Kwa kulinganishwa na asilimia 4.5 ambacho ni wastani wa kiwango cha ukuaji wa uchumi wa China katika miaka mitatu iliyopita, kiwango hicho ni cha kasi, hali ambayo inaonesha kuwa uchumi wa China unafufuka kwa utulivu.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita wakati China ilipokuwa ikikabiliana na janga la COVID-19, ilichukua hatua kali mbalimbali za kuzuia virusi, ili kulinda afya na usalama wa maisha ya watu.
Hatua hizo zilifanikisha China kukabiliana na janga hilo, lakini wakati huo huo zilileta athari mbaya kwa uchumi. Tangu kumalizika kwa hatua hizo mwishoni mwa mwaka jana, uchumi wa China umeonyesha maendeleo ya kufufuka, hasa katika sekta ya huduma.
Ikilinganishwa na nchi nyingine, ukuaji wa uchumi wa China katika nusu ya kwanza ya mwaka huu ulikuwa wa kasi zaidi kuliko wa nchi kubwa kiuchumi. Katika robo ya kwanza ya mwaka huu, pato la taifa la Marekani, Umoja wa Ulaya na Japan lilikua kwa asilimia 1.8, 1 na 1.9.
Nchi zilizoendelea zinahangaika kukabiliana na changamoto za mseto za mfumuko wa bei na kudidimia kwa uchumi. Utulivu wa maendeleo ya uchumi wa China umeendelea kuwa injini muhimu ya uchumi wa dunia.
Biashara kati ya China na nchi za nje pia imeendelea kustawi katika nusu ya kwanza ya mwaka huu. Takwimu zilizotolewa na Idara Kuu ya Forodha ya China zinaonesha kuwa, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, thamani ya jumla ya biashara ya bidhaa kati ya China na nchi za nje ilikuwa yuan trilioni 20.1 sawa na dola trilioni 2.8 za Kimarekani, ambalo ni ongezeko la asilimia 2.1 ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hicho.
Mauzo ya magari ya nishati mpya, betri za lithiamu-ioni, na paneli za umeme wa jua za China kwa nchi za nje yameongezeka kwa haraka sana. Wakati huo huo, nchi za ASEAN na nchi husika za Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” zimekuwa sehemu mpya zenye ukuaji wa haraka wa biashara na China.
Hata hivyo, hivi sasa maendeleo ya uchumi wa China yanakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo kupungua kwa mahitaji ya kimataifa, na tishio la vikwazo vya kibiashara vya Marekani na nchi nyingine za Magharibi.
Kuhusu ajira, kwa kuwa uchumi wa China uko katika mchakato wa kubadilika kutoka kutegemea zaidi nguvu kazi hadi kutegemea zaidi teknolojia na elimu ya juu, kiwango cha ukosefu wa ajira kimepanda kwa kiasi fulani. Lakini kwa upande mwingine, hatimaye uboreshaji wa muundo wa uchumi husaidia kutatua suala la ajira.
Kwa ujumla, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, uchumi wa China umeendelea kwa utulivu na kasi inayofaa, ambayo imeweka msingi mzuri wa maendeleo ya baadaye, na pia kuleta imani kwa maendeleo ya uchumi wa dunia.