyenye kudhuru mwili, hisia au kuleta madhara ya kisaikolojia kwa mtoto. Vitendo vya ukatili wa kijinsia vinajumuisha;
- Kuguswa au kushikwa bila ridhaa kijinsia mfano kutomaswa sehemu nyeti za mwili;
- Jaribio la kujaamiiana ambalo mkosaji alijaribu kufanya ngono na mtoto lakini hakufanikiwa; na
- Matumizi ya nguvu na kulazimishwa kufanya ngono (ubakaji au ulawiti) chini ya shinikizo au tishio.
- Mada Kuu
Kama tunavyofahamu kwamba wanaowanyanyasa watoto kingono wanaweza kuwa watu wa nyumbani, majirani, marafiki, ndugu na hata watu wasiowafahamu kulingana na mazingira watoto wanakuepo mfano nyumbani, shuleni au njiani. Kutokana na hulka ya watoto kuwa ni waoga hasa linapokuja suala la kuzungumzia mambo nyeti hasa ya kikatili wanayofanyiwa, hushindwa kueleza moja kwa moja kwa mzazi au mtu yeyote aliyemzidi umri kwa kuhofia kuadhibiwa na yule aliyemfanyia ukatili au huyo anayemfikishia taarifa hiyo.
Hivyo basi, linapokuja suala la kugundua kama mtoto anafanyiwa vitendo vya kikatili tusiwategemee sana watoto kutueleza moja kwa moja kwanza kama wazazi au walezi tusipokua wafuatiliaji wazuri kwenye maendeleo ya afya na ukuaji kwa watoto wetu hasa wenye umri mdogo. Hapa ninamaanisha wazazi au walezi kuongeza ukaribu na urafiki kwa watoto ili waweze kueleza yale yanayowasibu wanapochangamana na watu wengine kwenye mazingira mbalimbali wanayokuwepo pamoja na kugundua mabadiliko wanayopitia kipindi cha ukuaji wao.
Kisa cha Kweli;
Jina langu ni Helena, nimelelewa kwenye familia iliyozungukwa na ndugu wengi. Hivyo, nimekulia katika mazingira hatarishi ya kutaka kunyanyashwa kingono na ndugu pamoja na majirani kwani nikiwa nasoma shule ya msingi nimewahi kunusurika kubakwa katika nyakati mbili tofauti. Naaandika haya nikiwa naamini kama siyo elimu ya kawaida pamoja na ulinzi niliokua napewa na wazazi wangu, namna ya kuwa makini na kujenga mipaka na watu wengine, nakiri kwamba ningedhalilishwa mno kingono na watu hao waliokosa maadili. Nakumbuka tangu nilipoanza shule ya msingi, wazazi wangu walizoea mara kwa mara kunieleza mambo yafuatayo ambayo naamini yalikuwa silaha kubwa ya kunisaidia kuepuka kutendewa ukatili wa namna hii;
- Kutokupokea zawadi yoyote kutoka kwa mtu nisiyemjua,
- Nisifuatane au kucheza na watu nisiowajua,
- Nisikubali kushikwa maeneo nyeti ya mwili wangu (hili alipenda kusema mama yangu wakati akiniogesha),
- Nitoe taarifa kwa mzazi au mtu yeyote aliyenizidi umri ikiwa kuna mtu anataka kunifanyia kitendo kibaya,
- Pia, nisiogope vitisho vya mtu yeyote anayetaka kunifanyia kitendo kibaya kwani hawezi kunidhuru,
- Pia, ilikua ni marufuku kuagizwa sehemu yoyote nyakati za jioni jua likishazama.
Madhara Ya Unyanyasaji Wa Mtoto
Madhara makubwa yanayosababishwa na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto ni kama ifuatavyo;
- Madhara ya muda mrefu ya kimwili, magonjwa ya ngono na mimba za utotoni;
- Kuathirika kwa ukuaji wa ubongo wa mtoto na madhara ya kisaikolojia au matatizo ya kihisia kama hofu na sonona;
- Tabia hatarishi kama ushoga na usagaji; na
- Watoto kukua wakiwa wamebeba chuki, visasi na maumivu ambayo husababisha kuwa na maamuzi magumu wanapokuwa watu wazima mfano kukataa kuoa au kuolewa.
- Maoni ya Mwandishi
- Nianze na kina mama ambao ni walezi wa familia, wahakikishe wanapata muda kufuatilia maendeleo ya afya na ukuaji wa watoto wao ili kuweza kubaini tofauti au changamoto anazopitia mtoto kwenye ukuaji wake. Sisemi vibaya ila nawaonya sana wanawake ambao wanapenda kuwaachia wasaidizi wa majumbani kufanya kila kitu kinachomhusu mtoto mfano kuhakikisha mtoto ameoga, amekula na amelala. Kiukweli hili ni tatizo kubwa kwa sababu wakati mwingine watoto wanapitia ukatili na mateso mengi lakini hawezi kusema maana wengine ni wadogo kabisa.
- Wazazi/walezi na walimu kwa pamoja kuwaelimisha watoto wote wa kike kwa wakiume ili waweze kujitambua na kujilinda wao wenyewe kwa msaada wenu.
- Vyombo vya sheria na madawati ya jinsia kuzidi kusimamia haki za watoto na kutilia mkazo kwenye suala la adhabu kali dhidi ya ukiukwaji wa haki za watoto na ukatili wa kijinsia bila kujali uhusiano uliopo kati ya mtoto na mtuhumiwa; na
- Wote kwa pamoja kulingana na nafasi yako kwenye jamii, kuwathamini na kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kutoa taarifa kwenye vyombo vya sheria na haki za watoto.
- Hitimisho;
Attachments
Upvote
2