Kwa biashara inayoweza kututajirisha ni kuku tu!!!!, sasa wote tukiuza kuku nani atatuuzia kilauri na kitimoto, si tutapata shida!
Halafu hizi dvd na vitabu si ni njia tu ya kufikisha ujumbe kama ujumbe huu ulivyonifikia kwa kupitia ka smartphone kangu, kwa hisani ya JF, au dvd na vitabu zina alergy (sijui nimepatia?) na utajiri?
Afu wamesemaje vilee! ... Eeeh eti kuku wa kisasa ni mataahira, mimi ndio leo nimejua, ninachoshangaa zaidi ni nini kimewafanya hawa kuku wa kisasa wakawa mataahira?
Sijazipinga hizo DVD na vitabu moja kwa moja lakini je ni kweli zinakufikisha kwenye mafanikio. By the way naandaa chapisho ambalo nitalileta hapa JF ambalo litaleta mwongozo mzima wa ufugaji wa kuku wa kienyeji. Hebu soma Trela yake kabla sijalileta chapisho lote, halafu naomba sana Watanzania tusiwe na moyo wa kukata tamaa kama ambao ninauona kwa baadhi ya watu hapa.
UFUGAJI BORA WA KUKU WA KIENYEJI
SEHEMU YA KWANZA
UTANGULIZI
Napenda kumshukuru mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kwa namna moja au nyingine kutoa mchango wangu kwa mtindo huu. Huu ni kama mwongozo tu wa nini utakabiliana nacho au unatakiwa kufanya katika zoezi zima la ufugaji wa kuku wa kienyeji. Nimeamua kuuleta kwenu wana JF ili kwa mtu mwenye malengo ya kufanikiwa kupitia ufugaji wa kuku ajue mlolongo mzima na changamoto ambazo atakabiliana nazo.
A. KWA NINI KUKU WA KIENYEJI?
1. Wastahimilivu wa magonjwa lakini ni muhimu wakikingwa na magonjwa ya kuku kama mdonde, ndui ya kuku n.k ili kuweza kuwaendeleza.
2. Wana uwezo wa kujitafutia chakula ardhini.
3. Wana uwezo wa kuatamia mayai, kutotoa na kulea vifaranga na ustahimilivu wa mazingira magumu kama ukame, baridi n.k
4.Nyama na mayai yake vina ladha nzuri kuliko kuku wa kisasa.(PATA SUPU YA KUKU WA KIENYEJI ILI UTHIBITISHE)
5. Wana uwezo wa kujilinda na maadui kama mwewe n.k . Pamoja na sifa hizi ni muhimu muhimu kuku hao wakapewa matunzo mazuri, wakawekwa kwenye mabanda mazuri, wakapewa maji na chakula cha kutosha.
B. FAIDA ZA KUKU WA KIENYEJI.
Faida ni nyingi na zinafahamika lakini nitaeleza zile ambazo kwa wengine huenda zikawa ni ngeni kwao.
- Mayai huweza kutumika kwa tiba. (Pata maelezo jinsi yai la kuku wa kienyeji linavyoweza kutumika kwa tiba kutoka kwa wataalam wa tiba mbadala)
- Kiini cha njano cha yai kinaweza kutumika kutengenezea mafuta ya nywele (shampoo)
- Manyoya yake yanaweza kutumika kama mapambo.
Fuga kuku upate faida kwa kuzingatia:
Chanjo ya mdondo kila baada ya miezi mitatu na chanjo ya ndui mara mbili kwa mwaka
Zuia viroboto, utitiri na minyoo.
Chagua mayai bora kwa ajili ya kuatamiza
Panga kuuza kuku kwa makundi uongeze kipato
Kula mayai na kuku kadri uzalishaji unavyoongezeka.
Kipato unachokipata utenge pia na kiasi kwa ajili ya uendelezaji wa kuku
C: MAPUNGUFU
Yako mapungufu mengi yanayofahamika lakini hapa naomba niweke lile la muhimu zaidi. MAGONJWA kama mdondo na ndui huathiri ufugaji wa kuku kutokana na kutokuzingatia kuchanja kuku kwa wakati.
D: KABILA ZA KUKU WA KIENYEJI
Kuna maelezo ya kusisimua sana kuhusu makabila ya kuku wa kienyeji, hata hivyo kuna ugumu kidogo kuweza kuyachanganua makabila hayo kutokana na muingiliano mkubwa wa vizazi kati ya aina mbalimbali za kuku hao. Hata hivyo kuku hawa wana tofauti za kimaumbile zinazosaidia kwa kiasi fulani kutambua uwepo wa baadhi ya makabila ya kuku. Kabila hizi pia zinahusishwa kwa kiasi kikubwa na eneo kuku wanakotoka. Baadhi ya kuku wa kienyeji wanaweza kutambuliwa kwa maumbile yao Mfano:
a. Kishingo - kuku wasio na manyoya shingoni
b. Njachama au Nungunungu - Hawa ni wale wenye manyoya yaliyosimama.
c. Kibwenzi - Ni wale wenye manyoya mengi kichwani.
d. Kibutu- Hawa hawana manyoya mkiani
Mwingiliano wa vizazi unaweza ukasababisha kuku kuwa na aina ya maumbile mchanganyiko. Mfano kuku aina ya kuchi anaweza kuwa na alama ya kishingo, Njachama, Kibwenzi au Kibutu.
Hivyo kabila za kuku zifuatazo zinaweza kutambuliwa kama ndiyo kabila za kuku wa kienyeji kulingana na maumbile yao na maeneo wanakotoka.