esther mashiker
JF-Expert Member
- May 29, 2018
- 616
- 552
KAMPUNI tatu kati ya tisa zilizoomba kununua ufuta katika wilaya tatu za mkoa wa Lindi kwa njia ya mnada zitanunua kilo milioni 1.8 kwa bei ya Sh 2,860 na Sh 2,852. Hiyo ilibainika katika mnada wa mwanzo kata ya Mbondo wilayani Nachingwea mkoani Lindi, kwenye eneo linalosimamiwa na chama kikuu cha ushirika cha Runali mkoani Lindi.
Kwa mujibu wa taarifa, ufuta huo ni wa wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale na ulikuwa mnada wa kwanza kwa chama hicho cha Runali msimu huu. Katika mnada huo wa kwanza kwa msimu huu kwa wakulima wa wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale na kuendeshwa na chama kikuu cha Runali na kushuhudiwa na mkuu wa wilaya Nachingwea, Rukia Muwango wito ulitolewa kwa wakulima kulipwa kulingana na mwongozo wa mkoa.
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango alisema pamoja na kuridhishwa na mnada ulivyoendeshwa na wakulima kuridhia kuuza alisisitiza malipo ya mkulima yamkie ndani ya siku tatu za kazi baada ya kuuzwa mnadani.
Naye, Kaimu Mrajis wa Ushirika Mkoa wa Lindi Robert Nsunza aliwataka viongozi wa vyama vya msingi kuandaa taarifa ya malipo kadri ya walivyopokea ghalani na kuiwasilisha benki haraka iwezekanavyo ili malipo kwa mkulima kupitia akaunti yake yaweze kulipwa kama ilivyofanyika kwa chama cha Lindi Mwambao katika minada ya wilaya za kilwa na Lindi.
Akifunga mnada huo, Mwenyekiti wa chama kikuu cha Runali, Hassan Mpako alisisitiza wakulima kuzingatia ubora wa ufuta wanaopeleka ghalani ili kuvutia wanunuzi na kuimarisha bei. Hata hivyo, wako baadhi ya wakulima walieleza kuridhishwa na bei huku wakionesha wasiwasi wa kutolipwa kwa wakati.
Wakizungumza kwa wakati tofauti wakulima Shaban Makeru, mkazi wa Mirui Liwale na Lucas Mchaya mkazi wa Mbondo Nachingwea walisema kwamba kila mtu anaelewa kinachoendelea katika korosho na kutaka hilo lisijitokeze katika ufuta. Msimu uliopita wa mwaka jana ufuta uliuzwa hadi Sh 3,800 kwa kilo na kuamsha ari ya wakulima kulima kwa wingi zao hilo kwa kutumia mbegu bora zinazozalishwa na kutatiwa na taasisi ya utati wa kilimo TARI Naliendele.