Wanataaluma wamepitia katika kumbo la wakati ambao historia imewaachia jeraha kubwa la fedheha juu ya kile kinachoitwa uhuru wa kufikiri. Uhuru pekee wa wanataaluma na nafasi muhimu ya maisha ya Mwanazuoni ni uhuru wa kufikiri.
Uwezo na tabia za Wanazuoni kuyaangalia masuala mbalimbali katika mawanda na matao yake, kuachilia maslahi binafsi, itikadi, imani na kuonesha mitazamo kiuchambuzi ni tabia ambayo imekuwa ikizimwa kila wakati. Mwanataaluma anapochambua jambo kitaaluma anachohitaji ni uhuru wa kufikiri juu ya jambo hilo.
Vyuo vinavyozalisha wanataaluma, vinapaswa kuwa majukwaa huru ya kitaaluma na siyo majukwaa huru ya kuminya uhuru wa kufikiri. Tunajiuliza ipo wapi mamlaka ya wanataaluma kama wamepokwa uhuru wao wa kufikiri?. Ni kama tunaambiwa fikiri hapa mpaka hapa ila huko kwingine acha.
Tunaweza tukaogopa kusema juu ya uhuru huu kwa kujua au kutojua lakini kwa hakika yapo madhara makubwa sana pale Jamii inapokosa uhuru wa kufikiri na tena kufikiri tofauti. Utofauti wetu katika kufikiri ni zao la mitazamo, itikadi na imani lakini si kile tunachokifikiri. Tunachokifikiri ndicho kinachotuunganisha licha ya ukweli kuwa imani, itikadi na mitazamo yetu inaweza ikatifautiana sana.
Jamii ya wanataaluma "think tanks" inapojengewa ukasuku wa kufikiri katika mkondo uleule unapendwa na wateule na kunyimwa uhuru wake wa asili wa kufikiri madhara yake hukigharimu kizazi kizima.
Jamii inapofikiri kwa hofu haiwezi kufikiri kwa kina hali inayofanya mambo yake mengi kuwa na utatuzi wa juu juu huku ikiacha sababu chanzi "root causes". Kufikiri ni hali ya kuumba, kufikiri ni kufanya vitu vitokee, kufikiri ndiyo kazi pekee ya kiumbaji kupitia maarifa.
Akili yenye uhuru wa kufikiri ndiyo inayoweza kuhoji haswaa na tena kuihoji na mamlaka kwa sababu katika uhuru wa kufikiri mamlaka ni nidhamu, mamlaka ni heshima, mamlaka ni ukweli na ukweli ndiyo uhuru wenyewe.
Kusema ukweli kitaaluma ni mtihani mkubwa sana kwa sababu ya kongwa kubwa la madhila ya kukosa uhuru wa kufikiri. Kinachosemwa ni kile chenye maslahi fulanifulani na si katika mawanda yote "multiple dimensions"
Mitazamo tofauti juu ya ujenzi wa hoja ni jambo jema kitaaluma lakini madhila ya kukosa uhuru wa kufikiri yanawafanya wanataaluma kujitenga kimaslahi.