imem2022
New Member
- Aug 17, 2022
- 2
- 1
- Utangulizi`
Mazingira ni jumla ya ardhi, maji, hewa na kila kilichopo ndani yake, mwanadamu akiwa sehemu ya mazingira anawajibu mkubwa katika usimamizi wake. Aidha, mwanadamu ana mchango mkubwa sana katika uzalishaji wa taka ikiwemo taka ngumu na aina mbalimbali za taka katika mazingira.
Taka ngumu ni aina ya taka ambazo huzalishwa maeneo tofauti tofauti kutokana na mabaki ya vitu, baada ya kuzalisha vitu au yasio kuwa na matumizi katika hali mango.
Kaya ni nyumba na wakazi wake kuchukuliwa kama kitengo.
Taka ngumu ni aina ya taka ambazo huzalishwa maeneo tofauti tofauti kutokana na mabaki ya vitu, baada ya kuzalisha vitu au yasio kuwa na matumizi katika hali mango.
Kaya ni nyumba na wakazi wake kuchukuliwa kama kitengo.
- Hali ya sasa
Hali halisi ya sasa katika udhibiti wa taka ngumu katika ngazi ya kaya, maeneo ya biashara na uzalishaji si rafiki kwa mazingira katika kushughulikia maendeleo endelevu ya jamii zetu kwa ujumla. Ni hali ya mazoea kwa jamii zetu kuwa na chombo kimoja cha kukusanyia taka na kupelekea ugumu katika kutenganisha taka hizo; na hata hivo si wote wanavyombo vya kukusanyia taka na kupelekea kuzagaa kwa taka kutokana na tabia ya kutupa taka nyakati za usiku hasa maeneo ya miundombinu kama barabarani na madaraja. Ni dhahiri udhibiti wa taka katika kaya na maeneo mbalimbali ya biashara haujasimamiwa ipasavyo hivo kupelekea kuzagaa kwa taka ngumu katika mitaa na maeneo mbalimbali katika mazingira. Hii huathiri sana mazingira hasa ardhi na maeneo ya vyanzo vya maji na kupelekea hitaji la jitihada za makusudi kufanyika ili kuokoa hali hii.
- Maono
- utunzaji wa mazingira ya ardhi.
- kupunguza kasi ya magonjwa ya mlipuko yatokanayo na taka ngumu katika ngazi ya kaya na jamii kiujumla.
- kutengeneza nyanja za kipato katika kaya kupitia udhibiti wa taka ngumu.
- kuchochea kasi ya kuchakata tena, kutumia tena na kupunguza taka ngumu katika mazingira.
- Kupunguza gharama ya matumizi ya fedha ya serikali katika udhibiti wa taka ngumu .
- Mikakati
Mgawanyo wa taka ngumu katika ngazi ya kaya, maeneo ya biashara na uzalishaji.
Moja ya jitihada zinazotazamiwa kuzingatiwa ni kuhamasisha matumizi ya vyombo viwili ili kuwezesha utenganyishwaji wa taka kati ya taka za vyakula na taka rejea. Ambapo taka rejea zinaweza kuwa chanzo cha kujipatia kipato kwa kuzikusanya na kuziuza kwa mawakala wa viwanda vinavyo tegemea taka hizo kama malighafi na vilevile, taka za vyakula zinaweza kutumika kwa matumizi ya mbolea bustanini na mashambani.
- Utoaji wa elimu juu ya namna ya mgawanyo wa taka ngumu unaoweza kufanyika.
Kuielimisha jamii juu ya zoezi la utenganishwaji wa taka ni jambo muhimu kwani kwa sasa jamii haina uelewa juu ya umuhimu wa utenganishwaji wa taka na manufaa wanayoweza kuyapata kutokana na taka hizo, hii itakuwa ni chachu katika kufikia lengo la kuwezesha utenganishwaji wa taka na usimamizi wa mazingira kwa ujumla.
- Kuboresha mahusiano kati ya wananchi, serikali za mitaa na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa mazingira.
Mahusiano kati ya pande hizi tatu ni muhimu kwani wananchi wapo karibu na serikali za mitaa ambazo husaidiana na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa mazingira zinahusika na uondoaji wa taka kwa makundi. Uwepo wa utenganishwaji wa taka katika dampo ambazo zinasimamiwa na mamlaka zinazohusika na uondoaji wa taka ni jambo muhimu ili kuendeleza desturi ambayo imejengwa kuanzia hatua ya awali (majumbani, maeneo ya biashara na uzalishaji), jitihada hizi zitapelekea mafanikio makubwa katika usimamizi wa mazingira kupitia udhibiti wa taka.
- Utoaji wa motisha ili kuhamasisha zoezi la udhibiti na usimamizi wa taka ngumu.
Zoezi hili ni muhimu kwa kaya, maeneo ya biashara na uzalishaji yatakayofanya vizuri katika udhibiti wa taka ngumu kwa kupewa zawadi mbalimbali, lengo ni kutoa motisha na kuhamasisha jamii nzima katika usimamizi wa mazingira kwa udhibiti wa taka ngumu katika hatua ya awali.
- Utungaji na usimamizi wa kanuni na sheria ndogo zinazowahusu wazalishaji na wafanyabiashara ambao wanachangia katika uzalishaji wa taka ngumu.
Nguvu ya ziada inahitajika katika usimamizi wa kanuni na sheria ndogo na utungaji wa kanuni na sheria nyingine zinazohusu uidhinishaji wa biashara, viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kuwezesha na kusimamia shughuli hizo za uzalishaji ili kuwezasha kurejea taka baada ya kuzitenganisha katika hatua ya awali na katika dampo lakini pia kanuni na sheria kwa kila kaya kuwa na vyombo vya kuwekea taka.
- Hitimisho
Sera ya taifa ya mazingira inasisitiza maendeleo endelevu ambapo jamii zetu za kitanzania lazima zitategemea mazingira kujiendeleza pia kuna mahusiano makubwa kati ya umaskini, maendeleo na mazingira. Mazingira yakiharibiwa yataleta ugumu kwa binadamu kujitafutia riziki, lakini pia katika shughuli za kujitafutia riziki watu wanaweza kuharibu mazingira. Kuyatunza mazingira na wakati huo huo kutafuta kipato kwa kupitia mazingira ndio changamoto kwa jamii, kwa tafsiri hiyo elimu kwa jamii inahitajika. Udhibiti wa taka ngumu katika ngazi ndogo na ya chini ya kaya itakuwa na manufaa sana kwa jamii nzima kwani katika kaya ndiko jamii inakotengenezwa. Uhusiano wa jamii, serikali za mitaa na mamlaka za mazingira ni muhimu sana katika suala nzima za udhibiti wa taka ngumu kuwepo na mawasiliano ili kufanya mazingira kuwa safi. Maendeleo endelevu yanalenga katika kuwezesha jamii kuweza kujipatia mahitaji yake kutoka katika mazingira kwa wakati uliopo na kwa kizazi kilichopo lakini pia na kwa kizazi kijacho kuwa na uwezo wa kupata mahitaji yao bila changamoto kutoka kwenye mazingira.
Upvote
0