Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
KWA UFUPI
Inashangaza kuona kuwa, pamoja na kuwachuja wauguzi hao waliokuwa wameomba kupewa mafunzo ya uuzaji wa maduka ya dawa muhimu, bado walikuwapo wengine waliobainika kutokuwa na ujuzi wowote katika fani hiyo.
Habari kwamba watu 462 kati ya 1,205 waliokuwa wakisailiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Baraza la Wafamasia katika Mkoa wa Mwanza wamebainika kuwa na vyeti feki ni za kushtua na kutia hofu kubwa. Kubainika kwa watu hao kulijitokeza wakati walipokuwa wakifanyiwa mafunzo kuhusu uuzaji wa dawa katika maduka yanayouza dawa muhimu ambayo hutolewa tu kwa maelekezo ya madaktari.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza juzi, Mratibu wa Mpango wa Maduka Muhimu unaoratibiwa na Baraza la Wafamasia, Richard Silumbe alisema Mkoa wa Mwanza unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu waliobainika kuwa na vyeti bandia. Kwa mujibu wa mratibu huyo, asilimia 46 ya watu waliofika katika usaili huo walikuwa na vyeti bandia vinavyodaiwa kutolewa na baadhi ya hospitali mkoani humo. Alisema hali hiyo haikubaliki, hasa kutokana na ukweli kwamba watu hao wapo dukani na wanaendelea kuwahudumia wananchi.
Kama tulivyodokeza hapo juu, hali hiyo ni ya kushtua na kutia hofu kubwa. Inapofikia wakati sekta muhimu kama ya afya ikavamiwa na watumishi ambao hawana sifa ya kutoa huduma nyeti kama hizo, ni ushahidi kwamba hakuna mwananchi hata mmoja aliye salama.
Inashangaza kuona kuwa, pamoja na kuwachuja wauguzi hao waliokuwa wameomba kupewa mafunzo ya uuzaji wa maduka ya dawa muhimu, bado walikuwapo wengine waliobainika kutokuwa na ujuzi wowote katika fani hiyo.
Jambo lililozidi kuleta utata ni kuwa, kati ya watu hao 1,205 waliofika katika usaili huo, 743 vyeti vyao havikuonyesha kasoro yoyote. Lakini ulipokuja mtihani, wengi wao walishindwa kujibu maswali hata yale ambayo hayahitaji mtu kuwa amesomea mambo ya afya. Hapo ndipo ilipogundulika kwamba wengi wao walikuwa wauguzi feki na vyeti walivyokuwa navyo vilikuwa vya kuazima au kukodi.
Hatuoni haja ya kusisitiza umuhimu wa kuwapo maduka hayo ya dawa muhimu, kwani mpango huo umeanzishwa kwa ajili ya kutoa huduma sahihi kwa wananchi tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma. Wizara ya Afya inasema umuhimu huo ndiyo hasa ulioifanya kuamua kujiridhisha kuhusu watoa huduma hao kwa kuwapatia mafunzo ili waweze kutoa huduma za uhakika.
Kwa kiasi fulani, wizara husika lazima ikubali kubeba lawama kwa kuacha tatizo la vyeti bandia kukua hadi kufikia kiwango hicho. Ni jambo lisiloeleweka kwa watumishi wa sekta hiyo nyeti kupewa ajira kwa kutumia vyeti bandia pasipo kugundulika. Swali ambalo ni vigumu kupata jibu ni kuwa, ni watu wangapi nchi nzima hadi sasa wameathirika kiafya kutokana na kupewa huduma na watu hao ambao hawana sifa isipokuwa wanatumia vyeti feki?
Nani asiyejua kwamba wamiliki wengi wa maduka hayo ya dawa muhimu wanakodi vyeti vya mafamasia ili maduka hayo yaweze kusajiliwa na kufanya biashara, kama wafanyavyo askari wanaokodisha silaha kwa wahalifu na kulipwa fedha kila wanapofanya hivyo?
Tunadhani sasa ni wakati mwafaka kwa Serikali kufanya msako nchi nzima ili kuwanasa mafamasia feki na maduka ya dawa muhimu yenye wahudumu wasio na vyeti wala sifa.
Msako huo ufanyike kuanzia makao makuu ya mikoa na wilaya hadi tarafa, kata, vijiji na vitongoji. Ni kwa njia hiyo tu tutaweza kuepuka maangamizi ya maisha ya wananchi.http://www.mwananchi.co.tz/uchambuzi/-/1597604/1725312/-/m3pcl7z/-/index.html