Wakati Masakata ya ufisadi BoT na Richmond yakiendelea, tujikumbushe la IPTL
Joseph Mihangwa Machi 5, 2008
Raia Mwema
WATANZANIA wengi bado wanalikumbuka sakata la ugomvi kati ya kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na TANESCO kati ya mwaka 1999 na 2001 kuhusu gharama za ujenzi wa mtambo wa umeme wa Tegeta na bei ya umeme baada ya TANESCO kugundua udanganyifu mkubwa katika mkataba wao.
Katika tafrani hiyo, IPTL iliifikisha TANESCO kwenye mahakama ya kimataifa ya usuluhishi ikidai mkataba uheshimiwe na ilipwe dola milioni 4.6 au Shilingi bilioni 4.6 kwa mwezi kwa kutumia huduma za IPTL chini ya mkataba wa miaka 20.
IPTL ilishinda kesi katika mazingira ya kutatanisha pamoja na mahakama hiyo kukiri kwamba gharama za mkataba wa IPTL ziliongezwa kinyemela kwa dola milioni 24. TANESCO inatakiwa kulipia huduma hizo iwe imezitumia au haikuzitumia. Hili tutalifafanua baadae.
Licha ya TANESCO na baadhi ya watendaji wakuu wa serikali kudai mahakamani kwamba IPTL ilighushi hati, na kwamba kulikuwa na mazingira ya rushwa katika mkataba huo, mahakama hiyo iliendelea kuagiza kuwa mkataba uheshimiwe. Hiyo maana yake ni kwamba kwa miaka 20 mfululizo watumiaji wa umeme na walipa kodi watabeba mzigo wa kulipa Shilingi bilioni 4.6 kwa umeme wasiouhitaji wala kuwa na uwezo wa kuugharamia.
Haya ni matokeo ya hujuma ya wajanja wachache waliohusika na mkataba huo.
Katika makala hii, kwa kutumia vyanzo vyetu mbalimbali, tutaelezea kwa kifupi chimbuko la sakata hili na athari lililoleta kwa uchumi wa nchi na kwa walipa kodi wa Tanzania kwa ujumla. Sakata hili lilianzaje na ilikuwaje?
Ni hivi: Ukame mkubwa uliotikisa mwaka 1994 ulisababisha kukauka kwa Bwawa la Mtera ambalo ndicho chanzo kikubwa cha umeme unaotumika nchini. Kwa sababu ya ukame huo, mgawo wa umeme ukaikumba nchi na uzalishaji viwandani ukashuka. Waliokuwa na uwezo walinunua jenereta ndogondogo za umeme kwa matumizi ya nyumbani ambapo akina mie walirejea kwenye enzi za ujima za kutumia vibatari.
Zilikuwa enzi za giza nene, enzi za dhiki na wajanja wakaamua kutumia hali hiyo kujinufaisha. Kwa vipi?
Serikali ilifikia uamuzi wa haraka wa kupata umeme wa dharura. Hapo ndipo baadhi ya wafanyabiashara nchini wakaja na mawazo ya ufumbuzi wa tatizo hili. Mmoja wa hao alikuwa Reginald John Nolan, mfanyabiashara wa Kiingereza (Irish) aliyependekeza serikali inunue mtambo wa umeme (turbine) wa megawati 109 kutoka kampuni ya General Electric, na umeme uliotarajiwa kuzalishwa ungemgharimu mtumiaji mara nne zaidi ya umeme unaozalishwa na jenereta zenye kutumia mafuta ya dizeli.
Bila kujali yote hayo, mpango wa Nolan uliendelea vizuri huku ukiungwa mkono na kupewa nguvu na wanasiasa na watendaji wa ngazi za juu nchini. Karibu na mwisho wa maelewano (deal ) mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini, Bwana Notoo Konishi alishtushwa na gharama za mradi huo na kumwandikia Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Nishati na Madini, kumtahadharisha juu ya pendekezo la Nolan; akionya kwamba kama serikali ingekubali pendekezo hilo tete, Benki ya Dunia ingejitoa kuhudumia sekta ya nishati nchini na wafadhili wengine wangejiengua pia.
Kwa huruma na nia njema, na kwa lengo la kuiepusha Tanzania na mpango hatari wa Nolan, Benki ya Dunia ilijitolea kununua mitambo miwili ya megawati 75 kama msaada ili kuongeza uwezo wa TANESCO na kupunguza tatizo la umeme nchini.
Ikumbukwe pia kwamba mwezi mmoja kabla ya mazungumzo kati ya Nolan na serikali kuanza, kampuni nyingine ya Malaysia ya Mechmar, ilifikia makubaliano na Wizara ya Nishati na Madini ya kutengeneza umeme chini ya mpango wa Independent Power Project (IPP) kama njia ya kuendeleza uhusiano wa nchi masikini za Dunia ya Tatu na kufanya Mechmar kuwa kampuni kubwa ya kwanza kuwekeza katika sekta ya umeme nchini. Na kwa mara nyingine mpango wa Nolan ulizidiwa kete na Mechmar, licha ya kupigiwa debe na watendji serikalini na waunganishi wa "michuzi" wa kimataifa
Inasemekana, Waziri wa Mipango wa wakati huo, Horace Kolimba (hayati), pengine kwa nia njema kabisa, ndiye aliyefanya uwekezaji wa kampuni ya Mechmar ukubalike nchini. Inasemekana Kolimba alitembelea Malaysia, Julai, 1994 na kueleza tatizo la mgawo wa umeme nchini Tanzania na azma ya serikali ya kulimaliza haraka. Serikali ya Malaysia ilimkutanisha na wawekezaji wa nchi hiyo na baadaye akawaalika kutembelea Tanzania ili kutathmini hali.
Kwa kufanya hivyo, Kolimba hakujua kwamba alikuwa akikaribisha mwekezaji mumiani nchini.
Datuk Baharudan wa kampuni ya Mechmar alifanya mazungumzo na Waziri wa Maji Nishati na Madini pamoja na Meneja Mkuu wa TANESCO, Naibu Kamishna wa Nishati na Msaidizi wa Rais wa mambo ya uchumi ambao wote walithibitisha kwamba TANESCO na serikali ziliukaribisha "ukombozi" huo kutoka Mechmar.
Mwezi mmoja baadaye mkataba wa "kifo" ulitiwa sahihi na IPTL ikaanzishwa. Ni nani huyu IPTL? Alifikaje Tanzania? Alisaidiwa na nani kuliteka soko la umeme nchini?
IPTL ni ushirika wa kibiashara nchini kati ya Shirika la Mechmar (Malaysia) linalomiliki asilimia 70 ya hisa na kampuni iitwayo VIPEN Ltd ya mjini Dar es salaam inayomiliki asilimia 30 ya hisa. VIPEN ilianzishwa na Bakari Somji (hayati). VIPEN ni mashuhuri kwa kuunganisha mipango ya kibiashara nchini kati ya makampuni ya kimataifa na serikali ya Tanzania na kupata misaada kutoka nje.
Aidha mmoja wa watu viunganishi waliotumwa na VIPEN kwa kasi hiyo ni Mtanzania mmoja ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa VIPEN na IPTL. Huyo alipewa jukumu hilo kwa sababu ya kufahamiana vizuri na wakubwa wa Benki Kuu (BOT). Wakati mwingine kiunganishi huyu huambatana na msafara wa Rais katika ziara mbalimbali nje ya nchi kama mwakilishi wa sekta binafsi nchini. Kwa jinsi hii alikuwa katika nafasi nzuri kupitisha "sumu" ya IPTL kwa urahisi serikalini.
Nini kilichokubaliwa chini ya mkataba kati ya IPTL na TANESCO? Kilitekelezwa kama ilivyokusudiwa?
Wakati serikali ikiidhinisha mkataba wa miaka 20 wa kuuziana umeme (power purchase agreement) kati ya IPTL na TANESCO, mwaka 1995, ilibainisha kwamba IPTL wangejenga mtambo wenye kutumia mafuta ya dizeli wa megawti 100; yaani slow speed diesel power plant (SSD) pale Tegeta, jijini Dar es salaam, kwa gharama ya dola 163.5 na kwamba gharama za ujenzi zilikadiriwa kufikia dola milioni 126.39.
Ilikubaliwa pia kwamba ushuru kwa matumizi ya umeme huo ungetegemea gharama halisi za ujenzi
Lakini badala yake, na bila ya kukubaliana wala taarifa kwa TANESCO, IPTL, kwa makubaliano na kampuni Martsila, iliamua kujenga kwa bei hiyo ya dola milioni 163.5 mtambo wa dizeli (MSD) ambapo bei yake halisi ilikuwa dola milioni 85.7. Mtambo wa MSD unataka gharama kubwa kuhudumia na una maisha mafupi.
Kufuatia uamuzi huo wa upande mmoja, bei ya mtambo huo hafifu ilipanda kinyemela kwa asilimia 33 kutoka dola milioni 85.7 hadi dola milioni 111.2 pamoja na kwamba ulikuwa hafifu kwa sifa.
Mnamo Septemba 1997, tatizo la umeme nchini lilirejea tena. Hata hivyo, safari hii sio kwa sababu ya ukosefu wa mvua bali ilitokana na TANESCO kukosa fedha za kulipia ushuru wa mafuta ya kuendeshea kutoka nje.
Kilichoshangaza ni kwamba wakati Hazina ilikataa kuiondolea TANESCO ushuru wa mafuta wakati huo huo iliendelea kutoa msamaha wa kodi kwa wafanyabiashara wa mafuta ya kula walioagiza kutoka nje. Kwa wengi, hiki kiliashiria rushwa kwa viongozi wa serikali ili kuibeza na kuikwaza TANESCO isiweze kupata nafasi ya kujiimarisha na kuipa nafasi IPTL kusimika makucha yake katika sekta ya umeme.
Hii ilikuwa wazi kwa sababu hofu ya IPTL ilikuwa dhahiri kufuatia kusimikwa kwa mitambo ya megawati 73 pale Ubungo (Oktoba 1995) na mwingine wa megawati 180 (uliofadhiliwa) uliotarajiwa kukamilika kule Kihansi. Mitambo hiyo miwili ingetosheleza mahitaji ya watumiaji; na hivyo kutishia hali ya kuendelea na mradi wa IPTL.
Kama tulivyoona mwanzo kwamba Benki ya Dunia haikupendelea mradi wa IPTL. Uligubikwa na mizengwe tangu mwanzo kwa hiyo benki hiyo iliendelea kuiwekea ngumu IPTL; huku baadhi ya vigogo nchini wakiendelea kuupigia debe mradi huo kwa nguvu zote.
Oktoba 1997, Benki hiyo iliishinikiza serikali ya Tanzania kutia saini mradi wa gesi wa Songas uliofadhiliwa na serikali ya Canada baada ya kuona serikali inataka kuutelekeza na kuukumbatia mradi wa IPTL. Lengo la mradi huu lilikuwa kuipatia Tanzania umeme rahisi.
Ingawa ulibuniwa kabla ya ule wa IPTL na serikali ya Canada kulipia dola milioni 200, serikali ilijifanya kuufumbia macho huku ikiendelea kuijengea jina IPTL na kutoa msamaha wa kodi na upendeleo mwingine. Kama isingekuwa hila za IPTL kwa kushirikiana na baadhi ya vigogo nchini, Tanzania ingekuwa imeanza kuvuta umeme wa gesi tangu mwaka 1997.
Ujanja wa IPTL ulijidhihirisha zaidi Desemba 1997 pale ambapo, kupitia taarifa yake yenyewe, ilidanganya kwamba kitendo cha kubadili aina ya mtambo wa SSD uliokusudiwa kujengwa Tegeta na kujenga mtambo duni na rahisi wa aina ya MSD, kwa gharama zile zile, eti kilifahamika mapema na kuidhinishwa na TANESCO yenyewe.
Taarifa hiyo ilipingwa vikali na Mkurugenzi Mtendji wa TANESCO, Baruany Luhanga kwamba ni ulaghai wa hali ya juu wa IPTL.
Kwa upande wake, IPTL ilidai kwamba mtambo wa awali katika mkataba (PPA) aina ya SSD haukukusudiwa bali uliokusudiwa ni aina ya MSD na kwamba hili lilikuwa kosa la uchapishaji. IPTL waliendelea kusisitiza uhalali wa gharama za ujenzi kwa dola milioni 163 na kukataa kwa jeuri kutoa ushahidi wa hati za awali kwa madai kwamba tenda hiyo ilikuwa ya wazi na kwamba hati hizo zilikwishapotea.
Ni kutokana na ubabaishaji huu wa IPTL kwamba Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Maji na Madini, Patrick Rutabanzibwa alilazimika kumshauri Rais afute "biashara" hii na IPTL na kwa bahati nzuri aliuona ukweli huu ingawa hakuweza kuufuta mradi huo, na badala yake alionya juu ya "mchezo mbaya" wa IPTL kwa Watanzania.
Hapo, Katibu Mkuu huyo alifanikiwa kumshawishi Rais aagize mkataba huo ushughulikiwe kwa njia ya usuluhishi na kituo cha kimataifa cha usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji (International Centre for the Settlement of Investment Disputes for Arbitration)- ICSID, mjini London, Novemba 1998.
Wakati wa kusikilizwa kwa mgogoro huo, kitu cha kushangaza ni kwamba yule muunganishi wa dili zote kati ya IPTL na vigogo serikalini alikiri waziwazi (Mei 8, 2000) kwamba baada ya mvua kubwa za El-Nino kunyesha mwaka 1997, hapakuwa na haja tena ya mradi wa IPTL. Mahakama ilibaini kuwa mradi rahisi wa mtambo wa MSD uliongezwa bei kinyemela kwa dola milioni 24; lakini ikaamua mkataba uendelee kwa sababu mabadiliko kutoka mtambo wa SSD yalifanyika mapema kwa vigogo serikalini na TANESCO kuridhia.
Kufikia hapo, kuna maswali mengi ya kujiuliza juu ya uhalali wa mradi huu wa IPTL. Maswali kama je; licha ya Benki ya Dunia kuonya juu ya athari za mradi huu kwa uchumi wa taifa, kwa nini viongozi serikalini waliruhusu uendelee?
Ukweli mwingine uliojidhihirisha ni kwamba chini ya mkataba wa awali ,IPTL ilitakiwa kujenga nyumba 37 kwa dola milioni 7.6 lakini zilipunguzwa hadi 10 na gharama za ujenzi huo (dola milioni 7.6) zikaongezwa kwa zaidi ya asilimia 130. Hata hivyo, nyumba zilizojengwa ni sita tu!
Akitoa ushahidi kwenye ICSID, mmoja wa wanasheria wa TANESCO alibainisha wazi kwamba haikuhitajika mtaalamu wa majengo kutambua kwamba nyumba sita za ghorofa moja zisingeweza kugharimu dola milioni 7.6 sawa na Shilingi bilioni 7.6.
Ushahidi uliopo unabainisha pia kwamba kampuni ya Nartsila iliuza mtambo wa umeme kama huo (MSD) kwa nchi zingine za Kiafrika kwa dola milioni 60 tu. Kwa hiyo, kwa kuongeza gharama mara mbili, IPTL na Nartsila (kwa njama za pamoja) walijihakikishia faida kubwa kuweza kurejesha fedha zao kabla hata mradi huo haujaanza kufanya kazi.
Kwa kuwa serikali ilifahamu fika juu ya uwezekano wa kutumia vyanzo mbadala kuweza kujitosheleza kwa umeme, kwa nini ilighairi kuvitumia vyanzo hivyo na badala yake ikaendelea kuupigia debe mradi wa IPTL?
Tumeona kwamba ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Maji na Madini pamoja na Mkurugenzi Mtendji wa TANESCO, Baruany Luhanga ndio pekee waliojitoa mhanga kuzungumza kwa uwazi na ukweli juu ya "mchezo mchafu" wa IPTL hapa nchini. Je vigogo wengine walilionaje hilo na walichukua hatua gani?
Tumejifunza nini kwa sakata hili? Tuyaangalie kwa ufupi tu maoni ya baadhi ya viongozi kuhusu sakata hili.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali iliupitia mkataba wa IPTL na TANESCO kwa niaba ya serikali na kuona ulikuwa "unakubalika kabisa kabisa".
Hata hivyo, kinyume chake washauri wa TANESCO (Canada and Hunton and Williams walitoa taarifa ya uwazi na ukweli kwamba mradi wa IPTL ulikuwa haufai, ulikuwa mradi wa kipindi kirefu wakati tatizo uliolenga kutatua lilikuwa la kipindi kifupi, ulikuwa wa gharama kubwa bila sababu na tatu ulizidi mahitaji halisi ya umeme nchini kwa hiyo watumiaji na walipa kodi wangevikwa gharama za kuzalisha umeme wasiouhitaji. Aidha, gharama zake ziliongezeka na kuwa kubwa kupindukia ili kuinufaisha IPTL.
Vilevile washauri hawa walibainisha kwamba mkataba uliwapendelea mno IPTL na kuifunga nchi shingoni kulipia huduma zisizohitajika. Aidha mkataba haukuweka ukomo wa muda wa kukamilisha ujenzi na kwamba gharama zilizopaswa kulipwa na TANESCO zingelijadiliwa baada ya mradi kukamilika. Aidha kutokuwapo muda wa kukamilisha mradi ilikuwa ni kuiumiza TANESCO kutokana na kupanda kwa gharama.
Hatuwezi kusema kwamba ziara ya Waziri wa Nishati na Madini nchini Malaysia, Februari 1997, haikuwa ya manufaa kwa nchi; lakini tunashangazwa sana na tamko lake baada ya kurejea kutoka ziara hiyo kwamba haikuwa vibaya wala ukinzani (contradiction ) kwa miradi ya IPTL na Songas kuendeshwa kwa pamoja wakati akifahamu fika kwamba kuendesha miradi yote ingeathiri uchumi duni wa nchi.
Jumuiya ya kimataifa kwa upande wake ilishindwa kuvumilia sakata hili. Katika kikao cha ushauri kati ya Tanzania na mashirika ya wafadhili ya kimataifa, Desemba 1997 na Mei 2000, mjini Dar es salaam, mara mbili mjumbe wa Umoja wa Ulaya (EU), Peter Christiansen alitoa hisia zake kwa kusema "Umoja wa Ulaya unasikitishwa na hali ya serikali ya Tanzania kukaa kimya kwa vitendo vya viongozi wake wa ngazi za juu wa chama na serikali kuhusishwa na (mchezo mchafu) sakata la IPTL.
Naye mwandishi wa shirikisho la Reuters, Mark Dodd Julai 1998 alisikitika kuondoka nchini bila mahojiano na Rais Mkapa amuulize mantiki ya uhalali wa mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Waziri wa Madini na Nishati kutia sahihi mkataba wa IPTL ambao IMF tayari iliueleza kuwa "ni mzigo usiotakiwa kwa uchumi wa taifa na kwa walipa kodi wa nchi hii."