Ufafanuzi wa mdau kuhusu usambazaji wa pembejeo za korosho msimu 2026/2027

Ufafanuzi wa mdau kuhusu usambazaji wa pembejeo za korosho msimu 2026/2027

Kayugumis

Senior Member
Joined
Jun 6, 2022
Posts
160
Reaction score
172
Nikiwa kama mdau wa sekta ya Korosho hapa nchini, ambaye nimezaliwa na kulelewa kwa zao hili la Korosho, kwa maoni yangu tunapaswa kuheshimu hatua kubwa inayopigwa katika kusimamiwa na kuendelezwa kwa zao hili, ambalo limekuwa likitumika na baadhi ya watu vibaya kwa maslahi yao binafsi ili kuvuruga mipango na mikakati iliyopo bila kuangalia kwa upande mwingine ambao kumekuwa na jitihada kubwa katika kuboresha maslahi ya wakulima.

Nitakuwa mchoyo wa Fadhila nisipoandika maoni haya kwa kueleza kwa uchache ambayo nayafahamu yaliyosaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa baadhi ya kero ambazo zilikuwa zinawakabili wakulima wetu, kwa kipindi cha zaidi ya miaka minne, tumeshuhudia kwa kiasi kikubwa kuondoka kwa kilio cha wakulima wa zao la korosho ambao walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, vifungashio kwa wakati na hata malipo yao kwa kwa wakati.

Mchango huu kwa kiasi kikubwa umechangiwa na kuanzishwa kwa Taasisi ya Korosho Cooperative Joint Enterprise Limited (KCJE), ambayo ni Taasisi iliyosajiliwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania chini ya kifungu cha 33 cha Sheria ya Vyama vya Ushirika Sura ya 211 Pamoja na marekebisho yake ya Mwaka 2025 na Kanuni zake za mwaka 2015 na kupata namba ya usajili AFF-MTR-MTR-MC-2023-104.

Pamoja na mambo mengine Taasisi hii imekuwa ikifanya shughuli kubwa ya kuratibu na kusimamia ununuzi na usambaji wa pembejeo, kuratibu na kusimamia usambazaji mfumo wa Mizani za kidijitali kwenye Vyama vikuu vya Ushirika, na kuratibu na kusimamia ununuzi wa magunia kwenye vyama hivyo pia, na taasisi hii tangu ianzishwe ina takribani miaka minne tu, lakini tumeona mabadiliko makubwa ambayo pia yamechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo kutoka tani 240,000 hadi tani 618,000.

Nikiiyaelekeza maoni yangu kwa upande wa suala la usambazaji pembejeo, kutokana na taarifa za uhakika nilizonazo ni kuwa tayari zaidi ya tani 15,000 za Salfa ya Unga zimeshasambazwa kwa wakulima wa Korosho nchini, huku usambazaji huo ukiwa unaendelea.

Salfa hiyo ya unga ilisambazwa kutokana na kuwa na tani 16,000 zilizokuwa zimebaki msimu 2025/2026, baadae KCJE iliagiza tani 10,000 na kumaliza kiasi kingine cha tani 5,000, huku viuatilifu vya maji lita milioni 2 vikipokelewa pamoja na salfa hizo mwaka huu.

Kuhusu Viuatilifu vya maji, ni kuwa tayari zaidi ya lita milioni 3.2 zimesambazwa kwa wakulima msimu 2026/2027, ambayo ni mara mbili zaidi ya kiasi cha lita milioni 1.5 zilizokuwa zimekusudiwa kusambazwa awali.

KCJE ililazimika kuongeza kiasi hicho cha viuatilifu vya Maji, baada ya kuona kutakuwa na ucheleweshaji wa salfa ya Unga kutokana na mzozo uliokuwa unaendelea katika nchi za mashariki ya kati ambako ndipo salfa ya unga inapotokea, ambao ulisababisha bei kuongezeka maradufu.

Kwa hiyo inawezekana kabisa kukawa na changamoto za hapa na pale katika mchakato mzima wa uagizaji na usambazaji wa pembejeo msimu 2026/2027 lakini KCJE imejitahidi sana katika kuhakikisha kuwa wakulima wanafikiwa na pembejeo hususan za maji ambazo kulikuwa na bakaa ya wastani wa lita milioni 7, katika msimu uliopita, na kusaidia kuwafikia wakulima kwa wakati hali ambayo imepunguza usumbufu kwa kiasi kikubwa, na ikumbukwe kuwa nchi yetu haina kiwanda cha kuzalisha pembejeo zinazotumika na zao hili, hivyo jitihada za watendaji ndio zilizotumika ili kukabiliana na changamoto hizo, kwani wengi wetu tunafahamu yanayoendelea huko mashariki ya kati.

Ni vema pia kujua kuwa tangu KCJE ianze kuagiza pembejeo, kumekuwa na mtiririko mzuri wa ongezeko la viuatilifu vinavyowafikia wakulima wa korosho nchini tena kwa wakati, hivyo kuongeza uzalishaji.

Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha misimu mitano kuanzia 2021/2022 hadi 2025/2026, jumla ya lita 11,002,730 za viuatilifu vya maji zimesambazwa, huku sulphur ya unga ikifikia tani 153,291.

Katika msimu wa 2021/2022, zilisambazwa lita 1,497,354 za viuatilifu vya maji na tani 13,562 za sulphur ya unga. Kiasi hicho kiliongezeka katika msimu wa 2022/2023 hadi lita 2,683,682 za viuatilifu na tani 15,014 za sulphur.
Msimu wa 2023/2024 ulirekodi usambazaji wa lita 1,989,238 za viuatilifu vya maji na tani 39,275 za sulphur, kabla ya kuongezeka zaidi mwaka 2024/2025 ambapo lita 2,689,581 za viuatilifu na tani 41,263 za sulphur zilisambazwa.

Katika msimu wa 2025/2026, jumla ya lita 2,142,875 za viuatilifu vya maji zilisambazwa, huku sulphur ya unga ikifikia kiwango cha juu cha tani 44,177.

Ongezeko hilo la usambazaji wa sulphur linaonesha kuendelea kwa jitihada za kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo muhimu kwa wakati, jambo linalolenga kudhibiti visumbufu na magonjwa ya mikorosho na hatimaye kuongeza uzalishaji wa korosho ghafi.

Nimalizie kwa kuomba wadau wote wanaouhisika kwenye mnyororo wa Sekta ya Korosho nchini, kuunga mkono juhudi zinazofanywa na KCJE katika kukuza na kuendeleza zao la Korosho na pale kunapotokea changamoto basi kuomba ufafanuzi kutoka kwa vyanzo sahihi ili kupata taarifa sahihi kutoka kwenye vyanzo vya kuaminika.

Na kama kuna mtu yoyote mwenye jambo na ushauri wowote kwa ajili ya kuboresha zaidi, ni vyema ajitokeze hadharani au kuwasiliana na watendaji wa taasisi hiyo ili kushauri naamini KCJE itakuwa tayari kupokea na kufanyia kazi ushauri wowote badala ya kujificha.
 
Back
Top Bottom