Labda niandike kwa namna nyingine nitumie takwimu na data nyepesi!
Mtu A anakaa Kibamba ambayo ni Kilometa 25 kutoka katikati ya jiji la Dar. Mtu huyu tumpe jina Masumbuko.
Masumbuko ana gari lake, ki-Rav4 na anafanya kazi pale NDC kama mtathmini wa Takwimu. Ana mke na watoto watatu.
Kila siku, Masumbuko anaamka saa 10 asubuhi, ili aanze kujiandaa kwenda kazini na kuwaanda Watoto wanaokwenda shule. Masumbuko anaondoka nyumambani kwake pale Kibamba ambako ni katikati ya Kwembe na Mbezi Luis saa 11 na nusu alfajiri. Safari yake ya kwenda kazini inamchukua masaa mawili au mawili na nusu. Kazini anatakiwa aingie saa 2 kamili asubuhi.
Tangu anapoingia barabara kuu ya Morogoro kuelekea mjini Dar Es Salaam, Masumbuko anasuasua kwenye foleni kwa masaa mawili huku gari likipiga kati ya gia ya kwanza na ya pili kutokana na msongamano. Kila baada ya kilometa moja au mbili kuna matuta seti tatu.
Masumbuko anaingia kazini saa 2 kasorobo, hapo katumia masaa mawili na karibu lita 6 za mafuta.
Muda wa kazi kwa kila siku kwa Masumbuko ni masaa 8 ya kazi tangu akiingia saa 2 asubuhi mpaka saa 11 jioni. Mahesabu ya haraka yanasema Masumbuko anaweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kwa masaa matano na nusu (5:30) kwa siku na hayo masaa mengine ni muda wa majeraha.
Ikifika saa 11 jioni, Masumbuko anaanza safari yake ya kurudi Kibamba na anakwama kwenye foleni kwa muda wa saa kaibu tatu, na hapa anamaliza lita karibu 8 za mafuta!. Haingii nyumbani mpaka saa 2 usiku.
Akifika nyumbani ndio asalimiane na mke na watoto, awajulie hali, aandalie mchicha wake pale nje kwa kutumia kurunzi na ahangaike kwenda kujaza maji kwenye Tanki la maji. Lakini kwa bahati mbaya, hakuna umeme, kuna mgao na maji pamoja na kuwa yana nguvu kidogo, lakini hawezi kujaza mapipa yake ya maji mpaka umeme urudi saa 5 usiku!
Masumbuko anakaa macho mpaka umeme unaporudi hapo saa 5 usiku na anatumia saa moja kujaza mapipa yake ya maji na anapoingia kitandani kulala ni saa 7 Usiku.
Ikifika saa 10 asubuhi, jogoo la pili linapowika, Masumbuko keshaamka, anajiandaa haraka ili awaone watoto na akimbilie kuwahi foleni.
Leo ni Jumatano, masumbuko ameamua kuacha gari na kupanda Kipanya, nacho kinachukua muda ule ule wa masaa mawili asubuhi lakini anapata ahueni maana nauli ni shilingi 1,500/= kwa safari yake mpaka mjini na si kumaliza lita 6 akiwa ndani ya Rav 4 yake.
Akiwa kazini, leo JUmatano, Masumbuko anawaza kama kutakuwa na maji akirudi nyumani maana Dawasco wamekata maji wakidai kuna maji yanaletwa na Wachina. Ama Masumbuko anatafakari kama kutakuwa na umeme akifika nyumbani na kama foleni itakuwa na ahueni maana kapanda kipanya!
Siku nzima Masumbuko katawaliwa na mawazo ya tangu alipoamka na atarudi vipi nyumbani ili awahi kuwaona watoto wake, aende kununulia wale kuku zake chakula na apate kupumzika kwa kutosha.
Matokeo ya tija na ufanisi kwa siku ya leo kutoka kwa Masumbuko ni saa moja na nusu la yyeye kufanya kazi kwa ufanisi na tija.
Jioni inafika Masumbuko huyo anakimbilia Posta mpya akapande Kipanya arudi Kibamba.
Sasa Masumbuko ni lini na ni wakati gani atakuwa na amani ya moyo kuwa anaweza kuleta uwiano wa maisha yake ya nyumbani na ajira yake? Je Masumbuko atawezaje kuendelea kuwa na tija na ufanisi ikiwa siku nzima akiwa kazini anawazia kero za yeye kuja kazini kwa kuganda kwenye foleni, kukosekana maji na umeme na kikubwa kukosa muda wa kukaa na mke na watoto kwa muda unaotosha?
Je ile ndoto ya Maisha Bora kwa kila Mtanzania itatimilikaje ikiwa Masumbuko anasumbuka kila siku kwa hizi kero pamoja na kuwa ana ajira?