Cheif Thomas Marealle Paramount Chief.
Anatokea Marangu.
Rafiki wa Abdulwahid Sykes.
Rafiki yake Ally Sykes.
Abdu Sykes akimtania Chief Thomas Marealle.
Akimwambia,'' Unajua Tom kwa nini wewe Waingereza
wanakuita ''Chief'' hawakuiti ''King?''
Abdu alikuwa anaendelea na kumwambia, ''Waingereza
wanaona wakikuita wewe ''King'' utafanana na Mfalme
George.''
Wote wataangua kicheko.
Hata hivyo siku zote Abdu alikuwa akimuita Chief Marealle ''King
Thomas Marealle.''
Siku moja nimekutana na David Marealle.
Tukiishi jirani lakini hatukuwa na mazoea.
Siku tulipopata wasaa wa kuzungumza akanambia.
Alipokuja Dar es Salaam kwa mara ya kwanza alipokewa
na Abdulwahid Sykes.
Alitoa sifa nyingi sana za shukurani nami nikamfahamisha kuwa
huyo mie ni mzee wangu.
Sasa kabla hatujakwenda mbali sana nakuwekea hapa kitu ustaladhi nacho
Insha Allah:
Shukurani
''...kazi hii isingewezekana kama isingekuwa kwa msaada wa hali na mali nilioupata toka kwa Ally Sykes.
Ally Sykes alinipa wasaa wa kuzungumzanae kila nilipotaka, akanieleza madhila ya ukoloni pamoja na kuwa ni mtu wa shughuli nyingi.
Yeye hivi sasa anaendesha biashara yake toka ofisi yake iliyoko katikakati ya mji wa Dar es Salaam.
Aliniruhusu nisome majalada yake binafsi, barua zake, shajara na kumbukumbu nyinginezo za ukoo wa Sykes.
Ally Sykes alinifahamisha kuwa kumbukumbu hizi zilikuwa ndani ya sefu ambayo haikupatwa kufunguliwa kwa zaidi ya miaka therathini.
Nikiyapitia majalada yake nilishangazwa na utaratibu wa Ally Sykes wa kupanga kila kitu na kila kipande cha habari mahali pake hata kingekuwa kidogo namna gani wakati ule wa harakati.
Ally Sykes ana barua ya mwaka 1954 iliyoandikwa kwa penseli toka kwa Zuberi Mtemvu kwenda kwake akimtaarifu juu ya mazungumzo aliyokuwanayo (Mtemvu) na Nyerere kuhusu yeye na TANU; stakabadhi ya hundi ya posta toka kwa Ally Sykes kwenda kwa Japhet Kirilo wakati wa Mgogoro wa Ardhi ya Wameru.
Nakala ya barua isiyokuwa na tarehe kutoka TAA kwenda kwa Malkia Elizabeth iliyotiwa saini na viongozi wote wa TAA:
Rais Julius Nyerere, Makamu wa Rais Abdulwahid Sykes, Katibu Mkuu Dome Okochi, Naibu Katibu Dossa Aziz, Mweka Hazina John Rupia, Naibu Mweka Hazina Ally Sykes ikimpongeza Malkia kwa kutawazwa.
Barua ya mwaka 1952 toka kwa Rashid Mfaume Kawawa kutoka Bukoba kwenda kwa Ally Sykes ikimfahamisha juu ya hali ya siasa katika Kanda ya Ziwa.
Nyaraka kutoka kwa Lady Judith Listowel, Kenneth Kaunda, Julius Nyerere, Kasela Bantu, Chifu Thomas Marealle ...orodha haina mwisho...''
Kutoka (''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes...'')
Nyingi katika hizi ni barua ambazo Ally Sykes alikuwa akipokea kutoka kwa wazalendo hawa waliokuwa wanapambana na wakoloni.