SoC03 Ufanisi mbovu wa sheria

SoC03 Ufanisi mbovu wa sheria

Stories of Change - 2023 Competition

SanPedro

Member
Joined
Apr 4, 2019
Posts
41
Reaction score
89
Sheria ni mfumo wa kanuni na taratibu zilizowekwa kwenye jamii na mamlaka kwa ajili ya kuongoza matendo na kuratibu mahusiano baina yaoili kukuza, kuendeleza na kudumisha amani, utulivu na utengamano.

Ufanisi wa sheria ni uwezo wa sheria zilizowekwa kwenye jamii na mamlaka kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuleta matokeo chanya katika utekelezaji wake bila kuathiri mfumo wa utendaji kazi.

Hapa nchini, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ndio chanzo kikuu cha sheria. Kwa kawaida sheria hutungwa na bunge au mamlaka nyingine za kutunga sheria, ambapo sheria zilizotungwa na bunge huitwa sheria kuu. Sheria zilizotungwa na mtu, chombo au mamlaka yoyote iliyoruhusiwa kutunga sheria hiyo kwa mujibu wa sheria kuu iliyopitishwa na bunge, huitwa sheria ndogo. Mfano wa sheria ndogo ni sheria zilizotungwa na halmashauri za jiji, manispaa, miji, mkoa, wilaya au waziri.

Kadharika, chanzo kingine cha sheria nchini Tanzania ni maamuzi ya mahakama ya rufaa na mahakama kuu. Maamuzi ya mahakama hizi hufuatwa na mahakama za ngazi ya chini katika kuamua kesi za namna hiyo.

Kwa mujibu wa ibara ya 97(1), ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, bunge litatumia madaraka yake ya kutunga sheria kwa kufuata utaratibu wa kujadili na kupitisha miswada ya sheriaambayo hatimaye itabidi ipate kibali cha Rais, na muswadahautakuwa sheria mpaka uwe umepitishwa na bunge nakukubaliwa na Rais.

Zifuatazo ni baadhi ya sheria zilizotungwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuonesha ufanisi mbovu wakati wa utekelezaji wake, kwani zilileta matokeo hasi na yasiyo na tija, tofauti na ilivyokusudiwa.

Sheria ya mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma nambari 2 ya mwaka 2018. Sheria hii ilipitishwa na bunge mnamo Januari 31, 2018 na kusainiwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tano, Daktari John Pombe Magufuli Februari 8, 2018. Mara tu baada ya kuanza utekelezaji wake, sheria hii ilizua mvutano mkubwa kati ya wafanyakazi, wawakilishi wa wafanyakazi, waajiri na serikali. Hii ni kutokana kuwa kanuni ya sheria hii ilikuwa na vikokotoo ambavyo vinabinya uwiano na usawa wa mafao baina ya wastaafu.

Mvutano kati ya wawakilishi wa wafanyakazi, waajiri na serikali ulipelekea sheria hii kuonekana haina tija katika jamii na inakiuka haki za wafanyakazi. Hali iliyompelekea aliyekuwa Rais wakati huo, hayati Daktari John Pombe Magufuli kukaa meza moja na wadau wa sheria hii ili kufikia muafaka wa muelekeo wa utoaji wa mafao kwa wanufaika.

Hali kadharika, katika serikali ya awamu ya sita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassani, mnamo tarehe 14 May, 2022 alitoa maelekezo mapya kuhusu kanuni ya mafao kwa wastaafu.

Sheria ya huduma za habari nambari 12 ya mwaka 2016. Sheria hii ilitungwa na bunge na kupitishwa na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, hayati Daktari John Pombe Magufuli mnamo tarehe 16 Novemba, 2016. Utekelezaji wa sheria hii ulitengeneza mazingira magumu kwa wadau wa vyombo vya habari kutokana na kanuni kama vile; magazeti kutakiwa kupata leseni badala ya kibali cha moja kwa moja. Kama sheria zingine, sheria hii haikonesha ufanisi mzuri kwani taifa lilishuhudia ufutwaji holela wa leseni za magazeti. Kadharika, sheria hii inaingilia uhuru wa wanahabari hususani wahariri, kwani kwa mujibu wa kifungu cha 7 (2) (b) (iv), cha sheria hii; vyombo vya habari vinafaa kutangaza na kuchapisha habari na masuala yenye manufaa kwa taifa kadiri itakavyoelekezwa na serikali.

Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2019. Licha ya muswaada wa sheria hii kuzua mjadala mkali na sintofahamu kwa wadau wa siasa na umma kwa ujumla mnamo Januari 2019, lakini aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Daktari John Pombe Magufuli mnamo Februari 2019, aliweza kupitishwa sheria hii. Sheria hii haikuleta tija kwa umma, kwani kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa sheria hii hazikuwa na ufanisi mzuri wakati wa utekelezaji wake. Sheria ilibinya uhuru na haki ya wananchi kushiriki na kufanya mikusanyiko ya amani.

Kadharika, sheria hii ilikiuka haki ya wananchi kupata habari kwasababu sheria iliwalazimu watu binafsi na asasi za kiraia kupata kibali kutoka serikalini kabla ya kutoa elimu ya uraia kwa umma. Kupitia sheria hii pia, msajiri wa vyama vya siasa alipewa mamlaka ya kuingilia mfumo wa uchaguzi wa ndani wa vyama vya siasa kwani sheria inampa nguvu ya kuitisha taarifa kutoka kwa vyama vya siasa, kusimamisha wanachama na kufuta vyama vya siasa kutokana na sababu atakazozitaja.

Kabla sheria haijapitishwa na Rais. Muswaada wa sheria husika hupitia hatua kadhaa kama vile; kutangazwa kwenye gazeti la Serikali, kusomwa bungeni na kisha kupata ridhaa ya Rais. Na katika utaratibu wa kutunga sheria, ibara ya 100(1), ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inaeleza kuwa kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano nautaratibu katika bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika mahakama au mahali pengine nje ya bunge.

Kwakuwa bunge ni chombo cha uwakilishi cha wananchi, hivyo ni muhimu wabunge watumie nafasi na wajibu wao kwa mujibu wa katiba, kutunga sheria zinazoweza kuleta matokeo au mabadiliko chanya katika jamii ili kuimarisha, kukuza na kulinda utawala wa sheria. Ufanisi mzuri wa sheria utasaidia kupunguza au kuondoa kabisa mvutano kati ya serikali, wananchi na wadau wa sheria kama vile mashirika au asasi za kiraia. Kadharika ufanisi mzuri wa sheria utasaidia katika kuhamasisha, kukuza na kulinda haki za binadamu.
 
Upvote 4
Back
Top Bottom