Si unaona hii habari hapo chini?
Sumu ya ubaguzi si nzuri jamani!
Tulikoe Taifa letu!
Kibao chawageukia Wapemba
2008-05-18 11:44:54
Na Mwinyi Sadallah,Zanzibar
Wasiwasi umetanda visiwani Zanzibar kufuatia kusambaa kwa vipeperushi vinavyowataka wakazi wa Pemba kuondoka haraka kisiwani Unguja na kurudi kwao.
Kukamatwa kwa wananchi saba wanaohusishwa na kosa la uhaini kumeonekana kusababisha chuki na uhasama wa kisiasa miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.
Hali ya kisiasa visiwani hapa inazidi kuwa tete baada ya wananchi wa Unguja nao kusambaza vipeperushi vinavyounga mkono kisiwa cha Pemba kujitenga na vingine vikiwataka wapemba waondoke.
Baadhi ya wananchi waliohojiwa na Nipashe jana walisema sasa ndio itajulikana ipi mbichi na ipi mbivu, wenginewanasema wapemba ndio watakaopata shida zaidi iwapo wataamua kujitenga.
```Kuendelea kukamata watu Pemba ni sawa na kukaribisha machafuko, tunaomba Rais kikwete kusitisha mara moja zoezi hilo,``alisema Bw,Said Kombo mkazi wa Bububu.
Bw.Kombo alisema hivi sasa watu 10,000 waliosaini waraka huo wametishia kujisalimisha katika vituo vya polisi kitendo ambacho kinaweza kusababisha vurugu.
Wakizungumza kwa nyakati tafauti walisema hali ya kisiasa Zanzibar ilianza kutulia mara tu baada ya Rais Jakaya Kikwete kukiri kuwepo mpasuko wa kisiasa na kuahidi kuushughulikia.
``Lakini sasa mambo yamegeuka na hali ni ya kusikitisha,`` alisema mkazi mmoja wa Unguja.
Bw. Salum Ahmed mkazi wa Mchangani mjini Unguja, alisema kukamatwa kwa watu hao kumerejesha hali ya wasiwasi na baadhi ya watu wameanza kukimbia maeneo wanayoshi.
``Kimsingi makosa ya uhaini ni pale watu wanapotaka kupindua serikali au kumuua Rais sidhani kama kutoa maoni ni kosa la uhaini.
Mbona waliokata umoja wa kitaifa na kusema hapana cha mseto hawakuambiwa wanahatarisha umoja wa kitaifa``, alisema Bw. Salum mbaye ni mwalimu.
Mfanyabiashara maarufu Zanzibar , Bw. Mohammed Raza, alisema serikali ya Muungano inapaswa kuwaachia watu hao waliokamatwa ili kuendeleza nia njema ya mazungumzo ya mwafaka baina ya CCM na CUF.
Alisema jambo la msingi kwa sasa ni kwa CCM na CUF kuendelea na mazungumzo ili kumaliza mpasuko wa kisiasa uliopo Visiwani.
Alisema matatizo yanayojitokeza Zanzibar hivi sasa yanachangiwa na mfumo mbaya wa
Katiba ya Muungano na ya Zanzibar.
Bw. Masoud Suleiman alisema tamko la Polisi kuwa kuna watu wengine wanaendelea kutafutwa litasababisha mazingira ya wasi wasi na baadhi ya wananchi kuanza kukimbia maeneo yao.
``Ndugu zangu wako Pemba na nimesikia kuna watu wameanza kukimbia, sasa mazingira kama haya yanaibua siasa za chuki``, alisema.
Alisema wananchi waliopeleka barua ofisi za Umoja wa Matifa jijini Dar es Salaam walikuwa wakitoa maoni yao kama Katiba ya nchi inavyowaruhusu na haikuwa busara kuwakamata na kuwafungulia mashitaka.
``Mbona kuna Wabunge wa CCM katika utawala wa mzee Mwinyi walipeleka hoja Bungeni ya kuwepo serikali tatu, kwa nini hawakukamatwa na kufunguliwa mashitaka ya uhaini,`` alihoji Bw. Suleiman.
Wakati hali hiyo ya wasi wasi ikionekana wazi huku vipeperushi vya kurushiana matusi vikizagaa, Rais wa Zanzibar ,Bw.Amani Abeid Karume amenukuliwa akisema hali ya Zanzibar ni ya amani na shwari tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.
Rais Karume aliyasema hayo jijini Washington Marekani alipokuwa na mazungumzo na Watanzania wanaoishi nchini humo.