Uchaguzi 2020 UCHAGUZI 2020: Vyombo vya Habari tunavyovihitaji Tanzania

Uchaguzi 2020 UCHAGUZI 2020: Vyombo vya Habari tunavyovihitaji Tanzania

Joined
Nov 2, 2007
Posts
12
Reaction score
9
Uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 umeanza. Je, tunahitaji Vyombo vya Habari vyenye sifa zipi wakati tukiingia kwenye kampeni hizi? Nimeorodhesha hapa chini matarajio 7 ambayo yanapaswa kufikiwa na vyombo vya habari nchini ili kujenga mazingira bora ya Kampeni na Uchaguzi.

1. Vyombo vya habari vinavyotoa fursa linganifu kwa vyama vya siasa na wagombea: Uchaguzi ni ushindani na ushindani unakuwa ushindani kama wanaoshindana wanapewa fursa linganifu ya kushindana kupitia vyombo vya habari. Umuhimu huu unatajwa kwenye kanuni za Utangazaji za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kifungu cha 19 (a) ambacho kinawataka watoa leseni wote kutoa fursa linganifu na fursa sawa kwa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi. Hii maana yake ni moja – Vyombo vya Habari visiwe na upendeleo. Visipendelee upande mmoja wa ushindani. Vitoe fursa yenye manufaa kwa vyama vyote na wagombea wao.

Wajibu huu ni mkubwa zaidi kwa ‘vyombo vya habari vya umma’ kama Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). Tarehe 18/8/2020, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage alisisitiza wajibu huu kwa ‘Vyombo vya Habari vya umma’ wakati akiongea na wahariri wa Vyombo vya Habari. Vyombo hivi vina wajibu wa kutoa fursa linganifu na sawa kwa vyama na wagombea wao.

2. Vyombo vya Habari vyenye kuangazia ilani za vyama na sio watu: Kuna makundi matatu muhimu hapa: vyombo vya habari, wapiga kura na wagombea na vyama vyao. Kila kundi lina wajibu wake. Wagombea na vyama vya siasa wanawajibika kujiuza kupitia ilani zao. Ni ilani za uchaguzi ndizo zenye kubeba matumaini ya wapiga kura ambao wajibu wao ni kufanya maamuzi sahihi yatokanayo na taarifa sahihi. Taarifa hizi hutoka kwenye ilani za uchaguzi. Hivyo, ni wajibu wa vyombo vya habari kuangazia ilani za vyama – zimebeba nini, zinatengeneza matarajio gani kwa wananchi, zinatekelezeka na kwa kiasi gani, zimetekelezeka na kwa kiasi gani nk. Kuangazia wagombea (watu) pekee bila ilani wanazopaswa kuzitetea ni kuwanyima fursa adhimu wananchi ya kuhabarishwa na hatimaye kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wakati ukifika.

3. Vyombo vya habari vyenye kuchambua habari na sio kuandika matukio: Wakati wa chaguzi ni wakati wa matukio. Kila mwanasiasa atakuwa na tukio, vyama vya siasa vitakuwa na matukio, wanachama nao watakuwa na matukio. Ni wajibu wa vyombo vya habari kujikita katika kuchambua hayo matukio na sio kuyaandika tu kama yanavyotokea. Uchambuzi wa matukio husaidia kuamsha umma, kujenga hadhira dadisi, kuzalisha jamii yenye kuthamini mijadala. Haya yote hukomaza jamii kifikra na kimaamuzi na hili ndilo jambo la msingi kwa wakati huu.

4. Vyombo vya habari vyenye kutoa maoni kinzani: Tafiti za Ubora wa Maudhui ya vyombo vya habari Tanzania kwa mwaka 2019 na 2020 zinaonyesha uchache wa maoni kinzani kwenye maudhui ya vyombo vya habari. Vyombo vya habari vimekuwa vikiandika na kubeba maoni ya aina moja, maoni ya kundi moja, maoni yenye kuakisi mtazamo wa upande mmoja. Wakati wa uchaguzi ni wakati wa ushindani, ni wakati wa kushindanisha hoja, ni wakati wa kushamiri kwa maoni kinzani. Hivyo basi, ni wajibu wa vyombo vya habari kuandika na kurusha maoni kinzani yanayotoka kwa wagombea mbalimbali, kwenye makundi mbalimbali na kwenye vyama mbalimbali.

5. Vyombo vya habari vyenye kutoa haki ya kujibu tuhuma kwa wakati: Kanuni za Maudhui za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za mwaka 2018 kwenye kipengele cha 19 (k) kinachohusu habari za uchaguzi kinaelekeza Vyombo vya Habari kutoa nafasi ya kujibu tuhuma kwa mtuhumiwa ndani ya saa 24. Kipindi cha Uchaguzi ni kipindi kinachozalisha tuhuma. Tuhuma baina ya wagombea, tuhuma baina ya vyama, tuhuma baina ya wagombea na vyama nk. Ni wajibu wa Vyombo vya Habari kutoruhusu tuhuma kutolewa bila kujibiwa. Kila anayetuhumiwa ni vema apewe nafasi ya kujibu tuhuma zake na ni vizuri zaidi kama tuhuma hizo zitajibiwa ndani ya habari husika.

6. Vyombo vya habari vyenye kubeba sauti za wananchi: Lengo la uchaguzi ni kuwapatia fursa wananchi kuchagua viongozi watakaowaongoza. Mnufaika mkuu ni mwananchi. Ni wananchi hawa hawa ndio wenye kujua nini wanataka, nini wanakosa. Ni wananchi hawahawa ndio wenye haki ya kutoa maoni kuhusu wagombea na vyama vyao. Vyombo vya habari vinawajibu wa kubeba sauti na maoni ya wananchi. Vyombo vya Habari visiwachukulie wagombea kama wasanii kwenye majukwaa na wananchi kama watazamaji wenye kufuata burudani. Wananchi ndio wadau wakuu na sauti zao hazina budi kupaishwa na zisikike.

7. Vyombo vya habari vyenye kuweka maslahi ya taifa mbele: Hapa nazungumzia maslahi ya taifa la Tanzania – sio maslahi ya mgombea, wagombea wala vyama vya siasa. Vyombo vya habari vimulike mienendo ya wanasiasa, vyama vya siasa, wafuasi na mashabiki wa vyama vya siasa na mienendo ya taasisi mbalimbali nchini ambazo kwa namna moja au nyingine zinahusika na uchaguzi. Vyombo vya habari viwe tayari kupaza sauti pale panapojitokeza dalili za uvunjifu wa amani nchini. Vipaze sauti yenye kusikika na yenye kukemea hali hiyo. Vyombo vya habari na waandishi wa habari wasiruhusu kuwa chanzo au kichochea cha vurugu nchini. Tanzania ni zaidi ya vyama vya siasa na wagombea wao.


Abdallah Katunzi

Mtafiti na Mshauri wa masuala ya Habari na Mawasiliano

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
 
Hili andiko limekuja wakati muafaka kabisa. Waandishi wa habari wameliona?

Ni andiko zuri na ni ukumbusho kwa wanahabari na vyombo vya habari nchini.

My only concern is whether the media we have can live to this aspiration. They are fighting several battles, some are silent. Angalia yaliyowakuta Clouds!
 
Mkuu asante sana kwa kutoa mwanga. Ila baadhi ya vitu vinavyofanya tusifike huko na tunakoelekea hali itazidi kua mbaya.

Hapa chini ni sababu zinazofanya Vyombo vya Habari kutetereka

1. Uwepo wa Sheria Kandamizi kwa Wanahabari na Vyombo vya Habari; Sheria kandamizi zimeendelea kuwa kikwazo katika utekelezaji na ufurahiaji wa uhuru wa kujieleza nchini Tanzania.

2. Tanzania imeporomoka kwa nafasi 25 katika orodha ya uhuru wa vyombo vya habari duniani. Tanzania imeporomoka hadi nafasi ya 118 kwa mwaka 2019 kutoka 93 mwaka 2018 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa tathmini.

3. kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwa mwandishi wa kujitegemea, Azory Gwanda. Kila Mwandishi anajipenda. Kuliko kufa, bora habari isiende hewani wanasema

4. kutimuliwa nchini kwa waandishi wawili wa Tume ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ), Angela Quintal na Muthoki Novemba 2018, kuliwatisha Waandishi na kuonekana wanaweza kufanywa lolote.

5. Adhabu Kali kwa Vyombo vya Habari; Kwa mwaka 2019 pekee, LHRC ilikusanya matukio mbalimbali ya vyombo vya habari kupewa adhabu ya kufungiwa na kulipa faini kubwa kubwa kwa madai ya kukiuka Kanuni za Maudhui ya Mtandao, ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kutoendana na viwango vya kimataifa vya uhuru wa kujieleza. Vyombo hivyo vya habari ni Gazeti la The Citizen, na televisheni za mtandaoni za Kwanza Online TV, Watetezi TV na Ayo TV. Hivi karibuni tumeshuhudia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikisimamisha gazeti la Mwananchi Mtandaoni kutochapa habari kwa miezi sita Wiki hii Clouds TV na Radio kufungiwa siku saba na Jahazi. Mara nyingi makosa yanayotumika kuvifungia na kuvipiga faini kubwa vyombo vya habari yamekuwa ni makossa ambayo yangeweza kurekebishwa na vyombo hivyo kuendelea na utendaji bila kufungiwa.

6. Ukamataji na Uwekaji Kizuizini wa Waandishi wa Habari kinyume na sheria; Matukio ya ukamataji wa waandishi wa habari kinyume na sheria kwa mwaka 2019 ni pamoja na tukio la ukamataji wa Erick Kabendera na Joseph Gandye. Kwa mujimu wa THRDC, katika kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba 2019, matukio 13 zaidi ya ukamati wa waandishi wa habari kinyume na sheria yaliripotiwa. Matuki haya na mengine yamekuwa yakitishia waandishi wa habari hasa wanaoandika habari zinazoibua changamoto za mamlaka na kuita uwajibikaji wa serikali na viongozi wake.

7. Waandishi wa Habari kujihusishana Siasa. Mfano Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2020, Waandishi wengi wa habari wamegombea vyama vya Siasa huku wakiwa ndani ya Vyumba vya habari. Hii inafanya habari nyingi za kisiasa kuwa za upande mmoja hasa upande wenye hela sio wenye haki.


8. Maadili ya Wamiliki na Waandishi wa Habari kuporomoka. Mwandishi wa habari siku hizi yupo tayari kumchafua mtu au kumpamba mtu kama amepewa hela kufanya hivyo.

9. Matamko ya wanasiasa. Mfano kuna mwanasiasa alisema, kama mlidhani mpo huru kwakusema lolote, kutafuta habari na kuzisambaza.......NOT TO THAT EXTENT

10. Wanasiasa kuvamia Vituo vya habari huku wamebebelea bunduki


Sababu zipo nyingi sana.

Ni wakati muafaka kwa Vyombo vya habari kujitathimini.

Imefika wakati vyombo vya habari kupingana kudai Uhuru wao na kupigia kelele Sheria Kandamizi.

Kama wataendelea kutengana, wote wataguswa na watazidi kushambuliwa wasipoungana.

Pole yao.
 
Umeandika vizuri na kuchambua vyema.

Bahati mbaya sana vyombo hivyo vya habari havipogo Tanzania, na havitakuwepo Tanzania ikiwa tutaendelea kuwa chini ya CCM.
 
Uchaguzi Dah, badala ya vitu kuwa ya chama na chama, inafikia polisi, media, NGOs, matokea yake Kuna upotevu mkubwa wa target
 
Back
Top Bottom