SIKU moja baada ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tarime kumalizika baadhi ya watu waliokuwa wameletwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameshindwa kuondoka mjini hapa baada ya kukosa nauli.
Habari za uhakika zilizopatikana mjini hapa jana na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere, zinasema kumekuwepo na malalamiko ya wafuasi wa chama hicho kushindwa kusafiri hasa baada ya viongozi wa waandamizi waliokuwepo hapa kuondoka ghafla hata kabla ya kutangazwa matokeo ya ubunge na udiwani juzi.
Katika kinyanganyiro hicho, mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Charles Mwera, aliibuka mshindi baada ya kupata kura 34,545 dhidi ya mpinzani wake wa CCM, Christopher Kangoye.
Hatua ya kuondoka viongozi waandamizi wa CCM akiwemo, Katibu Mkuu Yusuf Makamba, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda, Tambwe Hizza na wengine wengi kimeonekana kuacha kilio kikubwa kwa watu waliotegemea kupewa fedha kwa ajili ya nauli ya kuwasafirisha.
Mmoja wa wanaCCM ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema kitendo walichofanyiwa na viongozi hao ni funzo kubwa kutokana na ukweli kuwa waliahidiwa fedha kwa ajili ya masuala mbalimbali yakiwemo nauli, posho na fedha za kujikimu kwa siku ambazo walikuwa mjini hapa.
Alisema baada ya kukimbiwa na viongozi hao, hivi sasa wamebaki kuwa ombaomba na hawajui nini hatima yao ya kuendelea kubaki hapa huku shughuli zao nyingi zikikwama kutokana na kushindwa kuondoka.
Tumeletwa Tarime kwa ahadi nyingi na Makamba na viongozi wengi lakini sasa mambo yameharibika wameamua kutukimbia, tena bila hata kutuaga, maana tumekuja kumuona Makamba kwenye luninga akizungumza na waandishi wa habari mjini Mwanza juzi... sasa tabia kama hii inajenga picha gani katika siku zijazo? alihoji mwanachama huyo.
Alisema mbali yake yeye kuna baadhi ya wafuasi hao hivi sasa wamekuwa katika wakati mgumu kupata mlo wa mchana na jioni kutokana na kuishiwa fedha, hali ambayo wamesema kama ikiendelea itawaweka katika wakati mgumu.
Lakini kwa upande wake, Makongoro alisema amesikia kuwepo kwa suala hilo lakini aliahidi kuwasiliana na viongozi wenzake wa chama haraka, ili kubaini ukweli kama ni kweli au la ili waone namna ya kuchukua hatua haraka ili kunusuru watu hao.
Nimesikia kuwepo kwa malalamiko hayo na tayari kuna waandishi wa habari wamenipigia simu kuulizia tatizo hili... napenda kutumia nafasi hiyo kuwaomba kwanza niwasiliane na wenzangu ili tuone ni kweli au la, alisema Makongoro.
Alipoulizwa juu ya viongozi wa CCM kuondoka kimya kimya mjini hapa, Makongoro hakuwa tayari kutoa sababu za kukubali au kukataa zaidi ya kusisitiza kwamba wameondoka kwa taratibu za kawaida kama siku zote.
Hivi sasa kumekuwepo na uvumi mwingi kwamba viongozi wetu wametoroka hapa Tarime baada ya kubaini kwamba tumeshindwa kwenye uchaguzi... ukweli ni kwamba wameondoka kama watu wengine wanavyoondoka katika safari zao, sasa nashangaa kusikia kwamba wametoroka, alisema Makongoro.
Katika hatua nyingine, mbunge mteule wa Tarime, Charles Mwera, amesema kazi ya kwanza kuifanya kwa wananchi wa Tarime ni kuhakikisha anaendeleza yale yote yaliyokuwa yakifanywa na mtangulizi wake, marehemu Chacha Wangwe.
Alitoa kauli hiyo mjini hapa wakati alipokuwa akiagana na timu ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali hapa nchini, waliokuwa hapa kwa ajili ya kuripoti habari za uchaguzi.