Tarime yatikisika
Mwandishi Wetu Oktoba 8, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiishutumu Polisi na vyama vya NCCR-Mageuzi na DP kufanya kazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Tarime, hali katika jimbo hilo imezidi kuzizima na joto la uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumapili.
Hayo yakiendelea, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amewasili Tarime na ataanza kujibu mapigo akitumia helikopta maalumu ya kukodi ili kukamilisha kampeni kabla ya Jumapili.
Kwa muda mrefu sasa, Chadema imekuwa ikidai kwamba NCCR-Mageuzi wakiongozwa na Mwenyekiti wake, James Mbatia na DP chini ya Christopher Mtikila, wamekuwa wakitumiwa na CCM katika kuvihujumu vyama vya upinzani wakati wa uchaguzi, lakini sasa shutuma hizo zimezidi kukua na kuanikwa hadharani huku Polisi nayo ikiongezwa mkumboni.
Katika mkutano na waandishi wa habari jana Jumanne, Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema ya kuwa kuna ushahidi wa wazi kwamba NCCR-Mageuzi na DP wamekuwa wakifanya kazi ya CCM na sasa wanasaidiwa na Polisi waliopelekwa kulinda usalama jimboni humo.
Akisaidiwa na kiongozi mwingine mwandamizi wa chama hicho, Chiku Abwao, Lissu alisema imethibitika kwamba NCCR-Mageuzi na DP wanatumika na CCM kuvuruga nguvu ya upinzani na vyama vinavyolengwa ni Chadema na CUF. Chiku Abwao amewahi kuwa kiongozi na Mbunge kupitia NCCR-Mageuzi na ametoa siri ya baadhi ya maamuzi ya kuua upinzani aliyopingana nayo kabla ya kukihama chama hicho.
Viongozi hao wa Chadema wamekumbushia jinsi NCCR-Mageuzi ilivyohujumu upinzani katika uchaguzi mdogo wa marudio uliofanyika kisiwani Pemba, ambako waliweka wagombea kinyume cha maamuzi ya vyama vingine vya upinzani wakati mara kadhaa Mtikila amekuwa akitoa kauli zenye kuvishutumu vyama vya CUF na Chadema.
Lissu alisema wakati mwaka huu, NCCR-Mageuzi na DP vimeweka kambi Tarime kuihujumu Chadema na kuisaidia CCM, mwaka 2005 vyama hivyo, alisema, vilifanya kampeni kuvuruga nguvu ya upinzani na Mtikila wa DP alimwekea pingamizi Mgombea Mwenza wa Chadema, kabla ya pingamizi lake kutupwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na baadaye Mahakama.
Kwa upande wa Polisi, Chadema wanadai kwamba badala ya kulinda amani na kuvitendea haki vyama vyote, jeshi hilo limekuwa likionekana kupokea amri na maelekezo kutoka kwa viongozi na mashabiki wa CCM bila kuzingatia sheria na taratibu za kazi zao.
"Chadema kinalaani vikali matukio ya hivi karibuni ya Polisi kutumia mabavu, vitisho na vitendo vya ukandamizaji ili kuwatisha wananchi wa Jimbo la Tarime kwa lengo la kuisaidia CCM kushinda Tarime. Tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi huo wiki tatu zilizopita, mamia ya wananchi, hasa vijana, wa maeneo mbalimbali ya Jimbo la Tarime wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka mbalimbali ya kubambikiza," alisema Lissu.
Lissu amesema licha ya sheria kuruhusu Mahakama kutoa dhamana kwa wale wanaotuhumiwa kwa makosa hayo, karibu wananachi wote waliokamatwa wakati huu wa kampeni za uchaguzi wamenyimwa dhamana kwa kisingizio kwamba wanahatarisha usalama wakati huu wa kampeni za uchaguzi mdogo.
"Wakati wanachama na wafuasi wa CHADEMA wakiwa wanakamatwa na kunyimwa haki yao ya kupata dhamana, wanachama wa CCM pamoja na makada wao wamekuwa hawachukuliwi hatua zozote za kisheria licha ya kufanya vitendo vya uvunjaji sheria wazi wazi," alisema.
Alitoa mfano wagombea wa CCM pamoja na wanaowaunga mkono kutoa kauli za kuchochea vurugu na kauli za kijinai lakini wamekuwa wakiachwa bila kukamatwa wala kuchukuliwa hatua zozote.
"Wagombea wa CCM na wagombea pandikizi wa CCM kutoka vyama vya DP na NCCR-Mageuzi au wapambe wao wa karibu, wametoa tuhuma za uongo na uzushi hadharani kwamba Chadema ndicho kinachohusika na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime Marehemu Chacha Zakayo Wangwe, hakuna hata mmoja wao aliyekamatwa au hata kutakiwa kutoa maelezo Polisi pamoja na kwamba tuhuma hizo za uzushi na uongo ni kosa la jinai chini ya sheria za nchi yetu," alisema Lissu.
Alisema hata ilipotokea kupigwa mawe kwa gari la Chadema aina ya Fuso likiwa limeegeshwa usiku kupigwa mawe na wanachama wa CCM, wahusika wa CCM waliokamatwa na walinzi wa Chadema na kufikishwa Kituo cha Polisi cha Wilaya waliachiliwa huru pamoja na kukiri kuwa walitumwa na kiongozi mmoja wa CCM kufanya uhalifu huo.
"Kiongozi wa CCM aliyetuhumiwa kuwatuma wahalifu hao naye hajakamatwa wala kuitwa kwa mahojiano na Jeshi la Polisi. Aidha wanachama wengine wawili wa CCM ambao walitajwa kuhusika na tukio hilo mpaka leo hawajakamatwa na kufikishwa Polisi huku Polisi wakisema kuwa wanawatafuta ilihali vijana hao wakionekana mitaani Tarime wakiendelea na kampeni za CCM," alisema.
Katika kuelezea matukio ya mabavu, Lissu amesema wagombea ubunge na udiwani wa Chadema Charles Mwera na John Heche Suguta, Mkurugenzi wa Vijana Makao Makuu John Mnyika na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Dk. Ben Kapwani pamoja na viongozi wengine wa wilayani Tarime walikamatwa na kuwekwa mahabusu kwa kisingizio cha kufanya mkutano usiokuwa na kibali.
"Ikumbukwe kwamba Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 na Kanuni za Uchaguzi wa Wabunge na wa Rais za mwaka 2005 hazizungumzii chochote juu ya vyama vya siasa kuomba vibali vya kufanya mikutano yao wakati wa kampeni za uchaguzi," alisema.
Alisema Chadema hakikuwa na wajibu wowote kisheria wa kuomba kibali cha mkutano wake wa kampeni kwa Jeshi la Polisi na hivyo, kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata wagombea na viongozi si halali na kinalenga kuibeba CCM katika uchaguzi huo mdogo kwa kuwatisha wagombea, viongozi, wanachama na wapiga kura wanaokiunga mkono Chadema.
Viongozi wa Chadema walikamatwa juzi wakiwa wanatoka eneo la Buhemba ambako walikuwa wamemaliza kuhutubia mkutano wa hadhara.
Msafara wa magari na watu waliokuwa wanawasindikiza wagombea kurudi mjini ulijikuta ukisimamishwa kwenye eneo la Gereza la Buhemba.
Baada ya kufikishwa Polisi viongozi hao wa Chadema walikataa kuandika maelezo yao pasipo kuwa na wakili wao ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee. Wakili huyo baadaye aliruhusiwa kuingia kituo cha Polisi kabla ya wao kuachiwa huku wafuasi wao wakiendelea kushikiliwa kitendo kilichopingwa na viongozi hao.