BoT yachunguza ufisadi ndani ya Benki ya Posta
na Ratifa Baranyikwa
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
SIKU chache baada ya kuibuka kwa tuhuma za ubadhirifu ndani ya Benki ya Posta (TPB), Benki Kuu (BoT) imekiri kutuma maofisa wake kufanya uchunguzi ndani ya benki hiyo.
Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndullu alilithibitishia gazeti hili jana kuwa, BoT imewatuma maofisa hao kufanya uchunguzi.
Hata hivyo, kwa kutaka kutohusisha suala hilo na tuhuma za ubadhirifu zinazoikabili TPB, Profesa Ndullu alisema kuwa wachunguzi hao walitumwa katika utaratibu wa kawaida wa BoT kuzikagua benki kila baada ya muda fulani.
Pamoja na kusema hivyo, alisema zinapotokea tuhuma za kuwapo kwa matatizo ya kiutendaji, basi maofisa hao wa BoT hulazimika kufanya uchunguzi wa kina zaidi, ili kubaini mapungufu.
Taarifa zilizoifikia Tanzania Daima siku kadhaa zilizopita, zilibainisha kuwa maofisa hao wawili wa BoT, ambao majina yao hayakutajwa, walitumwa kwa kazi maalum ya kuchunguza tuhuma hizo za ubadhirifu.
Sisi tunafanya uchunguzi
ni kawaida yetu, tunaita on site supervision inategemeana na taarifa ya benki
kila baada ya miezi mitatu tunafanya uchunguzi na tunafanya kama sehemu ya kazi yetu, alisema Ndullu.
Tanzania Daima ambayo ilikuwa ikifika mara kwa mara katika ofisi za Makao Makuu ya benki hiyo mwezi uliopita kwa nia ya kuonana na Mtendaji Mkuu wake, Alphonse Kihwele, imekuwa ikipewa taarifa za kuwepo kwa vikao vya bodi ya wakurugenzi.
Kuibuka kwa tuhuma hizo katika mtandao wa intaneti, kuliwashtua viongozi wakuu wa benki hiyo, ikiwamo Bodi ya Wakurugenzi na kwa kushirikiana na menejimenti iliunda kamati maalumu ya kuwasaka watu wanaoaminika kusambaza taarifa hizo hali iliyosababisha bodi hiyo kuwapa likizo za lazima maofisa wake watatu.
Hata hivyo, Kihwele akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili ambalo lilikuwa likitaka kupata ufafanuzi wa juu ya kile kinachoendelea kwenye vikao hivyo sambamba na kutaka kupata maendeleo ya uchunguzi, alimtaka mwandishi wa habari hizi kuandika maswali aliyotaka kumhoji na kisha kuyawasilisha ofisini kwake.
Tanzania Daima ilifanya hivyo na kuwasilisha maswali kwa Mtendaji Mkuu huyo, lakini hata hivyo alipopigiwa simu alisema kuwa hana majibu ya maswali aliyoulizwa.
Katika maswali ambayo gazeti hili lilitaka kupata uthibitisho, ni pamoja na kuwepo kwa taarifa za benki hiyo kuwafukuza kazi watumishi wake kwa madai kuwa ndio waliovujisha siri za benki hiyo.
Aidha, ufafanuzi mwingine ambao ulikuwa ukihitajika ni pamoja na kutaka kujua zoezi la kuwachunguza watu wanaoaminika kutoa taarifa za siri za benki hiyo kwenye mtandao wa Jamboforums.
Habazi zilizopatikana zinadai kuwa, moja kati ya ufisadi unaotajwa unahusisha tuhuma za kughushi barua ya Bodi ya Benki ya Posta, ili kumuwezesha Kihwele kuongezewa mkataba, wakati bodi inadai haikuwahi kukaa kikao kupendekeza aongezewe muda.
Mbali na tuhuma hizo, pia imeelezwa kuwa ufisadi mwingine uliofanyika unamhusisha kigogo mwingine anayedaiwa kuwalazimisha watengeneza mahesabu katika Idara ya Fedha kuhakikisha wanatoa hesabu zinazoonyesha benki inapata faida kinyume cha ukweli.
Aidha, tuhuma nyingine zilizomo kwenye waraka huo ni zile zinazodai kuwa, menejimenti imeandaa mtandao unaowahusisha baadhi ya wafanyakazi ndani ya benki hiyo, ili kuweza kufanikisha ufisadi huo.
Pamoja na mambo mengine, inadaiwa kuwa, timu hiyo ndiyo iliyoiingiza benki hiyo katika mikataba mibovu ikiwemo ule wa uwekezaji na uendeshaji wa mashine za kutolea fedha (ATMs) ambazo zinadaiwa kuigharimu benki hiyo mamilioni ya fedha.
Mkataba huo ambao TPB imeingia na taasisi moja ya fedha unaelezwa kuwa, ni kielelezo tosha cha mikataba ya kifisadi yenye nia ya kuliangamiza shirika ambapo benki hiyo imekuwa ikiilipa taasisi hiyo mamilioni ya pesa bila kupata faida yoyote.
Katika waraka huo wenye kurasa tisa, pia ufisadi mwingine uliolalamikiwa ni ule wa kuwepo utaratibu wa kulipa watu binafsi au kampuni za wanaodaiwa kuwa ni za marafiki pasipo kufuata taratibu zozote za fedha.
Utata mwingine umeibuka katika kesi inayodaiwa kuwa ni ya kupanga ikimhusisha ofisa mstaafu wa jeshi aliyeishitaki TPB, ambako katika kesi hiyo walitumiwa mawakili wa nje kuitetea benki hiyo huku mlalamikaji akitetewa na kampuni ya uwakili inayomilikiwa na mmoja wa watendaji wakuu wa benki hiyo.