University of Dodoma (UDOM)
Public Institution
- Feb 24, 2024
- 50
- 55
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kukuza ubora wa elimu kwa kuandaa mashindano ya umahiri wa lugha ya Kichina, “Chinese Proficiency for Foreign College Students 2026” yaliyofanyika Jumanne tarehe 5 Mei 2026, katika ukumbi Mikutano wa Ndaki ya Sayansi za Jamii(CHSS).
Mashindano hayo yalilenga kuimarisha ujuzi wa lugha za kigeni miongoni mwa wanafunzi wa lugha ya kichina na kuwafungulia milango ya fursa za kimataifa katika elimu, ajira na ushirikiano wa kimataifa.
Katika mashindano hayo, vyuo viwili pekee nchini vilishiriki, UDOM na Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM), vikiwa na jumla ya washiriki kumi. Washindani walipimwa katika uwezo wa kuzungumza lugha ya Kichina, uelewa wa utamaduni wa kichina pamoja na ubunifu wa kisanaa.
Akifungua mashindano hayo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Razack Lokina amesisitiza umuhimu wa jukwaa hilo kwa maendeleo ya wanafunzi, akieleza kuwa linawajengea uwezo wa kitaaluma, kujiamini na kuwapanulia upeo wa fursa za kimataifa.
“Hili si jukwaa la ushindani pekee, bali ni daraja linalounganisha tamaduni na kufungua milango ya fursa kwa vijana wetu katika ulimwengu wa sasa,” alisema Prof. Lokina.
Katika matokeo, mshindi wa kwanza, Bwana Meshack Zuberi kutoka UDOM, anatarajiwa kuungana na washindi wengine wawili kuwakilisha katika ngazi ya kitaifa itakayofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Washindi hao watapata fursa ya kushindana na wenzao kutoka vyuo mbalimbali nchini kabla ya kuwania ushindi katika ngazi ya kimataifa nchini China.
Mashindano hayo yameendelea kuthibitisha nafasi ya lugha ya Kichina kama nyenzo muhimu ya mawasiliano ya kimataifa na kichocheo cha fursa za elimu na ajira kwa vijana wa Tanzania.