Kitu kimoja ambacho baadhi ya watu wanadharau kukizingatia ni kuwa, Ubungo inakua kwa kasi sana. Ongezeko la makazi ya watu katika jimbo hilo ni kubwa na la haraka kuliko sehemu yoyote ya Jiji. Na kila inapotokea ongezeko hilo, mahitaji mapya hujitokeza na yanapojitokeza yanasababisha malalamiko mapya.
Ukweli ni kwamba, Ubungo ya leo sio ilivyokuwa miaka michache ya nyuma. Nakumbuka mwaka 2000 sehemu kama Mavurunza, King'ong'o na nyinginezo zilikuwa hazifikiki na wala hayakuwa makazi ya kutarajiwa. Sehemu kama Goba ambazo zinapitika kwa urahisi sasa zilikuwa ngumu pia. Ukienda Goba leo, utashuhudia ukuaji wa kasi uliofanyika. Ni sehemu ambayo kupata ardhi ni ngumu kama sehemu nyingi za Jiji ambazo zimeendelea sana. Nina rafiki yangu mmoja alinunua ardhi mwaka 2000 kwa shilingi 3.5mil (nusu eka), sasa ardhi kama hiyo ni 35mil na haipatikani kwa urahisi.
Ukweli utabaki kuwa, hakuna Mbunge anaeweza kufanya kila kitu kinachotarajiwa na watu wote hasa katika nchi masikini na yenye mahitaji mengi kama Tanzania. Hakuna Mbunge anaeweza kuhakikisha maji yanamfikia kila mtu, kwa wakati yanapohitajika bila kuwa na malalamiko yoyote.
Miaka mitano iliyopita, maji lilikuwa tatizo kubwa sana Ubungo. Na kama wengine watakumbuka, wananchi wengi walitaka hilo ndio liwe tatizo la kufanyiwa kazi pekee (ingetosha). Angalau leo yanapatikana walau kidogo (kwa mgao). Tofauti na umeme au baadhi ya mahitaji mengine, maji hayatengenezwi kwa mitambo au viwandani. Yanakusanywa na kusambazwa. Kiasi kinachoweza kumfikia mtu mahali alipo, kinategemea sana miundombinu iliyopo na umbali, terrain na kadhalika ambazo mtu huyo anaishi.
Anyway, mwaka wa uchaguzi umefika. Ubungo itakuwa na Mbunge mpya ifikapo mwisho wa mwaka huu. Inawezekana akaja na maajabu.