SoC02 Uchumi: Siri ya mafanikio ya kudumu

SoC02 Uchumi: Siri ya mafanikio ya kudumu

Stories of Change - 2022 Competition

DnS8elpmis

New Member
Joined
Jul 26, 2022
Posts
3
Reaction score
1
Siri ya Mafanikio ya Kudumu


Maisha ni vita. Hasa wakati uchumi ndio hoja kuu. Hivyo ni muhimu kuwa na nyenzo za ushindi. Nyenzo kuu itakayo kupa nafasi ya kupata ushindi, tena wa kudumu, ni kujitambua. Mapambano ya maisha ni endelevu na yenye kubadilika mara kwa mara. Kwa wale wanao jitambua ni rahisi kutabiri yajayo na kubadilika kwa wakati ili kukwepa majanga ya kiuchumi. Kuishi bila kufanya bidii ya kujitambua ni sawa na dereva kuachilia usikani na kukitegemea chombo kifuate njia bila muongozo.


Faida za kujitambua

Kwa vile sisi binadamu tunaishi, tunakua na kubadilika. Kwa maana hiyo mchakato wa kujitambua pia ni swala endelevu. Faida zake pia ni endelevu na jinsi utakavyo weka bidii ndivyo matokeo yatafuata.


1. Maamuzi bora
Mambo unayo kutana nayo katika maisha yako leo, ni mkusanyiko wa matokeo ya maamuzi ya nyuma. Yaani unavuna ulichokipanda. Haiwezekani kuishi bila kukosea. Ila, inawezekana kabisa, kuongeza idadi ya maamuzi yaliyo bora na yenye tija. Baada ya muda utaanza kuona kama vile mambo yana kwenda unavyotaka na ushindi kwako kua hali ya kawaida. Haya ni malipo ya malimbikizo ya maamuzi sahihi.


2. Malengo sahihi
Ishirini na nne. Hii ndio idadi ya masaa tunayopata wote kila siku. Pamoja na ilo kuna watu wanaonekana kufanya mambo mengi sana na masaa yao 24 kuzidi wengine. Kwa anaye jitambua ni rahisi kujua ni wapi ipo njia bora zaidi kwake, ya kuijenga hali yake kiuchumi. Malengo bila kujitambua ni kama kucheza bahatinasibu na maisha ilhali mbadala upo. Malengo yako yanapo chimbukia katika kujifahamu, yatakua sambamba na uhalisia wako. Hili litakuruhusu kutimiza majukumu na kazi zako kwa kasi na ufanisi zaidi, hivyo kufanya mengi na yaliyo bora!


3. Uthubutu, Kujiamini na Heshima
Unapo jitambua unakijua kina chako, unatambua uwezo na madhaifu yako. Unaelewa mahitaji yako, na maamuzi yako yanaendana na malengo yako. Katika hali hii inakua rahisi kujua muda wa kusikiliza au kutafuta ushauri. Wakati huo huo uwezo wa kutambua muda wa kumwaga bidii na roho yako katika swala lenye tija kwako. Hata kama wengine hawaoni ivyo.

Jinsi ya kujitambua


Kwa vile kujitambua ni mchakato endelevu basi pia kuna namna na pia viwango tofauti vya kujitambua.

1. Utambuzi wa msingi
Hapa ni vitu kama:

  • Jina na jinsia.
  • Ukabila yaani kwa mfano, mhindi, mzungu au msukuma, mjaluo hizi ni sifa za kikabila.
  • Sifa za kimaumbile kama urefu, ufupi, unene.
  • Hali ya afya; ulemavu magonjwa ya kurithi.
  • Vipaji, talanta na uwezo wa zaidi ya kawaida katika fani mbali mbali .

Kwa asilimia kubwa sifa hizi zinaweza kuboreshwa, kama ilivyo vipaji na talanta. Ama kutafutiwa mbinu za kurahisisha maisha kama ilivyo kwa ulemavu na magonjwa . Jinoe katika kipaji chako, soma zaidi katika fani yako, kama una ulemavu angalia kuna namna gani ya kurahisisha maisha. Kila changamoto ina fursa ndani yake, na ikichezewa basi fursa hugeuka sumu. Mfano mzuri wa hili pale ambapo aliyezaliwa kwenye mali anashindwa kujijenga kiuchumi kwa sababu wa wepesi wa maisha. Halafu aliyezaliwa katika ufukara anapata nguvu kutokana na maisha magumu na kupambana hadi kupitiliza malengo na matarajio. Hivyo basi jitambue ili ujilinde na ujikwamue.


2. Utambuzi wa mazingira
Katika sehemu hii,

a) Uwepo wa kijiografia, uko wapi duniani? Bara lipi, nchi gani, mjini au jijini?

b) Pia ni muhimu kutambua kipindi ambacho unaishi, kwa mfano hii enzi ya teknolojia na mawasiliano kidunia . Ila ukitazama kwa mabara Africa hivi sasa inaingia katika enzi ya viwanda na uchakataji. Na wakati huo huo; Tanzania ipo katika mapinduzi ya kilimo biashara, muamko mkubwa wa viwanda na uchakataji, mwisho linafuata wimbi la teknolojia na mawasiliano linalozidi kushika kasi kila siku. Pamoja na hayo, hali ya kiuchumi ya dunia kwa sasa imezorota kwa sababu ya janga la UVIKO-19.

c) Mwisho na kwa hakika muhimu sana katika mazingira, ni watu. Kwa kutambua uhalisia wa watu walio tuzunguka tunapata fursa ya kujihusisha na wale walio na tija katika mapambano au basi kukwepa waleta majanga . Kwa dhana hii hii, ni rahisi kuchambua watakao faa katika vita za maisha.

Muda mwingine mazingira yanaweza kuwa kikwazo ama yakawa ni baraka isiyo na mfano. Bila kufikiria mazingira basi mafanikio ni ya bahati na yana uwezekano mkubwa wa kupotea kwa urahisi zaidi. Mfanyabiashara je mazingira yako yanakupa nini ambacho hujakitumia, au yanakunyima nini? Mwanafunzi mazingira yako ni rafiki kwa malengo yako. Jitambue, jilinde, jikwamue, usitembee Kariakoo siku nzima na ndoto ya kuokota dhahabu, mwisho wake ni njaa na yakikukuta utaishia hata kupigwa.


3. Utambuzi wa hali
Ili kuitambua hali yako ni lazima kutambua

a) Wadhifa wako, je wewe ni kiongozi au ni mfuasi? Umeajiri au umeajiriwa? Kila nafasi ina majukumu yake.

b) Ni mwana ndoa, unajitegemea au kutegemewa? Basi jiulize upo sehemu sahihi , iwapo jibu ni ndio, je kuna maboresho au la kuimarisha. Kama unahisi sehemu sio sahihi basi shida ni nini?

c) Na vipi kuhusu kazi unayofanya, malipo yake, hatima yake? Unakidhi mahitaji, unapata akiba?

d) Matarajio yako ukilinganisha na uhalisia wako?

e) Je kihisia uko sawa. Wengi tunapuuza umuhimu wa hali ya kihisia, ila hili ni jambo linaloweza kukutoa katika reli za uhakika wa mafanikio na kukubwaga kwenye korongo la shida zisizoisha. Hakuna mtu ambaye hajawahi kujikuta amekumbwa na hisia kali na kutamani kuzichukulia hatua. Na lazima unaweza kumbuka mtu walau mmoja unaemfahamu, aliyejifunga utumwa wa kihisia. Labda ni hisia za kimapenzi, hasira, chuki. Jaribu ujiangalie na jicho kavu kama vile unavyoweza angalia uhalisia wa mtu mwingine.

f) Mahusiano yako. Katika maisha tunakuwa na mahusiano mengi. Kuanzia yale binafsi, ya kifamilia, kikazi na ya duniani kiujumla mahusiano yetu yana nafasi kubwa sana katika mafanikio yetu. Kwa mfano, ni ngumu kufika mbali ikiwa malengo yako na mwenza wako hayaendani. Ila wakati huo huo inatia nguvu iwapo ndugu na jamaa wanaunga mkono bidii zako kwa moyo mmoja.


Hitimisho

Zoezi la kujitambua si zoezi rahisi, kwani inakulazimu ujiangalie bila aibu, ujichambue ndani na nje, na uwe tayari kukutana na ukweli mchungu na kuumeza. Hakika ni ngumu, ila bila shaka wepesi wa kutatua tatizo unaongezeka jinsi tatizo linavyo tambulika kwa kina zaidi. Ila sio hicho tu, pia hata kuweza kuitumia fursa ipasavyo ni muhimu kuielewa fursa mwanzo hadi mwisho. Hii ndio misingi ya ushindi.

Ukweli ni kwamba mara nyingi tunafanya maamuzi mengi kwa misukumo ya nje au mihemko ya ghafla. Maamuzi haya chimbuko lake ni kuishi kama mpofu ilhali upeo upo. Muda mwingine matokeo huwa ni ya papo kwa hapo wakati mwingine matokeo yanakuja wakati hata chanzo kilishasahaulika. Sasa katika vita kali kwanini ujinyime asilimia hata moja ya ushindi?

Hoja zilizojadiliwa hapa ni mwanzo tu. Kwa kuorodhesha yaliyoainishwa utapata mwangaza wa kukupa mwelekeo katika safari ya kujitambua. Ni mkusanyiko wa haya mambo unao kutambulisha wewe katika uhalisia wako.Jitambue uwe na jicho pevu kwa wengine ila hasa kwako wewe mwenyewe. Tabia yako ndio ufunguo wa utajiri wako; jitambue, urekebishe madhaifu, uimarishe vipawa vyako, ili ufikie kilele cha ubora wako.

Naamini unaweza!
 
Upvote 0
Back
Top Bottom