SoC03 Ugonjwa wa Shinikizo la Damu ni wa Wote Sasa, Tuwajibike Kuudhibiti

SoC03 Ugonjwa wa Shinikizo la Damu ni wa Wote Sasa, Tuwajibike Kuudhibiti

Stories of Change - 2023 Competition

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Joined
Jul 30, 2022
Posts
321
Reaction score
691
Utangulizi
Miaka ya nyuma, magonjwa mengi yasioambukiza yalitawala sana nchi zilizoendelea, magonjwa haya ni shinikinizo la juu la damu, kisukari, saratani, magonjwa ya figo, na kadhalika; ambayo pia yaliwapata watu wenye umri mkubwa, yaani kuanzia miaka 60 na kuendeleza. Wakati huo, nchi nyingi zinazoendelea (ikiwemo Tanzania), magonjwa yaliyotawala sana ni yale ya kuambukiza, kama kipindupindu, homa ya matumbo, magonjwa ya kuhara, malaria, kifua kikuu, na kadhalika.

Katika karne hii ya 21, mambo yamegeuka, wakati magonjwa haya yakipungua nchi zilizoendelea; katika nchi zinazoendelea, pamoja na uwepo wa magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukiza yameongezeka kwa kasi kubwa kwa watu wa karibu marika yote na yanaongoza kwa vifo!

Kilelezo Na. 1: Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mloganzila
Hospitali a Muhimbili Mloganzila 2.png

Chanzo: www.mloganzila.or.tz

Kilelezo Na. 2: Wananchi Waliofika Hospitali Kufanyiwa Uchunguzi

Wananchi Wakisubiri Vipimo 2.png

Chanzo: www.mloganzila.or.tz

Kilelezo Na. 3: Baadhi ya Wataalamu Wakichukuwa Vipimo vya Awali Ikiwemo Shinikizo la Damu na Kiwango cha Sukari kwa Wananchi Waliofika Kupata Huduma.


Wataalamu Wakichukuwa Vipimo Na 3.png

Chanzo: www.mloganzila.or.tz

Ukweli huu unathibitishwa na taarifa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili – Mloganzila (Nov. 14, 2021), kwamba, zaidi ya asilimia 70 ya vifo vinavyotokea nchini na duniani husababishwa na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Kisukari, Pumu, Shinikizo la juu la damu.

Pia, kwa mujibu wa gazeti la Dira Makini (Mei 17, 2023), Mheshimiwa Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, amesema, hapa nchini takwimu kutoka kwenye mfumo wa ukusanyaji taarifa za Afya (DHIS2) zinaonesha kuwa jumla ya wagonjwa 2,535,281 walitibiwa magonjwa yasiyoambukiza kwenye vituo vya afya nchini kwa mwaka 2017. Amesema wagonjwa hao wameongezeka hadi kufikia 3,440,708 kwa mwaka 2021. Ongezeko hili (wagonjwa 905,427 kwa miaka mitano) ni sawa na ongezeko la asilimia 9.4.

Katika Makala hii, nitajikita zaidi katika ugonjwa wa shinikizo la juu la damu kwakuwa miongoni mwa magonjwa haya yasiyoambukiza, ndio unaoongoza kwa watu kuugua na vifo.

Shinikizo la Juu la Damu
Kwa mujibu wa Kliniki ya Cleveland, Shinikizo la Juu la Damu ni hali ya msukumo wa damu katika mishipa ya ateri kuwa mkubwa kuliko kawaida na kwa muda mrefu.
Watoa huduma za afya huita shinikizo la damu “muuaji wa kimya” kwa sababu, kwa kawaida hauna dalili zozote.

Shinikizo la damu ni kipimo cha msukumo wa damu katika kuta za mishipa. Shinikizo lako la damu lina namba mbili:
Namba ya juu ni “Systolic Blood Pressure” ambayo hupima msukumo kwenye kuta za ateri wakati wa mapigo, moyo unaposinyaa.
Namba ya chini ni “Diastolic Blood Pressure”, ambayo hupima msukumo kwenye kuta za ateri katikati ya mapigo wakati moyo unatanuka.

Shinikizo la damu hupimwa katika kipimo cha milimita za zebaki (“Millimeters of Mercury – mmHg”).
Shinikizo la damu kwa kawaida linatakiwa kuwa 120 au chini yake (Namba ya juu) na 80 au chini (Namba ya chini). Mtu anayekuwa na namba juu ya hizi atakuwa na shinikizo la juu la damu.

Kielelezo Na. 4: Kipimo cha Shinikizo la Damu
Kipimo cha shinikizo la damu.png

Chanzo: High Blood Pressure

Kielelezo Na 5: Ukweli Kuhusu Shinikizo la Juu la Damu

Hypertension Image 1.png

Chanzo: https://www.heart.org/en/health-topics/high-blood-pressure

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya Tanzania (Apr. 13, 2022), Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amebainisha kuwa asilimia 26 ya watu wazima wenye umri wa miaka kati ya 25 hadi 64 wana shinikizo la Juu la damu, hali inayosababishwa na mtindo wa Maisha ikiwemo ulaji wa vyakula vya mafuta mengi, matumizi ya pombe kupita kiasi na kutofanya mazoezi.

Aidha, Dkt. Sichalwe amesema kuwa, taarifa za utafiti zilizofanywa katika baadhi ya hospitali za rufaa zimebaini kuwa, wastani wa watu 19 katika kila watu 100 wanaolazwa kwa tatizo la shinikizo la juu la damu hufariki dunia.

Sambamba na hilo, ameweka wazi kuwa, hali ni mbaya zaidi kwa wagonjwa wa kiharusi, ambapo katika kila watu 100 wanaolazwa, watu 39 wanafariki kwa tatizo hilo la shinikizo la juu la damu.

Kwa mujibu wa gazeti la Dira Makini (Mei 17, 2023), Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, alisema, ugonjwa wa shinikizo la damu ndio ulioongoza miongoni mwa magonjwa yasioambukiza, ambapo waliongezeka kutoka wagonjwa 688,901 kwa mwaka 2017, hadi kufikia wagonjwa 1,345,847 kwa mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 95.4 katika kipindi hicho.

Waziri Ummy ameendelea kusema, “Takwimu hizi zinatuonesha kwamba wagonjwa hawa wenye shinikizo la damu wameonekana kuongezeka takribani mara mbili zaidi kwa kipindi cha miaka mitano (Health Statistical Bulletin, 2022)

Sababu za Kuongezeka kwa Ugonjwa wa Shinikizo la Juu Tanzania
Kwa mujibu wa taarifa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila (Nov. 14, 2021), “Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu umekuwa ukiongezeka zaidi nchini kutokana na mtindo wa maisha ikiwemo ulaji usiyofaa, matumizi ya chumvi, msongo wa mawazo, matumizi ya wanga kwa wingi kuliko mbogamboga, pamoja na matumizi ya mafuta kwa wingi na kutokufanya mazoezi” amesema Dkt. Mwanaada Kalima.

Nini cha Kufanya Kupunguza Ugonjwa wa Shinikizo la Juu la Damu?
Kuacha ulaji usiofaa! Hii ni shida kubwa kwa watu wengi, hasa vijana; kwani wengi hawali milo inayopendekezwa, kama wanga kiasi, mboga za majani, matunda na kadhalika, badala yake hupendelea vyakula vya kukaanga (kama viazi – maarufu kama chips, nyama nyekundu) na vyakula vilivyokobolewa (mfano, wali na sembe).

Kupunguza au kuacha matumizi ya pombe; kuepukana na matumizi ya tumbaku, na kuepukana na msongo wa mawazo.

Kuwa na utamaduni wa kupima afya mara kwa mara, kubaini magonjwa mbalimbali, pamoja na shinikizo la juu la damu.

Kufanya mazoezi ya mwili kila siku, pamoja na kunywa maji walau lita moja na nusu kila siku.

Serikali na wadau wengine kutoa elimu kwa umma jinsi ya kuudhibiti ugonjwa huu.

Kila anayethibitika kupata ugonjwa huu, ahudhurie hospitali na kufuata maelekezo yote ya tiba.

Matumizi ya tiba asili. Sambamba na tiba nyingine, wataalamu wa tiba asili wahusishwe kutoa tiba kwa ugonjwa huu, pamoja na mengine.

Hitimisho
Kila mmoja awajibike kujilinda na kulinda wengine dhini ya shinikizo la juu la damu ili kutunza nguvukazi ya taifa.

Marejeo
Dira Makini (Mei 17, 2023), Waziri Ummy Atoa Tamko Kuhusu Shinikizo la Juu la Damu.

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila (Nov. 14, 2021), Magonjwa Yasiyoambukiza Kinara katika Kusababisha Vifo Nchini.

High Blood Pressure: What You Need To Know

High Blood Pressure

Wizara ya Afya Tanzania (Nov. 10, 2022), Magonjwa Yasiyoambukiza, Ajali na Afya ya Akili Yanazuilika.

Wizara ya Afya Tanzania (Apr. 13, 2022), Asilimia 26 Ya Watu Wazima Wana Shinikizo la Juu la Damu.
 

Attachments

  • Hospitali a Muhimbili Mloganzila .png
    Hospitali a Muhimbili Mloganzila .png
    286 KB · Views: 13
Upvote 7
Kuna haja ya serikali kudhibiti uzalishaji na/au uingizaji nchini wa bidhaa zinazochochea magonjwa yasiyoambukiza (ikiwa ni pamoja na shinikizo la juu la damu).
 
Kuna haja wataalamu wa lishe kufikisha elimu ya lishe bora kila mtaa/kijiji, maana lishe duni na ulaji hovyo ndio sababu kuu ya maradhi kama ya shinikizo la juu la damu.
 
Back
Top Bottom