Tatizo madogo tukiwapa sapoti huwa mnakengeuka sana na kuwa wajeuri kama si viburi. Unakuta dogo nimekukuta kitaa hauna ramani nimekuleta kwenye biashara yangu nikahitaji sana uaminifu wako.
Nikakupa hifadhi sehemu ya kuishi, uhakika wa chakula na posho kama sio mshahara na kuanza kukufundisha biashara na mifumo yake na nikikutaka uwe mwaminifu na mtendaji muadilifu.
Ila mkishaona mnategemewa tu mnaanza ingia tamaa mnataka mtupindue wakubwa zenu na kuanzisha biashara nje ya hizi tulizowapa msimamie.
Mnaanza kuwa wajeuri, mnaanza kutuibia na kufinya faida zetu ili ziingie mifukoni mwenu. Mnasahau kuwa tumewatoa sehemu ambapo mlikuwa hamna pa kujishika na hamkuwa na heshima kwenye jamii. Ila mkipata kajeuri ka uhakika wa hata laki mbili kwa mwezi mnasahau kuwa maisha ni magumu sana na hakuna aliyekuwa akiwajali kipindi mpo nje ya mfumo. Ila sasa tumewasitiri kwenye tumifumo twetu huku ili wadogo zetu at least muitwe wanaume mnaojitafutia na wenye kipato mnatuona sisi ni takataka na kuanza kuota pembe.
Ndio maana muda mwingine tunasoma hizi nyuzi zenu za toba na maombi tunatamani kutoa sapoti ila sasa tukiwaza kwamba miezi michache ijayo pengine mwaka kuna uwezekano mkubwa mkakengeuka basi tunaingia baridi na kuishia kuduwaa.
Tutafika kweli maendeleo ya kiuchumi ya juu kama hatuna discipline ya kazi na kujituma plus uaminifu kwa wale waliotushika mkono nyakati ambazo kila mtu alituona takataka na jamii ilitukataa huku Dunia ikituelemea?!
Madogo mjifunze discipline, nazungumza haya kwa machungu ya moyoni maana yamenikuta kuna bwana mdogo alikuwa anasota kitaa anachakaa. Alikuwa anaishi na mama yake mkubwa ambaye alishamchoka anamwambia arudi tu kijijini.
Nilimjua kupitia shangazi yangu. Nikamwita dogo nikaketi nae kuzungumza kwa kirefu sana na kumpa inspiration ya tofauti sana hadi dogo akajiona ni silaha ya Nyukilia iliyokuwa imefichwa store bila kutumika.
Nikatafuta location sehemu, na nikaingia gharama ya vifaa vya kufungulia biashara ya chips. Dogo nikamwambia wewe sasa utakuwa manager hapa na nitakuletea watendaji wawili hapa. Na nikapata msaada wa bwana mdogo m'moja alikuwa anakuja nusu siku kumfundisha namna ya kupika vitu vya biashara. Baadae nikampa mpango kazi na namna ya kusimamia pesa na namna atakuwa ananitumia. Nikamuelekeza kuwa tutafanya hivyo huku tukiongeza matawi ya biashara zingine yeye awe manager wangu na nitakuwa namlipa mshahara kamili kama tutaenda vema ingawa kwa kuanza nitakuwa ninamposho.
Mwanzo tulianza vema na hadi nikamtafutia sehemu yake ya kuishi nalipia mimi, usafiri wa boda boda ulikuwapo so hakukuwa na shida ya kutoka na kufika nyumbani na ofisini. Dogo akakiri toka aondoke home kwa mama yake mkubwa amekuwa akipewa heshima na maneno niliyomfundisha ni kweli kabisa kwa sasa anajisikia imara sana.
Sasa shida ikaanza dogo alipokutana na kademu kake huko na kukapa mimba, akaanza mapicha picha na shida ambazo nilishamuonya sana awali.
Hapa dogo akawa anafeli maeneo mengi sana jambo ambalo lilinifanya kumuweka benchi na kupata kazi ya kutafuta mtu mwingine ambaye sikuwa na mipango nae kama tuliyopanga nae. Dogo akaingia kwenye bodaboda biashara ambayo mama yake na ndugu zake wameshamkataza sana tokea awali kuwa si salama kwake.
Naona mambo yake sijui yameendaje sababu hata yule binti walikuja kuachana na akawa namuona mara anaendesha bajaji mara ameanza kutumia viroba, nilikutana nae wakati fulani ameenda kuishi na wenzake ile ya kupanga chumba masela mpo hata watatu chumba cha 40,000/-.
Alikuwa anaonyesha kuwa anatamani sana kurudi ila mimi sikuwa tayari kumpokea tena maana kashaonyesha utomvu wa nidhamu. Kama amechagua maisha haya akaona kusimamia masharti niliyompa ni kazi basi itakuwa ni ngumu sana kwenda nae mbali.
Hizi ndizo changamoto huwa tunashindwa kumudu katika kuwasapoti madogo. Mnadharau watu wanaowapa dhamana. Sasa yule dogo kama tungeshirikiana vizuri mimi nina uhakika kwa sasa angekuwa anapata mshahara mzuri sawa na mwajiriwa wa serikalini na maisha yangeenda. Ila sasa madharau na kuchukulia poa biashara za chini za sisi wajasiriamali wa kitaa.