Wanachama 12 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamejitokeza kuomba kupitishwa kuwania ubunge wa Jimbo la Busanda wilayani Geita katika Mkoa wa Mwanza, Mei 24, mwaka huu. Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Busanda utafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Faustine Rwilomba aliyefariki dunia Machi 12, mwaka huu nchini India, ambako alikuwa amelazwa akitibiwa maradhi ya ugonjwa wa moyo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Geita, Rahel Ndegeleke alisema juzi kuwa kazi ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu ilikwenda vizuri kama ilivyopangwa na wanachama hao 12 ndio waliokamilisha taratibu. Ndegeleke aliwataja wanachama hao kuwa ni Sostenes Kurwa ambaye ni Mfamasia katika Mkoa wa Mwanza, Lolesia Bukwimba ambaye ni Meneja katika shirika lijulikanalo kwa jina la SEDA la Dar es Salaam ambalo linajishughulisha na utoaji wa mikopo kwa jamii.
Wengine ni aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo kuanzia mwaka 1995 hadi 2000, Ernest Kahindi ambaye alishindwa mwaka 2000 na Rwilomba. Kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo. Yumo Donald Max ambaye ni Mweka Hazina wa CCM wilayani Geita ambaye pia aliwahi kuwania ubunge katika Jimbo la Geita Mjini na kuangushwa na mbunge wa sasa, Ernest Mabina.
Wengine ni Lucas Bilie; Tumaini Magesa; Francis Misana; Sambili Mlingwa; Nicholaus Kasendamila; Abdallah Musa; Robert Kiganga na Jonathan Mpuya. Katibu wa CCM Wilaya alisema kura za maoni kwa ajili ya kumpata mgombea mmoja wa chama hicho katika uchaguzi huo zitapigwa Aprili 15, mwaka huu. Alisema utaratibu kwa ajili ya kumpata mgombea huyo ndani ya chama utakuwa ni ule uliotumika mwaka 2005.
Utaratibu uliotumika mwaka 2005 katika Uchaguzi Mkuu ndani ya CCM ni wa wajumbe wa mkutano wa jimbo kukusanyika kwa siku moja na kupiga kura za maoni juu ya mgombea wanayemtaka awanie nafasi ya ubunge ama udiwani. Juzi, NEC Taifa ya CCM ilileta mapendekezo ya kutumika kwa utaratibu mpya ambao wanachama wote wa CCM wa matawi watapiga kura katika jimbo husika.