KERO Ucheleweshaji wa Pasipoti: Changamoto na Maswali Yasiyojibiwa

KERO Ucheleweshaji wa Pasipoti: Changamoto na Maswali Yasiyojibiwa

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
A

Anonymous

Guest
Ucheleweshaji wa Pasipoti: Changamoto na Maswali Yasiyojibiwa

Mnamo tarehe 23 Septemba 2024, nilikamilisha hatua ya kwanza ya maombi ya pasipoti ya kawaida kwa kujaza fomu namba 24ER-Y091-Q020 na kuwasilisha viambato vyote vya msingi na ziada kwa njia ya mtandao, kisha kulipa shilingi 20,000/- za Kitanzania kama ada ya huduma. Siku iliyofuata, tarehe 24 Septemba 2024, nilikamilisha taratibu zote ikiwa ni pamoja na kuambatanisha fomu na viambato vya msingi kama vile nakala ya cheti cha kuzaliwa, kitambulisho cha Taifa (NIDA), kiapo cha mahakama cha mzazi mmoja, pamoja na barua ya maombi na kiambato cha ziada cha barua ya utambulisho kutoka serikalini ya mtaa.

Nilifuata taratibu zote kwa mujibu wa muongozo wa huduma ya pasipoti, ambapo baada ya ukaguzi wa fomu na viambato vyangu, nilijulishwa kuwa taarifa zangu zilikuwa kamili. Hivyo, niliendelea na hatua inayofuata ya kufanya mahojiano na Afisa Ernest Maganga. Baada ya mahojiano, nilifanya hatua ya kupiga picha na kufanya uthibitisho wa alama za vidole. Nilitarajia kuwa baada ya kumaliza taratibu zote, ningepokea pasipoti yangu katika kipindi cha siku 7 hadi 14 kama ilivyoelekezwa kwenye muongozo. Hata hivyo, nilijulishwa kuwa kulikuwa na changamoto za kiufundi, hivyo nikaelekezwa kurudi baada ya mwezi mmoja na wiki mbili, yaani tarehe 14 Novemba 2024.

Ilipofika tarehe 14 Novemba, nilifika ofisi za uhamiaji nikiwa na matumaini ya kupokea pasipoti yangu, lakini nilishangazwa na taarifa kwamba fomu yangu haikuchakatwa kwa sababu ya kipengele kimoja ambacho sikukamilisha, licha ya kuwa fomu ilikuwa imekaguliwa na mahojiano kufanyika mwezi mmoja na wiki mbili kabla. Baada ya kuelekezwa, nilikamilisha kipengele hicho kupitia mwanasheria wangu na kuirudisha tena fomu pamoja na viambato vyote ofisi za uhamiaji Kurasini. Nilijulishwa kwamba pasipoti yangu ingekamilika na kuwa tayari tarehe 22 Novemba 2024 na ningeenda posta, wizara ya mambo ya ndani kuichukua.

Ilipofika tarehe 21 Novemba 2024, nilipokea simu kutoka kwa namba 0784520840 iliyonijulisha kuwa pasipoti yangu bado haipo na kwamba nilipaswa kuleta matokeo yangu ya chuo pamoja na barua nilipojaribu Kuhoji alinikatia simu na toka hapo nikipiga simu haipokelewi. licha ya kuwa nikiwa katika hatua ya ukaguzi wa fomu, sikujulishwa kuhusu uhitaji wa taarifa hizo za ziada.

Maswali ya Kujiuliza:

1. Kwa nini taarifa za ziada na maboresho zilikuwa hazijafahamika miezi miwili nyuma, wakati nikiwa katika hatua ya ukaguzi wa fomu na mchakato wa mahojiano?kwani ingeweza kunisaidia kukamilisha mchakato wa maombi kwa wakati.

2. Kwa nini maafisa wa uhamiaji wanatupia lawama zote kwangu kwa makosa ambayo wao ndio waleyasababisha au kuyatengeneza? Ingawa niliwasilisha fomu na viambato vyote kwa usahihi, bado nashindwa kuelewa kwa nini nilikosa kupewa taarifa muhimu ambazo zingenisaidia kupunguza ucheleweshaji.

Kwa sababu ya ucheleweshaji huu wa pasipoti kwa miezi miwili, nilikosa ufadhili wa safari ya utalii wa nje baada ya mdhamini wangu kusitisha kwa kutozingatia kwangu muda (deadline). Hali hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa na ucheleweshaji wa pasipoti yangu, ambao ulileta athari kubwa katika mipango yangu ya safari.

Ushauri:

1. Kutengeneza Mfumo wa Ufuatiliaji wa Maombi: Mfumo huu uwape uwezo wateja kufuatilia hatua za uchakatwaji wa maombi yao ya pasipoti. Hii itasaidia kujua hali halisi ya ombi lao, nyaraka zilizokosekana, na maboresho yanayohitajika.

2. Masharti na Hatua Muhimu Ziwekwe Wazi na Kwa Wakati: Kueleza kwa uwazi taarifa zilizokosekana na maboresho yanayohitajika katika hatua ya ukaguzi wa fomu na mahojiano.

3. TAKUKURU na Wadhibiti Ubora kafanye kazi yao.
 
Back
Top Bottom