Magonjwa ya Zinaa ikiwemo kaswende yanachangia mtu kupata ugonjwa wa Afya ya akili ikiwemo Kupoteza Kumbukumbu, Msongo wa Mawazo na Mania.
UKIMWI pia unatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa matatizo ya Afya ya Akili kwa Wagonjwa.
UKIMWI pia unatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa matatizo ya Afya ya Akili kwa Wagonjwa.
- Tunachokijua
- Kaswende (Syphilis) ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na viini vya bakteria vijulikanavyo kama Treponema pallidum.
Ugonjwa huu husambazwa kwa njia ya mgusano wa via vya uzazi yaani ngono kupitia uke, mdomo pia sehemu ya haja kubwa.
Pia, watoto wachanga wanaweza kupata ugonjwa huu kutoka kwa mama zao kupitia kondo la uzazi.
Ugonjwa huu unaweza kudhuru uume, uke, mlango wa uzazi, sehemu ya haja kubwa, mrija wa mkojo, ubongo, midomo, mfupa, figo na ini.
Maambukizi ya kaswende husababisha vipindi tofauti vya dalili, na hivi hujulikana kama kaswende ya hatua ya kwanza, ya pili na ya tatu na hatua ya nne.
Midomo ya mtu mwenye ugonjwa wa Kaswende
1. Hatua ya kwanza
Huonekana wiki 3-4 baada ya kuingiliwa na vimelea vya ugonjwa huu. Huanza kuonekana kwa mchubuko mdogo wa mduara ambao mara nyingi huwa hauna maumivu.
Mchubuko au kidonda hiki hutokea kwenye eneo mahsusi ambapo vimelea vya ugonjwa vilitumia kuingia mwilini.
Inaweza kuwa mdomoni, sehemu siri au sehemu ya haja kubwa.
Mchubuko huu ambao unaweza kudumu hadi miezi 3 kabla haujapotea huwa ni chanzo kikubwa cha kusambaa kwa ugonjwa huu wakati wa kushiriki tendo la ndoa.
2. Hatua ya pili
Hii ni hatua ya kati. Ngozi huanza kutengeneza mabaka na koo huanza kusumbuliwa na vidonda.
Dalili zingine za hatua ya pili ya ugonjwa wa kaswende ni Maumivu ya kichwa, Uchovu, Homa, Kupungua kwa uzito wa mwili, Kunyonyoka kwa nywele na Maumivu kwenye maungio ya mifupa.
3. Hatua ya tatu
Ni hatua ambayo ugonjwa hujificha, huacha kuonesha dalili zozote za uwepo wake.
Dalili zilizokuwa zinaonekana awali hupotea, lakini bakteria wa ugonjwa huendelea kuwepo mwilini wakizaliana na kuongezeka.
4. Hatua ya nne
Hii ni hatua ya mwisho ya ugonjwa wa kaswende.
Mara nyingi huanza kuonekana baada ya kupita miaka 10-30 tangu vimelea vya kwanza viingie mwilini. Hatua hii ni hatari kwa uhai na huambatana na dalili zifuatazo;
- Upofu
- Kupotea kwa uwezo wa kusikia
- Matatizo ya mfumo wa fahamu hasa ubongo na uti wa mgongo
- Kuharibika kwa mifupa
- Kupoteza kumbukumbu
- Homa ya uti wa mgongo
Mhudumu wa afya ataelezea matumizi ya dawa pamoja na dozi sahihi kwa kadri atakavyoona inafaa.
Aidha, mtu anaweza kujikinga na ugonjwa huu kwa kuwa mwaminifu kwenye uhusiano wa kimapenzi na kutulia na mpenzi mmoja au kuepuka ngono zembe kwa kutumia kinga.
Kaswende husababisha matatizo ya Afya ya Akili ikiwemo Kupoteza Kumbukumbu?
Kwa mujibu wa Kituo cha Udhibiti na Kinga ya Magonjwa (CDC), pasipo kupata tiba sahihi, ugonjwa wa kaswende unaweza kusambaa kwenye ubongo na mfumo wa fahamu.
Madhara haya yanaweza kutokea kwenye hatua yoyote ya ugonjwa huu ambapo dalili zake zinaweza kuwa maumivu makali ya kichwa, uchovu wa misuli pamoja na changamoto mbalimbali za afya ya akili ikiwemo kupungua kwa uwezo wa kutunza kumbukumbu, kufikiri na kufanya maamuzi.
Haya yanathibitishwa pia na ripoti ya Tugce Toptan et al "Neurosyphilis: a case report" (2015), inayofafanua mgonjwa wa miaka 40 aliyepatwa na changamoto za afya ya akili kutokana na kuugua Ugonjwa wa Kaswende.
Agosti 24, 2023, Gazeti la Mwananchi lilichapisha pia makala ikimnukuu Daktari bingwa wa afya ya akili, Mfumo wa fahamu kutoka Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili-Mirembe, Dk Damas Andrea aliyesema kuwa ugonjwa huo unatabia ya kutoisha kabisa na badala yake unakwenda kwenye mfumo wa fahamu na kubaki katika eneo hilo kwa muda mrefu.
"Kama ulipata ugonjwa wa kaswende ukiwa na umri wa miaka 20 ukafikiri umepona, lakini kwa bahati mbaya unakwenda kwenye mfumo wa fahamu kisha unaibuka ukiwa na umri wa miaka 35 mpaka 60 ndio unajitokeza kwa njia ya aina nyingine ikiwemo changamoto ya kupoteza kumbukumbu, kuona au kusikia vitu ambavyo havipo"
Pia Dk Andrea alitaja magonjwa mengine yanayoweza kusababisha afya ya akili kuwa ni UKIMWI huku akisema kwa sasa Wizara ya Afya inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha vituo vya kutokea huduma za matibabu ya UKIMWI, pia huduma ya afya ya akili inatolewa.
Kwa mujibu wa Taasisi ya afya ya NIH, watu wenye ngozi nyeupe (wazungu) huwa na hatari kubwa zaidi ya kupatwa na changamoto hii kwa kiwango kinachofikia mara 2-3 kuliko watu weusi huku wanaume wakiwa na hatari kubwa zaidi ya kupatatwa na changamoto hii kuliko wanawake.
Kwenye baadhi ya kanda za Afrika, wastani wa visa vinavyofikia 2300 huripotiwa kuwepo kwenye kila kundi la watu 100,000.
Aidha, ni muhimu kuthibitisha kwanza uwepo wa maambukizi ya Kaswende kabla ya kuendelea na hatua ya pili ya kupima athari za maambukizi hayo kwenye afya ya akili ya mhusika.
Pamoja na maelezo mengine ya kitabibu ambayo JamiiForums imeyapata kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo tafiti na maelezo ya wataalam wa afya ya binadamu, imethibitika bila shaka kuwa ugonjwa wa Kaswende unaweza kusababisha changamoto za afya ya akili kwa mtu anayeugua asipopata matibabu sahihi.
Kwa mujibu wa Kituo cha Udhibiti na Kinga ya Magonjwa (CDC), dozi sahihi ya changamoto hii ambayo kitaalamu huitwa Neurosyphilis ni Aqueous crystalline penicillin G 18–24 million units kwa siku, inayotolewa kwa 3–4 million units kwenye mishipa ya damu kila baada ya saa 4 kwa siku 10–14.
Njia mbadala ni kutumia sindano za Procaine penicillin G 2.4 million units mara 1 kwa siku na vidonge vya Probenecid 500 mg mara 4 kwa siku, vyote kwa siku 10-14.