UDOM yaonyesha matokeo ya utafiti wa blockchain kuimarisha minyororo ya ugavi wa kilimo

UDOM yaonyesha matokeo ya utafiti wa blockchain kuimarisha minyororo ya ugavi wa kilimo

University of Dodoma (UDOM)

Public Institution
Joined
Feb 24, 2024
Posts
50
Reaction score
55
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, kimefanya warsha ya kuwasilisha na kujadili matokeo ya mradi wa utafiti kuhusu matumizi ya teknolojia ya Blockchain katika kukuza ubunifu jumuishi na kuimarisha ufanisi wa minyororo ya ugavi wa kilimo nchini.

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) 3.jpg
Warsha hiyo imefanyika leo katika Ukumbi wa East Africa uliopo Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu, ikiwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, viongozi wa vyama vya ushirika, watunza ghala pamoja na wawakilishi wa taasisi washirika, zikiwemo Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), TCDC na COPRA.

Akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Jefta Sunzu, amesema teknolojia ya Blockchain ina uwezo mkubwa wa kuboresha sekta ya kilimo kwa kumwezesha mkulima kupata taarifa sahihi na kwa wakati, kuongeza uwazi katika mnyororo wa ugavi na kupanua fursa za masoko.

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).jpg

Prof. Sunzu amesema mafanikio ya matumizi ya teknolojia hiyo yanategemea kuendelea kuimarishwa kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ili kuhakikisha wakulima wanapata manufaa ya moja kwa moja kutokana na mifumo ya kidijitali.

Kwa upande wake, Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu, Dkt. Hector Mongi, amesema utafiti huo umeibua mafunzo muhimu 10 yanayoonesha changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo. Miongoni mwa changamoto hizo ni mabadiliko ya mara kwa mara ya bei za mazao, kiwango kidogo cha ujuzi wa matumizi ya teknolojia za kidijitali kwa baadhi ya wakulima, umiliki mdogo wa simu janja na ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Mtafiti Mkuu, Dkt. Hilda Mwangakala, amesema pamoja na sekta ya kilimo kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania, bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa uwazi katika taarifa za masoko, mifumo isiyounganishwa ya utunzaji wa taarifa pamoja na ushiriki mdogo wa wakulima katika mifumo rasmi ya kifedha.

Amesema changamoto hizo ndizo zilizochochea kuanzishwa kwa mradi huo unaolenga kutumia teknolojia ya Blockchain kuongeza uwazi, ufanisi, uaminifu na ushirikishwaji katika minyororo ya ugavi wa mazao ya kilimo.

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) 2.jpg

Dkt. Mwangakala ameongeza kuwa mafanikio ya matumizi ya Blockchain na teknolojia nyingine za kidijitali katika sekta ya kilimo yatategemea uwepo wa sera rafiki, taasisi imara, miundombinu bora ya kidijitali, uwezo wa watumiaji pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya wadau wote.

Naye Mkurugenzi wa TEHAMA wa UDOM, Dkt. Deo Shayo, amesema mfumo wa Blockchain utawasaidia wakulima kuhifadhi taarifa za uzalishaji wa mazao yao kwa usalama, kufanya tathmini ya maendeleo ya shughuli zao za kilimo na kuongeza uwazi katika usimamizi wa taarifa.

Ameeleza kuwa mfumo huo una kiwango cha juu cha uaminifu kutokana na uwezo wake wa kulinda taarifa na kuhakikisha uwazi katika upatikanaji wake, jambo linaloufanya kuwa na manufaa makubwa ikilinganishwa na mifumo mingine ya kidijitali.
 
Back
Top Bottom