Hafla ya kutoa tuzo ya mpango wa utalii wa MKSE imefanyika hivi karibuni mjini Nairobi, Kenya. Kwenye halfa hiyo, waziri wa utalii wa Kenya Bw. Najib Balala amesema mpango huo ni sehemu muhimu ya kukuza sekta ya utalii, moja ya nguzo za uchumi wa nchi hiyo, na unalenga kuyapongeza mashirika yanayoweza kutoa huduma bora za utalii nchini Kenya. Mashirika hayo yanapaswa kutoa bidhaa mpya kwa njia ya ubunifu ili kukidhi mahitaji mapya ya wateja.
Kwa mujibu wa Baraza la Wasafiri na Utalii Duniani (WTTC), watu milioni 24 barani Afrika wanajihusisha kwenye utalii, na katika baadhi ya nchi za Afrika, sekta hiyo inaweza kuchangia asilimia 10 ya pato la taifa GDP. Mwaka 2019, sekta ya utalii imeingiza dola za kimarekani bilioni 168 barani Afrika. Na ripoti ya makadirio iliyotolewa mwezi Julai mwaka jana na Kamati ya Biashara na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa UNCTAD imesema katika hali mbaya zaidi, janga la COVID-19 litailetea sekta ya utalii hasara ya dola za kimarekani trilioni 3.3, na huenda nchi zinazoendelea zitaathiriwa vibaya zaidi.
Je, jinsi ya kukuza utalii kwa njia ya ubunifu katika msingi wa kudhibiti maambukizi ya COVID-19 ni swali linalohitaji majibu ya dharura? Hivi sasa, nchi nyingi za Afrika zinajitahidi kudhibiti maambukizi ya COVID-19 huku zikichukua hatua za kuwavutia watalii. Kadri hali inavyozidi kuwa tulivu, ndio Kenya inavyojitahidi kurudisha safari za ndege ndani na nje ya nchi, na hivi sasa sekta ya utalii na hoteli imeanza kufufuka taratibu, na kiwango cha kukodi hoteli katika baadhi ya vivutio vya utalii, mbuga za wanyama na jijini Naiorbi kimeongezeka na kurudi kwenye asilimia 25 hadi 40 ya hali ilivyokuwa kabla ya kutokea kwa COVID-19, wengi wao wakiwa watalii wa ndani. Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia nazo pia zimechukua hatua mbalimbali kuwapokea watalii wa kimataifa. Ikiwa sehemu ya mkakati wa kuhuisha utalii wa Kenya kwa ushirikiano kati ya serikali na mashirika binafsi, mpango wa MKSE unalenga kukuza utalii wa kitamaduni na kutoa bidhaa na huduma zenye sifa za kipekee za Kenya.
Kwa kuunganisha sekta nyingine, wigo wa utalii unaweza kupanuliwa. Ubunifu ni injini ya ukuaji wa uchumi na sekta ya utalii, na COVID-19 imehimiza matumizi ya “miundombinu mipya” kama vile 5G, akili bandia na big data kwenye sekta ya utalii, na kufanya “vivutio vya kidigitali, jumba la makumbusho la kidigitali na utalii wa kujipatia maarifa halisi kuwa hali halisi. Baadhi ya vivutio vya utalii vya Kenya pia vimetumia mbinu za teknolojia ya kisasa kutoa huduma za utalii katika mtandao wa internet. Kwa mfano, hifadhi ya Ol Pejeta nchini Kenya inafanya shughuli ya utalii kwenye mtandao wa kijamii ili watalii wasioweza kutalii watembelee kwenye mtandao wa internet.
Hasara zinazotokana na COVID-19 haziwezi kuondolewa ndani ya muda mfupi, na sekta ya utalii sio tu inahitaji usaidizi wa serikali, bali pia kutoa mikakati ya kukabiliana nayo katika msingi wa kudhibiti maambukizi ya virusi. Kwa upande mmoja, COVID-19 imeisababishia hasara kubwa sekta ya utalii, lakini kwa upande mwingine imefukuza shughuli za utalii zisizokuwa za kiubunifu. Ule msemo wa Mwenye Nguvu mpishe umejidhihirisha na kuongeza kasi ya mageuzi ya sekta ya utalii, kwa hivyo wadau wa utalii wanatakiwa kubadili mawazo yao, kuangalia mahitaji ya soko na wateja, na kuifanyia ubunifu na kuendeleza sekta ya utalii.