Julai 18, 2023, saa 3:19 usiku, mtumiaji wa Mtandao wa Twitter anayefahamika kwa jina la
Necto Kitiga aliweka
ujumbe unaotoa dokezo la kuonekana kwa Twiga maeneo ya
Ubungo, Dar es Salaam wakisafirishwa kuelekea kusikojulikana, hivyo aliwataka polisi kutoa tamko.
Necto Kitiga aliandika;
"Hapa ni Ubungo. Mapolisi watwambie hawa TWIGA wetu, wanapelekwa wapi? Siyo Kushughulika na watu wanaotetea raslimali za Nchi yetu Kama Kuuzwa kwa Bandari zetu au Mnawaita watu kwenye vituo vyetu Ili Kuendeleza wizi huu wa raslimali za Nchi hii kama mlivyohamia kwenye Twiga wetu?"
Hadi kufikia Julai 19, 2023, saa 3:00 asubuhi, ujumbe huu ulikuwa umesomwa na watu 8,056, ulipendwa mara 110, maoni 42 yalitolewa na watu 31 waliwashirikisha wengine kwa ku retwet kwenye mtandao huo.
Wachangiaji wengi wameonekana kutoa maoni yanyopinga usahihi wa taarifa hii.
Mathalani,
El Patron alisema
"Nyie ndio mnafanya watanzania waone siasa jau. Chakata taarifa zako kabla ya kwenda public."
Aidha, aliyewahi kuwa Mbunge wa
CHADEMA,
Joseph Selasini ni miongoni mwa baadhi ya watu wachache walioonekana wakikubaliana na madai haya. Aliandika;
"Ni kweli hapo ni Ubungo. Hao twiga walitolewa hifadhi ya Mikumi kwa ajili ya maonyesho ktk viwanja vya saba saba. Sasa wanarejeshwa hifadhini baada ya maonyesho kumalizika."
Ukweli kuhusu picha hii
JamiiForums imefanyia kazi suala hili katika kutafuta ukweli wake na kubaini kuwa, picha hii haihusiani na madai yanayotajwa na mtoa hoja, pia mazingira yake sio ya Tanzania.
Picha hii iliwahi kuwekwa kwenye
mtandao wa Reddit Oktoba 8, 2020, na mtumiaji wa Mtandao huo anayefahamika kwa jina la
r/hmmm.
Picha hiyo ilionekana tena kwenye mtandao huohuo
Oktoba 25, 2020 na
Oktoba 30, 2020 ukiwa na madai kuwa twiga hao walikuwa wanahamishwa kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine nchini Kenya.
Utafutaji wa picha kwa njia ya mtandao unaonesha pia kuwa Novemba 12, 2020,
Neverovali ILI DA aliweka picha hii kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook ikiwa na maneno
Prevoz žirafa.
Maneno haya yamebainika kuwa ni lugha ya
Kislovenia yaliyo na maana ya usafiri wa Twiga.
Mtumiaji mwingine wa Facebook,
Novemba 4, 2020 alitoa taarifa ya Twiga hao kuondolewa kutoka hifadhi ya Soysambu kutokana na uwepo wa mafuriko. Alisema;
"This is happening in Nakuru, Kenya where the giraffes are being evacuated by the Kenya Wildlife Service from the Soysambu Conservancy to another park because of flooding in the area."
Ushahidi huu kwa ujumla wake unathibitisha kuwa picha hii haikuchuliwa maeneno ya Ubungo, Dar es Salaam hivyo kufanya madai ya mhusika kuwa ni uzushi.