UDOM na IUCEA zaimarisha ushirikiano katika mpango wa kimkakati wa ufadhili wa masomo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

UDOM na IUCEA zaimarisha ushirikiano katika mpango wa kimkakati wa ufadhili wa masomo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

University of Dodoma (UDOM)

Public Institution
Joined
Feb 24, 2024
Posts
50
Reaction score
55
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), leo tarehe 17 Juni 2026, kimepokea ujumbe kutoka Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA) uliolenga kujadili ushirikiano katika utekelezaji wa Mpango wa Ufadhili wa Masomo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Scholarship Programme).

Ujumbe huo uliongozwa na Prof. Meshack Obonyo wa Kenya, Mkuu Mwandamizi wa Idara ya Ubadilishanaji na Ushirikiano wa IUCEA, pamoja na Dkt. Gervais Ndayizeye kutoka Uganda, Afisa Mwandamizi wa Programu za Ubadilishanaji wa Wanafunzi na Wataalamu wa IUCEA. Viongozi hao walitembelea Ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, kwa ajili ya mazungumzo kuhusu namna ya kuimarisha ushiriki wa UDOM katika mpango huo wa kikanda.

Katika kikao hicho, pande zote mbili zilijadili fursa zinazotolewa na EAC Scholarship Programme, hususan katika kuwawezesha wanafunzi wenye ufaulu wa juu wa kitaaluma wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo wa kifedha kupata elimu ya juu na uzamili. Aidha, programu hiyo inalenga kukuza ushirikiano wa kikanda, kuimarisha maendeleo ya ujuzi na kujenga uwezo wa kitaaluma unaohitajika katika maendeleo ya Afrika Mashariki.

Akizungumza wakati wa mazungumzo hayo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, alisema ushirikiano huo unaendana kikamilifu na dira ya UDOM ya kuendeleza ubora katika elimu, utafiti na ushirikiano wa kimataifa.

“UDOM itaendelea kuwa mshirika muhimu katika juhudi za kuimarisha elimu ya juu, utafiti na maendeleo ya rasilimali watu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ushirikiano huu unafungua fursa zaidi kwa vijana wetu kunufaika na elimu yenye ushindani wa kimataifa,” alisema Prof. Kusiluka.

Kwa upande wake, Dkt. Gervais Ndayizeye alieleza kuwa EAC Scholarship Programme imebuniwa kuwezesha wanafunzi wenye uwezo mkubwa wa kitaaluma kufikia ndoto zao za elimu bila kuzuiwa na changamoto za kiuchumi. Aliongeza kuwa mpango huo pia unalenga kuimarisha mshikamano wa kikanda na kuchochea maendeleo endelevu katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Naye Prof. Meshack Obonyo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za elimu ya juu katika kukuza ubadilishanaji wa maarifa, tafiti na uzoefu wa kitaaluma unaochangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika ukanda huo.

Ziara hiyo inaashiria hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya UDOM na IUCEA, huku ikiweka msingi imara wa kupanua fursa za elimu, utafiti, ubadilishanaji wa wanafunzi na wataalamu, pamoja na maendeleo ya rasilimali watu kupitia Mpango wa Ufadhili wa Masomo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
 
Back
Top Bottom