Uharibifu wa mazingira kupitia ukataji miti hovyo ni tishio kubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya - Mbeya

Uharibifu wa mazingira kupitia ukataji miti hovyo ni tishio kubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya - Mbeya

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
51
Reaction score
38
Uharibifu wa mazingira kupitia ukataji miti hovyo umeendelea kuwa tishio kubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Makala hii inaangazia sababu kuu zinazochochea kasi ya upotevu wa misitu katika wilaya hiyo.
WhatsApp Image 2026-04-16 at 16.38.27.jpeg
Kilimo cha Tumbaku na Nishati ya Kuni
Sehemu kubwa ya misitu ya Chunya inapotea kwa kasi kutokana na upanuzi wa kilimo cha tumbaku, ambalo ni zao kuu la biashara kwa wenyeji wa eneo hilo. Ripoti ya mwaka 2018 ya Beijing Wake Group on Environment and Development inaonesha kuwa, upanuzi wa mashamba na utumiaji wa kuni kukaushia tumbaku unachangia uharibifu wa misitu kwa asilimia 40 hadi 50 katika wilaya hiyo.

Mbali na tumbaku, mahitaji makubwa ya kuni na mkaa kwa matumizi ya nyumbani na biashara katika maeneo ya mijini yanachangia kupunguza misitu ya asili kwa asilimia 20 hadi 25.

RIPOTI JF.png
Kulingana na ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya mwaka 2017, mkoa wa Mbeya unategemea nishati ya kuni kwa asilimia 68 na mkaa kwa asilimia 7.4 kwa ajili ya kupikia, ambapo kiasi kikubwa cha nishati hiyo kinatoka wilayani Chunya.

4-16.jpg
Wafanyabiashara wa maeneo hayo, kama Veronica Mwasongole anayeendesha mgahawa huko Chalangwa, wanaeleza kuwa wananchi wengi wanashindwa kumudu gharama za nishati mbadala kama gesi, kwani mtungi mdogo wa kilo sita unauzwa kati ya Shilingi 25,000 hadi 29,000. Hali hii inawafanya waendelee kutegemea kuni na mkaa.

Uchimbaji wa Dhahabu na Ajira kwa Vijana
Utafiti mwingine wa mwaka 2025 uliofanywa na Chuo Kikuu cha Marekani unaonesha kuwa uchimbaji mdogo wa dhahabu, hasa katika vijiji vyenye migodi, unachangia uharibifu wa misitu kwa asilimia 25 hadi 30.

Kutokana na ukosefu mkubwa wa fursa rasmi za ajira, vijana wengi wamebaki bila kazi na hivyo kujingiza kwenye biashara haramu ya mkaa na ukataji miti ili kujipatia kipato. Mkazi mmoja wa Chalangwa, Ali Kumbise, anaeleza kuwa ukataji miti na uchomaji mkaa umekuwa kama kimbilio pekee la vijana kujikwamua kiuchumi.

Hata hivyo, usafirishaji wa mkaa huo umekuwa ukifanyika kwa njia za panya kwa kutumia pikipiki (boda boda) usiku na mchana. Elias Malima, Mhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani Chunya, anabainisha kuwa usafirishaji wa mkaa kwa kutumia pikipiki ni haramu na hatari kwa usalama wa barabarani, na wamekuwa wakipambana nao na kuwakamata wale wanaokiuka sheria.

Siasa na Udhaifu wa Usimamizi wa Sheria
Pamoja na kuwepo kwa Sheria ya Misitu Namba 14 ya Mwaka 2002, utekelezaji wake umekuwa na kusuasua kutokana na kuingizwa kwa masuala ya kisiasa.

Mbunge wa Jimbo la Lupa, Masache Kasaka, anakiri kuwa siasa zimeathiri sana udhibiti wa uharibifu wa misitu, hasa nyakati za uchaguzi.

Baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiwaingilia kati na kuwalinda wavunjaji wa sheria (wavamizi wa misitu ya hifadhi) kwa kisingizio cha kulinda kura zao.

"Watu wengi wanaenda kuvamia maeneo ya misitu, lakini mnapotaka kwenda kuwatoa wanakuja na kisingizio kwamba sisi ni wanachama wa chama fulani... mkienda kuwatoa hawa tutapoteza kura zenu. Lakini tunasema sheria ni sheria tu. Sheria haiangalii chama wala cheo cha mtu." — Mbunge Masache Kasaka.

Uchunguzi unaonesha kuwa misitu mingi katika kata za Sangambi, Makongolosi, na Chokaa haina mipango thabiti ya usimamizi (management plans) kutokana na gharama kubwa za uendeshaji, hali inayochochea udhaifu wa usimamizi wa rasilimali hizo.

Viongozi wa vijiji, akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji cha Chalangwa, Tadeo Mwagame, na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Chokaa, Blandina Chambo, wanaeleza kuwa wanaendelea kushirikiana na TFS kuweka ulinzi kwenye magambo ya misitu, ingawa changamoto bado ni kubwa kutokana na nguvu ya mtandao wa wahalifu hao.

Andiko la: Mwanaisha Makumbuli
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.

Pia soma ~
Dkt. Mzige: Misitu inapopotea Chunya -Mbeya, kiwango cha hewa safi ya oksijeni kinashuka, hewa ukaa ikiongezeka
 
Back
Top Bottom