Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Nitajitahidi kutafuta kwenye hifadhi za kumbukumbu,
Mshume Kiyate inafahamika wazi kuwa alikuwa rafiki wa karibu na mzee, nitajitahidi kupata picha zao pia.
Kwa kuwa umekubali kuwa Mshume Kiyate alikuwa ''rafiki wa karibu'' wa baba yako nakuwekea hapa kisa cha Mshume Kiyate na Julius Nyerere.
Nakuwekea hapa kwa kuwa naamini baada ya kusoma utachukua juhudi kuwaeleza wakubwa wampe heshima yake rafiki wa baba yako na wabadilishe kibao cha Mtaa wa Tandamti kisomeke ''Mshume Kiyate.''
Kifuatacho ndicho kisa chenyewe ambacho Nyerere alikipa jina ''the TANU spirit:''
Mwalimu Nyerere siku moja akizungumza na Dossa Aziz, Lucy Lameck, na Ahmed Rashad Ali katika kukieleza kile alichokiita ''the TANU spirit'' yaani ghera ya wana TANU alisema kuwa siku moja wakati wa kudai uhuru alikuwa anatoka nyumbani kwake Magomeni akija Kariakoo kwa miguu akielekea sokoni kutafuta mahitaji yake, lakini mfukoni alikuwa hana hata senti moja.
Njiani akakutana na Mzee Mshume Kiyate. Alipomuuliza anakwenda wapi, alimfahamisha kuwa anakwenda sokoni lakini hana fedha za kununua chochote. Mzee Mshume aliingiza mkono katika koti lake akatoa shilingi mia mbili akampa. (Ukitaka kujua thamani ya fedha ikutoshe tu kuwa wakati ule inasemekana nyumba ya vyumba sita kujenga Kariakoo ilikuwa inagharimu shilingi mia tano).
Kutokana na hali hii Mshume Kiyate aliona itakuwa ni kumtwisha Nyerere mzigo ikiwa atakuwa anashughulika na kuwatafutia wanae chakula na wakati huo huo anafanya kazi za TANU. Mzee Mshume akajitolea kuihudumia nyumba ya Nyerere kwa chakula.
Alifanya hivyo hadi uhuru ulipopatikana. Baada ya uhuru Nyerere alimwomba Mzee Mshume aache kufanya hivyo lakini alikataa na akamtafadhalisha Nyerere aendelee kula chakula chake na kile ambacho kinatolewa na serikali kwake yeye kama mkuu wa nchi alimuomba Nyerere awape wageni wake.
Mzee Mshume alifanya mengi katika kudai uhuru na baada yake. Baada ya maasi ya wanajeshi wa KAR tarehe 20 Januari, 1964, kuzimwa na Jeshi la Kiingereza, TANU ilifanya mkutano mkubwa sana Jangwani.
Mzee Mshume kwa niaba ya wazee wa TANU alipanda jukwaani na kumvisha Nyerere kilemba kama ishara ya kumuunga mkono. Picha ya mzee Mshume akimvisha Nyerere kilemba ilichapishwa katika magazeti mengi.
Halikadhalika picha nyingine mashuhuri ya Mzee Mshume na Nyerere ni ile iliyopigwa Novemba 1962 wakati wa Uchaguzi Mkuu. Picha hiyo inamuonesha Mzee Mshume akiwa amevaa koti, kanzu na kofia amemshika Nyerere mkono akimsindikiza kupiga kura.
Magazeti ya Chama na Serikali - Uhuru na Daily News yamekuwa yakiitumia picha hii kila baada ya miaka mitano katika uchaguzi wa rais kama njia ya kuwahamasisha watu kupiga kura na kumchagua Nyerere.
Kwa bahati mbaya si chama wala magazeti hayo yamekuwa na ujasiri wa kuandika maneno chini ya hiyo picha kueleza lini picha hiyo ilipigwa na huyo aliyekuwa kwenye picha na Nyerere ni nani.
Mwaka 1995 watu wa Dar es Salaam walipoamua kuubadilisha jina mtaa aliokuwa akiishi Mshume Kiyate, Mtaa wa Tandamti na kuuita ''Mtaa wa Mshume Kiyate'' kwa kuthamini mchango wake katika kupinga ukoloni, wanasiasa wageni, wasiojua mchango wa Mzee Mshume na baadhi ya magazeti yanayomilikiwa na Wakristo walitia dhana kuwa kilichowasukuma watu wa Dar es Salaam kufanya hivyo ni udini.
Kitu cha kusikitisha ni kuwa wakati magazeti yanapinga hatua hiyo si chama wala Nyerere rafiki yake aliyetetea jina la Mzee Mshume kwa kusema kuwa alikuwa anastahili heshima hiyo.
Kama wahusika wanavyotishwa na kueleza Abdulwahid Sykes alikuwa na mchango gani katika historia ya Tanganyika, vivyo hivyo wahusika wanaogopa kumueleza Mzee Mshume alikuwa nani.
Abdulwahid akiwa Market Master soko la Kariakoo na Mzee Mshume akiwa mmoja wa wauza samaki pale sokoni, pamoja walifanya mengi kuhamasisha harakati na kupata michango kutoka kwa wauza biashara wa pale kuijenga TANU.
Hadi kitabu hiki kinachapishwa kwa mara ya kwanza katika lugha ya Kiingereza mwaka 1998 kibao cha kuutambulisha mtaa ule kwa jina la Mshume Kiyate hakijawekwa. Kisa hiki kwa mara ya kwanza kabisa kilihadithiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Ditopile Mzuzuri Mkiwaona kada wa Chama Cha Mapinduzi.
Ditopile alikieleza kisa hiki kama alivyokieleza Nyerere kwa nia ya kuonyesha "moyo wa TANU." Kwa bahati mbaya waandishi wa magazeti wakapotosha kisa kizima.
Badala ya kutoa umuhimu kwa moyo wa ukarimu wa Mzee Mshume na kumuueleza kama mzalendo aliyejitolea katika kupigania uhuru, magazeti yakageuza maneno ya Ditopile kuwa masimango kwa Nyerere, yaani alikuwa akilishwa chakula bure.
Kwa ajili hii nafasi ambayo ingeliweza kutumiwa ili kueleza umuhimu wa Mzee Mshume ikapotezwa.
Kisa kingine cha kueleza "moyo wa TANU" ambacho Mwalimu Nyerere amepata kukieleza ni kile alichomueleza marehemu Profsesa Malima. Nyerere alikuwa anazungumza na Profesa Malima nyumbani kwake na katika mazungumzo Nyerere akamsikitikia Profesa Malima kuwa kuna watu wanamshutumu yeye kuwa hawapendi Waislam.
Nyerere alinyanyuka alipokuwa amekaa na kwenda chumbani kwake akatoka na moja ya picha za wakati wa kudai uhuru, akamuonyesha Malima. Nyerere akasema ''Profesa unaona picha hii, Waislam watupu, Mkristo ni mimi peke yangu, vipi mimi leo niwachukie watu walionifikisha hapa?''
Naamini hutakichukulia hiki kisa cha mapenzi, hisani, utu, huruma na wema baina ya baba yako na Mzee Mshume Kiyate kama ''ngano'' nyingine ya Mohamed Said. Bahati mbaya sana Mshume Kiyate amekufa na kuzikwa Nyerere hana taarifa na hakupata kusikika hata siku moja kumtaja, hata pale magazeti yalipokuwa yakipinga majina ya baadhi mitaa ya Dar es Salaam kupewa majina ya mashujaa wa uhuru, wazalendo wa Dar es Salaam, Nyerere hakusema lolote kuwaadhimisha wazalendo hawa kwa yale waliyofanya wakati wa kudai uhuru.
*Ahmad Rashad Ali ni yule niliyemtaja katika moja ya post zangu kuwa mwaka 1950 alikuwapo Nairobi Abdulwahid Sykes alipofanya mazungumzo na Kenyatta.