JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,780
- 6,607
Uchambuzi Mahsusi wa Julius S. Mtatiro (Wakili) na Ally M. Kileo (Wakili) kuhusu Uchaguzi wa TLS
Watanzania na mawakili tumesikiliza na kufuatilia kwa kina, mjadala wa wazi uliorushwa na Star TV siku ya Jumamosi 27 Julai, 2024 ukiwahusisha mawakili mbalimbali waliopendekezwa kuwania nafasi ya juu ya URAIS wa Chama cha Mawakili Tanzania – Tanganyika Law Society (TLS). Sisi ambao tuko kwenye tasnia ya sheria, pia kwa muda mrefu tumepata wasaa wa kutosha wa kuwafuatilia wagombea mbalimbali wa nafasi husika, kwa sababu wamekuwa ni wenzetu kwa namna moja au nyingine. Tunawapongeza sana mawakili wote walioshiriki katika mjadala huo wa wazi na ambao wanaendelea na kampeni na tunawatakia kila la heri.Kwanza ni muhimu tuanze kwa kuwatambua mawakili hawa vinara; BONIFACE A.K. MWABUKUSI (MBEYA); CAPT. IBRAHIM MBIU BENDERA (ILALA); EMMANUEL AUGUSTINO MUGA (ILALA); REVOCATUS LUBIGILI KIBWE KUULI (MZIZIMA); PAUL REVOCATUS KAUNDA (WESTERN ZONE); na SWEETBERT NKUBA (KINONDONI).
Sisi Mawakili Julius Mtatiro na Ally Kileo, tumepata wazo la umuhimu wa kufanya uchambuzi kwa wagombea hawa ili kuongeza na kushajiisha mjadala unaoweza kusababisha TLS ikaendelea kupata viongozi bora watakaoendeleza kazi nzuri kwa mujibu wa sheria inayounda Chama hicho. Kipekee na kwa nia njema, tumeona tuelekeze uchambuzi wetu kwa wagombea ambao tunadhani wanaweza kuweka ushindani wa kipekee katika kinyang’anyiro cha urais wa TLS.
Hii ni kwa sababu, licha ya kuwa tunatambua umuhimu wa wagombea wote, lakini tunatumia uhuru wetu wa kichambuzi kunoa shabaha ya mielekeo halisi ya nani na nani wanaonekana wana nguvu dhahiri katika kinyang’anyiro hiki na wana nafasi ya kukwea katika nafasi ya juu kuliko wengine.
Wengi wetu tumejifunza kuwa, wagombea wote 6 waliofuzu ni wazoefu na wana sifa mbalimbali za kiuongozi. Kila mmoja ana sifa za kipekee tofauti na wenzake na kila mmoja akiwa na uzoefu wa kipekee ambao si lazima ufanane na mwingine, na kwa hiyo ni wazi kuwa kila mgombea anaweza kuleta mabadiliko fulani au matatizo fulani atakavyopata nafasi ya kuhudumu urais wa TLS.
Kabla hatujafanya uchambuzi huu tulikuwa na maswali mbalimbali vichwani mwetu, ambayo tutayatumia kama msingi wa kile kinachoweza kutokea TLS na mwelekeo wake kwa siku zijazo. Maswali hayo ni pamoja na;
Je, TLS inahitaji Rais wa namna gani kwa muktadha wa sasa wa nchi yetu?
Je, mawakili, na hasa mawakili vijana wana matarajio gani na Rais wa TLS ajaye?
Je, TLS inaweza kujifunza mamnbo gani kutoka Pan African Lawyers Union (PALU) na Black Lawyers Association (BLA)?
Sera na ujiendeshaji kama huu wa PALU na BLA zinahitaji viongozi gani kuzisukuma kwa muktadha wa TLS?
Je, ukiwachambua mawakili wote ambao wanagombea urais wa TLS, ni wagombea gani miongoni mwao wanaonekana wana ushawishi, na kwa nini?
Je, miongoni mwa hawa wenye ushawishi mkubwa, ni nani anaweza kuiongoza TLS kwa mafanikio zaidi kuliko mwenzake? Kwa nini?
Misimamo na mitazamo ya washindani wakuu ina tija yoyote ndani ya TLS? Ni nani anaweza kuiongoza TLS kwa mafanikio zaidi?
Je, TLS inahitaji Rais wa namna gani kwa muktadha wa sasa wa nchi yetu?
Ni wazi kwamba, Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), kwa sasa kinahitaji Rais ambaye haji kujianzishia tu mambo yake vile atakavyo, kinahitaji Rais ambaye atakuja kuendeleza na kuweka mkazo kwenye mambo muhimu na mazuri (misingi) iliyowekwa na watangulizi wake, yaani Mawakili Profesa Edward Hosea na Harold Sungusia ambao wamefanya majukumu yao hivi karibuni – pamoja na kurekebisha maeneo ambayo hayakufanyika vizuri, bila kusahau kujenga uwezo wa kuwaunganisha mawakili.TLS ni Chama cha kitaaluma kinahitaji Rais mtendaji, mweledi, mtulivu, mwenye uwezo wa kushawishi wadau wote wa sheria ndani ya nchi, mwenye maono yanayoweza kutekelezeka bila papara. Atakayeweza kuwaunganisha mawakili wote, atakayekua kiungo muhimu kati ya TLS na mdau mkuu ambaye ni Serikali, na ambaye hatogeuka kuwa “msanii na mpiga kelele”, kueneza chuki kwa misingi ya uanaharakati, utofauti wa ufuasi wa vyama vya siasa, mihemko na jazba.
TLS inahitaji mtu mwenye visheni na busara za kutosha, ambaye anaweza kukisaidia Chama cha Mawakili kutekeleza majukumu yake katika hali ya utulivu na ufanyaji maamuzi wa pamoja na wenye tija.
Je, mawakili, na hasa mawakili vijana wana matarajio gani na Rais wa TLS ajaye?
Mawakili vijana, kama ilivyo kada ya vijana dunia nzima, wana matarajio ya kuona mabadiliko ya haraka katika maeneo muhimu wanayoyatarajia. Lakini mawakili hao wanahitaji washauri na waongozi wazuri, wanahitaji kujengewa utulivu na uwezo wa kuyaona masuala katika dhana pana ambayo inaweza kuwajenga na kuwafanya wawe mawakili wa kipekee siku za mbeleni.Mawakili vijana wanazo ndoto muhimu, wanayo matamanio ya kuona na wao wanalelewa na kukuzwa ili kufikia mipango yao. Mawakili vijana wengi hawana ofisi, wengi wanafungua kampuni za uwakili ambazo zinaongezeka ukubwa kwa hatua sana na wengi wanakata tamaa kwa sababu sekta ya sheria Tanzania na duniani kote imekua sana, imeongeza ushindani wa ndani uliopitiliza na ina changamoto zake. Kwahiyo changamoto hizi zinapaswa kutatuliwa au kuwekewa misingi itakayopelekea huko tuendako vijana wapya katika taaluma hii muhimu waweze kujisimamia na kusimama wenyewe.
Kimaadili pia, mawakili vijana wanayo dhima na wajibu wa kujifunza maadili na mienendo bora inayokubalika katika utekelezaji wa majukumu yao ya kiuwakili kama inavyoelezwa katika sheria na kanuni mbalimbali za maadili ikiwemo Kanuni za Maadili za Mawakili za Mwaka 2022.
Je, TLS inaweza kujifunza kitu kutoka PALU na BLA?
Katika kuitafakari TLS, tuliona tuweke uzoefu wa namna baadhi ya vyama vya mawakili duniani vinavyojiendesha, hasa eneo la kazi zake, utaratibu wa kufanya kazi hizo na wadau wake wakuu. Tunaweza kuchukua mifano ya PALU au Black Lawyers Association BLA. Unapofuatilia kwa kina yanayofanyika kwenye vyama hivi unagundua kuwa hivi ni vyama vinavyotoa taswira halisi kuhusiana na kazi kubwa inayofanywa kimkakati na kitaaluma kwenye tasnia ya sheria.Vyama hivi vimekuwa machampioni wa kuweka mkazo katika mabadiliko na masuala ya haki za binadamu na vinafanya kazi nzuri kwa karibu na serikali mbalimbali duniani bila kuviweka mbali vyombo vya haki vya kimataifa kushawishi na kutengeneza miswada inayoweza kuwa sheria kwa ajili ya kukuza haki na usawa duniani.
Vyama hivi vinatoa msaada wa kisheria kwa uzito kwa jamii ambazo hazijafikiwa ipasavyo na kuondoa matabaka yanayoweza kujitokeza. Vinatoa mafunzo na kozi mbalimbali kwa mawakili ili kuwajengea uwezo waweze kufanya kazi zao kitaaluma na kwa mafanikio.
Vimekuwa vinaingilia mashauri yenye maslahi mapana ya kitaifa, kuongeza changamoto kwa kukaa chini na serikali na vyombo vya sheria ili kushawishi mabadiliko mbalimbali katika masuala hayo na tasnia ya sheria, kimkakati na kwa utulivu na bila kuvunja uhusiano wake na serikali. Vyama hivi pia vimekuwa vikifuatilia mwenendo wa demokrasia na utawala bora na kuwaleta wadau mbalimbali wa sheria mezani hasa serikali na vyombo vyake, ili kutatua changamoto zilizoko kwa utulivu na maelewano. Haya yote yamekuwa yakifanywa kwa kuihusisha serikali na vyombo vyake vya kisheria kwa asilimia mia moja.
Sera na uendeshwaji wa PALU na BLA - Wanahitajika viongozi wa aina gani kwa muktadha wa TLS?
TLS ni Chama cha Kisheria (A statutory association), kilichoanzishwa mwaka 1954 kwa Sheria ya Bunge inayojulikana kama “The Tanganyika Law Society Ordinance 1954”. Kwa sasa, TLS inajiendesha kupitia Sheria iliyotungwa na Bunge inayojulikana kama Tanganyika Law Society Act, [Cap. 307 R. E, 2002]. TLS inayo malengo yake makuu yanayotajwa katika kifungu cha 4 cha sheria inayounda chama hicho.Malengo haya yanafanana sambamba na PALU na BLA. Hata hivyo katika kutekeleza na kufanikisha malengo haya ya TLS kama zilivyo PALU na BLA, mdau wake mkubwa ni Serikali
na vyombo au mamlaka mbalimbali za haki. Mdau wake mwingine mkuu ni Mahakama kwasababu mawakili ni maafisa wa mahakama kabla ya kitu kingine chochote. Kwa muktadha huu wa TLS, kunahitajika viongozi wenye ushawishi wa kisera na kimawazo kwa serikali na mahakama, ili viongozi hao wawe na uwanda mpana wa kufanya kazi na mamlaka hizi muhimu na zingine kwa maslahi mapana ya mawakili.
Mstari wa TLS kuelekea mahakamani na serikalini unapokatika au kuyumba, si rahisi mawakili peke yetu na chama chetu kufikia yale malengo tuliyojiwekea, kwani hatuishi ndani ya kisiwa peke yetu.
Je, ukiwachambua mawakili wote wanaogombea nafasi ya kiti cha urais wa TLS, ni nani miongoni mwao wanaoonekana wana ushawishi, kwa nini?
Baada ya ufuatiliaji na uchambuzi wa kina, kati ya wagombea wote waliojitokeza kwenye nafasi ya kiti cha Urais TLS, Mawakili BONIFACE A.K. MWABUKUSI (MBEYA) na SWEETBERT NKUBA (KINONDONI) wanaonekana kuwaa na ushawishi zaidi miongoni mwa wapiga kura mawakili. Tunatumia fursa hii kuwafanyia uchambuzi mawakili hawa, ambao miongoni mwao, mmoja wao ana nafasi ya kuwa Rais wa TLS.Lakini kipekee na si kwa ushabiki tutatoa maoni yetu juu ya ni nani miongoni mwao anaweza kuwa Rais Bora wa TLS ambaye atasimamia ndoto za mawakili walio wengi, hasa mawakili vijana ambao ndiyo kwanza wanajiwekea misingi – ikiwa ni pamoja na kusimamia mielekeo ya vyama vya mawakili vinavyofanya vizuri ngazi ya kimataifa, vya PALU na BLA kwa muktadha wa TLS.
Kwa nini Wakili BONIFACE A.K. MWABUKUSI ana ushawishi?
Wakili Mwabukusi ni Wakili Mwandamizi ambaye amewahi kuwa mtumishi wa serikali ya Tanzania kabla ya kuamua kuwa wakili binafsi. Hivi karibuni amekuwa akijijengea umaarufu kwa sababu ya misimamo yake mikali dhidi ya serikali, mamlaka mbalimbali za nchi pamoja na kupinga mara kwa mara mwenendo wa mahakama ya Tanzania.Kwa sababu hiyo, lipo kundi la vijana ndani na nje ya tasnia ya sheria linaloamini kuwa TLS inahitaji mtu atakeyeendesha mapambano ya kutosha dhidi ya serikali na mahakama kwani Mwabukusi anao uwezo wa kutamka lolote, muda wowote na bila kujali chochote. Anajiamini kupita kiasi na ana uwezo wa kufanya lolote bila kujali mamlaka zilizopo.
Katika mdahalo wa hivi karibuni uliorushwa na Star TV kutokea ukumbi wa maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, Wakili Mwabukusi ameweka wazi kuwa atakapokuwa Rais wa TLS atashawishi na kulazimisha mabadiliko katika sera, hali, na sheria mbalimbali hata kama ni kwa kutumia nguvu ya maandamano n,k.
Wakili Mwabukusi amekua mara nyingi akisisitiza kwamba haki haiombwi bali hudaiwa ikiwezekana hata kwa kutumia nguvu. Misimamo hii ni miongoni mwa sababu zinazomfanya apate ufuasi ndani na nje ya tasnia ya sheria hususani kutoka makundi ya vijana. Mwabukusi na kampeni zake kupitia vyombo kadhaa vya Habari ikiwemo na mitandao ya kijamii, anapata ufuasi kwa sababu amejipambanua kwa dhati kama mtu anayeamini kuwa uhusiano na
ufanyaji kazi wa TLS na serikali na mahakama, ni janga lisilokubalika. Huo ni mtego ambao unaweza kuifanya TLS isifikie malengo ya mawakili na kwa hiyo anaamini kuwa TLS ya ndoto zake ni ile ambayo itakaa upande mmoja, kisha serikali ikae upande wake na mahakama ikae kwake kisha wadau hawa watatu waanze mapambano. Mwabukusi katika hotuba zake amekuwa akisisitiza na kuongea kwa jazba kuwa hajawahi kushindwa na hamwogopi mtu yeyote yule.
Amekua akijinasibu mara zote mbele ya umma kuwa anayo imani zaidi ya ushindi na siyo majadiliano, maridhiano au makubaliano. Kauli na matamko ya namna hii mara nyingi, huzaa na kujenga ufuasi mkubwa miongoni mwa wana jamii hususani vijana kutokana na mchanganyiko wa changamoto kadhaa za kimaisha zinazowakabili ikiwemo udogo-udogo wa shughuli za kiuchumi na ukosefu wa ajira za uhakika. Mwelekeo wa namna hii kwa kawaida na msingi wake ni mlipuko na mhemko ambao baadaye huleta majuto.
Misimamo na mwelekeo wa Mwabukusi una tija yoyote ndani ya TLS?
Kwa uchunguzi na uchambuzi wa kina tulioufanya, tunajiridhisha na kuamini kuwa misimamo na mwelekeo wa Wakili Mwabukusi hautokua na tija ya aina yoyote kwa kipindi chote cha miaka mitatu endapo atapata fursa ya kuwa Rais wa TLS. TLS ni chombo cha kisheria na kinajiendesha kwa mujibu wa sheria na vikao.Mwelekeo huu wa Wakili Mwabukusi unamaanisha kuwa TLS itageuzwa kuwa uwanja wa mapambano ya siasa kali badala ya kuwa uwanja wa majadiliano, ushawishi, maridhiano, uunganishaji wa wadau (serikali na vyombo vyake kwa upande mmoja na mahakama kwa upande mwingine). Matamko na misimamo mikali ya wakili Mwabukusi ingeweza kuwa na tija kubwa endapo chama cha TLS kingelikuwa ni Chama kilichosajiliwa na msajili wa vyama vya siasa Tanzania kuwa na malengo makuu ya kushiriki siasa ndani ya nchi.
TLS sio chama cha Siasa. TLS hakikusajiliwa kwa mujibu wa sheria ili kushindana kwenye ulingo wa siasa na vyama vingine vya siasa au kupambana na serikali au kujenga hoja za kimapambano ili kipate uungwaji mkono.
TLS imeundwa kwa ajili ya kulinda na kusaidia wananchi kuhusiana na mambo ya kisheria kwa njia halali za kisheria. Lakini inao wajibu mkubwa na wa kwanza kuwakilisha, kulinda na kusaidia na kusimamia ustawi na maslahi ya wanachama wake. Kwahiyo, mtu yeyote anayetaka kuiongoza TLS anapaswa atuletee maono yenye uthabiti na ushawishi wa kisheria na kimantiki, ili tuwe na uhakika kwamba huyu tukimpa nafasi hii, atasimamia maslahi na ustawi wa wanachama na kuwa muunganishaji na daraja zuri la mawakili kuifikia serikali na vyombo vyake, vilevile mahakama na ngazi zake. Kinyume na hapo, sarakasi za matamko ya mitaani, jazba, vurumai, hekaheka za kisiasa na matamko ya kisiasa, haviwezi kuwa sehemu ya TLS ile iliyoundwa kwa mujibu wa sheria na ambayo inajikuza ili kujenga mawanda ya utendaji kazi ya PALU na BLA.
Kwa nini Wakili SWEETBERT NKUBA ana ushawishi kuiongoza TLS 2024-2027?
Kama ilivyo kwa mwenzake, Wakili Sweetbert Nkuba ni Wakili Mwandamizi ambaye amewahi kuwa mtumishi wa serikali ya Tanzania kabla ya kuamua kuwa wakili binafsi. Nkuba amekuwa mwanaharakati na kiongozi wa ngazi ya juu katika safari mbalimbali za maisha yake na alifikia hata kuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi, alipokuwa Chuo Kikuu.Wakili Nkuba katika matamko na mielekeo yake mbalimbali kwa TLS, amejipambanua wazi kuwa anakwenda kuwa Rais wa TLS, kwanza kuanzia pale walipoishia watangulizi wake mbalimbali, lakini akiweka mkazo kwenye eneo la kuimarisha mahusiano ya kimsimamo kati ya TLS na Mahakama na Serikali ili mahusiano hayo yawe chachu ya upenyezaji wa ushawishi na ajenda mbalimbali ambazo ni kilio cha mawakili, na hasa mawakili vijana.
Wakili Sweetbert Nkuba anaamini serikali na mahakama ni wadau wasiokwepeka, na kwamba TLS haiwezi kamwe kufanya kazi peke yake kwa kujifungia na kazi hizo zikafanikiwa. Wakili Sweetbert Nkuba anaamini kuwa TLS siyo jukwaa la kuendeleza malumbano na mapambano ya kisiasa, na badala yake ni jukwaa la kisheria linalojiendesha kwa vikao na mipango ya ndani iliyojaa utulivu na ushawishi wenye misimamo.
Katika hotuba zake Wakili Sweetbert Nkuba amejipambanua kama kiongozi aliyetulia, mwenye maono Chanya na mwenye kiu na ndoto kwamba TLS inaweza kusonga mbele na kuwa sehemu ya mabadiliko muhimu ya kisera, kisheria, kikatiba n.k masuala ambayo yameonekana kuwa kipaumbele muhimu katika Serikali ya Awamu ya Sita.
Kwa sababu hizi na nyingine, Nkuba amejenga ufuasi kutoka kwa wapiga kura wanaoamini kuwa TLS ili ishawishi mabadiliko mbalimbali yanayolinda hadhi na tasnia ya sheria na mawakili nchini Tanzania, inahitaji utulivu na shabaha halisi zitakazotekelezwa kimkakati na kwa dhana ya kutambua kuwa serikali na mahakama ni washirika muhimu katika michakato ya TLS.
Misimamo na mwelekeo wa Nkuba una tija yoyote ndani ya TLS?
Tunaamini kuwa, mwelekeo na msimamo wa Nkuba unaweza kuwa na tija ndani ya TLS. Ukweli ni kwamba TLS siyo jukwaa la mapambano ya barabarani, siyo eneo la vita wala siyo eneo la kushughulikiana na watu, serikali au mahakama.TLS ni chombo kinachoheshimika sana, ni jukwaa la kisheria linalopaswa kukaliwa na watu wanaofikiri sawa sawa, kwa ujasiri na utulivu, watu wanaoamini kuwa ni lazima wafanye kazi na wadau wengine bila kutukanana na kupambana ili wafikie malengo ya pamoja ya nchi – kwa sababu malengo hayo siyo ya mtu mmoja au kundi moja.
Wakili Nkuba ni mfano halisi wa kiongozi kijana, mtulivu, mwenye maono na anayeamini katika misingi ya ndoto zilizofikiwa na PALU na BLA, ambazo TLS inaweza kuzifikia kirahisi ikijiwekea malengo.
Ni kijana kiongozi anayeamini kuwa uongozi ni ajenda za pamoja, uongozi ni ushirikishaji na ushirikishwaji, na uongozi ni vile ambavyo kiongozi anajiweka miongoni mwa wenzake ili kulinda maslahi yao na kuheshimu maslahi ya kisheria ya mamlaka zingine.
Je, ni Mwabukusi au Nkuba? Ni nani anaweza kuiongoza TLS kwa mafanikio zaidi kuliko mwenzake? Kwa nini?
Tukiwa ni mawakili ambao ni sehemu ya TLS tuna uhakika asilimia mia moja kuwa, Nkuba atakuwa ni Rais bora zaidi wa TLS kuliko Mwabukusi. Sehemu ya uchambuzi huu imegusia kwa kina ni namna gani wawili hawa wana uwezo wa namna gani na wanaweza kuwa Marais wa namna gani.
Ni wajibu wetu kuyasema haya kwasababu hiyo ni njia ya kufumbua macho ya kila mmoja wetu ili mwisho wa siku kila kura itakayopigwa iwe kura ya mfano, yenye kuleta TLS inayohitajika katika muktadha wa wakati wa sasa na TLS inayoweza kujifunza na kujitengeneza kuwa PALU na BLA siku zijazo.
KUHUSU WACHAMBUZI:
Wakili Julius S. Mtatiro ni Mwanachama wa TLS, ana uzoefu wa uongozi ndani na nje ya serikali na katika vyama vya siasa. Mtatiro ni msomi mwandamizi mwenye Shahada ya Sanaa ya Elimu (BAED), Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Umma (MPA), Shahada ya Uzamili ya Sera za Umma (MPP), Shahada ya Sheria (LLB), Stashahada ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo (PGD in Legal Practice), Cheti cha Juu cha Fasiri na Ukalimani (ACTIS), Cheti cha Juu cha uongozi (CoL) na ni Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD). Mtatiro ni Kiongozi Mwandamizi na Mchambuzi wa Masuala ya Kitaifa na Kimataifa. +255787536759 (juliusmtatiro@gmail.com).Wakili Ally M. Kileo, Esq ni Wakili Mwandamizi na Mwanachama wa TLS na EALS. Ni Mkurugenzi Mwanzilishi wa Kampuni ya Sheria ya MDM Law Group yenye Makao yake Makuu jijini Dar es salaam. Ana uzoefu mkubwa wa utendaji kazi ndani ya serikali na katika sekta binafsi. Ana Shahada ya Uzamili kwenye Sheria za Makampuni na Biashara (LL.M in Corp & Commercial Law), Stashahada ya Uzamili ya Uandishi na Mawasiliano ya Umma (PGD in Mass-Comm), Shahada ya Sheria (LLB), Stashahada ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo (PGD in Legal Practice), Shahada ya Komputa kwenye Biashara (Bsc in Applied Business Computing). Pia ni Mshiriki wa Shahada ya Uzamivu (PhD). Wakili Ally M. Kileo pia ni Mwandishi Mahiri wa kitabu cha “Comprehensive Issues of Employment & Labor Law: Practice for Modern Business in Tanzania” ambacho kimejenga msingi mkubwa wa taaluma ya sheria katika eneo la biashara, ajira na mahusiano kazini. +255787630150 (kileoally@yahoo.com).