IslamTZ
JF-Expert Member
- Nov 22, 2010
- 309
- 182
Abuu Kauthar
Miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika, awamu sita za uongozi kuanzia mwaka Desemba 9, 1961 hadi leo Desemba 9, 2021. Kila awamu ilikuwa na mambo yake kutokana na mazingira ya wakati huo.
Julius Nyerere
Awamu ya kwanza chini ya Rais Julius Kambarage Nyerere ilikuwa ni ya kujenga utaifa (nation building) kwa kukifanya Kiswahili lugha ya taifa, kuunganisha Watanzania kupitia programu kama za kuchanganya wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali katika shule za serikali, jeshi la kujenga taifa na kadhalika.
Pia, ni kipindi ambacho yalifanyika majaribio ya ujenzi wa uchumi kwa misingi ya siasa ya kijamaa, ambao hata hivyo ulifeli kabisa. Uhuru wa watu binafsi na uhuru wa vyombo vya habari ulibinywa mno, Vyombo pekee vya habari vilivyokuwepo vilikuwepo wakati huo ni vya serikali, vya chama (CCM), na jumuiya zake.
Kimataifa, kilikuwa ni kipindi ambacho Tanzania iling’ara mno kutokana na siasa zake za kutofungamana na upande wowote na kushiriki kikamilifu katika ukombozi wa bara la Afrika katika nchi zilizchelewa kupata uhuru wake zikiwemo Angola, Msumbiji, Zimbabwe, na Afrika ya Kusini.
Hata hivyo, Nyerere alikuwa na undumilakuwili wakati mwingine. Wakati akihimiza umoja wa Afrika, kwa upande mwingine aliunga mkono watu jimbo la Biafra kujitenga kule Nigeria. Hapa nyumbani, alimudu kupambana na ukabila lakini ajabu ni kuwa yeye mwenyewe anatuhumiwa kwa udini na baadhi ya watu.
Ali Hassan Mwinyi
Ni rais wa kwanza mwenye asili ya Zanzibar na anatathminiwa kama kiongozi wa hovyo aliyeleta uholela hapa nchini lakini labda mazingira aliyorithi nchi yalimtaka afanye hivyo. Ameweka historia ya kushikilia nafasi mbili za urais: wa Zanzibar (na makamu wa kwanza wa rais pia) na kisha akawa Rais wa pili wa Tanzania.
Wakati Mwinyi anaingia madarakani mwaka 1985 ilikuwa dhahiri kuwa ujamaa ulishashindwa na nchi ilikuwa hoi. Mabadiliko yalihitajiwa, hasa kutokana na mbinyo wa mashirika ya kimataifa ya fedha ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB).
Mwinyi alisimamia mageuzi makubwa kutoka uchumi wa kijamaa hadi uchumi wa soko huria. Bahati mbaya soko huria likawa soko holela. Kwa maneno yake mwenyewe, Mwinyi alisema alipofungua madirisha kuingiza hewa nzuri, wakaingia na wadudu wabaya wengi.
Lakini yote kwa yote, kipindi cha Mwinyi kitakumbukwa kama kipindi cha mageuzi makubwa ya kisiasa na hadi ya kiuchumi. Uchumi ulifunguliwa ambapo sekta binafsi ikapewa kipaumbele katika uwekezaji huku serikali ikibaki na kazi ya udhibiti, vyombo vya habari vya binafsi vikarejea, taasisi za kiraia zikaibuka, na ukasimikwa tena mfumo wa vyama vingi.
Benjamin Mkapa
Mzee wa Uwazi na Ukweli, ambaye alitangulia mbele ya haki Julai mwaka jana. Benjamin William Mkapa alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1995 na alikuwa madarakani kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.
Yeye anasifiwa kwa kuleta nidhamu na taratibu serikalini. Mkapa alikuja kupambana na wale wadudu wabaya waliongia wakati Mzee Mwinyi alipofungua madirisha ili hewa ipite. Hata hivyo, yeye hakuhangaika sana na watu, kama ilivyokuwa kwa mwanafunzi wake, rais wa awamu ya tano. Yeye alishughulika zaidi na ujenzi wa taasisi.
Miongoni mwa taasisi alizozianzisha katika kuendeleza utawala bora ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF), Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF), Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) ambayo sasa inaitwa LATRA. Pia zimo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Wakala wa usajili wa Makampuni (BRELA) na Mamlaka ya Ujenzi wa Barabara (TANROADS).
Hata hivyo, makosa katika ubinafsishaji, machafuko ya kisiasa kule Zanzibar mwaka 2001 yaliyopelekea mauaji ya watu 21 na uuzaji wa nyumba za serikali ni mambo ambayo yatabaki kuwa doa katika utawala wake.
Mzee wa Msoga, Jakaya Kikwete
JK ni baba wa demokrasia ya Tanzania. Miaka 10 ya Kikwete katika nafasi ya uwaziri wa mambo ya nje chini ya Rais Mkapa, na kabla ya hapo malezi katika chama, jeshini na serikalini yalimuandaa vema Kikwete kwa urais.
Sawa, wengine wakina Mwinyi na Mkapa waliweka misingi lakini yeye aliulea mfumo huo. Hakuna wakati ambapo vyama vya siasa vya upinzani vilishamiri kama wakati wa miaka 10 ya Jakaya. Tunaweza kusema kilikuwa ni kipindi cha dhahabu cha demorasia yetu.
Sawa ni kweli kuwa katika kipindi cha utawala wake kulikuwa na kashfa nyingi ikiwemo EPA, Richmond, Tegeta Escrow lakini mifumo ya kupambana na ufisadi ilifanya kazi vema. Mdhibiti wa Hesabu za Serikali alifanya kazi kiweledi bila kuingiliwa, huku bunge nalo likifanya kazi yake ya kuisimamia serikali kwa uweledi na uwazi mkubwa.
Ila jamaa alipenda anasa na alipenda kusafiri mno. Safari zake ziligharimu taifa mabilioni ya shilingi, ambapo alipenda pia kubeba washkaji zake huko kutumbua raha. Waandishi wa habari waliokuwa karibu na Ikulu ya Jakaya wana mengi ya kusimulia kwenye eneo hili.
Kutokana na safari zake nyingi, JK hadi hivi sasa amekuwa mtu wa kimataifa sana, akiwa na connection kibao huko nje.
John Pombe Magufuli
Ni vigumu sana kumuelewa bwana mkubwa huyu ambaye sasa ni marehemu. Magufuli anamanisha mambo tofauti kwa watu tofauti. Kwa wapenzi wake, JPM ni mzalendo ambaye hajapata kutokea Tanzania, na kama kuna wa kumfananisha naye basi ni Nyerere tu.
Magufuli alipambana mno na ufisadi lakini pia alikuwa maarufu kwa kukiuka sheria za nchi. Mara nyingi neno lake lilikuwa sheria. Kwa neno lake tu, jambo lolote liliweza kuwa hata kama sheria inakataa. Mifano ni mingi, ikiwemo mariufuku ya mikutano ya siasa.
Magufuli aliminya mno uhuru na haki za binadamu. Kipindi chake kilikuwa kigumu sana kwa vyama vya upinzani, vyombo vya habari na taasisi za kiraia – hawa wote hawakupumua kabisa. Binafsi, niliacha kuandika kwa miaka mitano yote ya Magufuli baada ya kuona sielewi elewi mambo yanavyoenda, vile namna watu wanapotea hovyo, wanapigwa risasi, wanaswekwa ndani, wanafunguliwa mashtaka.
Ni baada ya kufariki huyu bwana mkubwa ndio walau sasa tunaona taasisi za kiraia zinarejea. Huwa nacheka nikiwaona leo wanasiasa, wanahabari na taasisi za kirai wanavyomvimbia mama. Kweli kila mtu na mnyonge wake! Katika kichekesho cha karne, eti REDET wamejitokeza kusema uchaguzi uliopita haukuwa huru wala wa haki!
Kama Jakaya alikuwa baba a demokrasia, Magufuli alikuwa ni dikteta mkubwa zaidi kuwahi kutokea katika taifa letu. Na kwangu udikteta wala sio neno baya, ni aina tu ya utawala. Kwa kutumia huo udikteta, nchi ilisogea. Naweza kuapa kuwa kusingekuwa na migao ya umeme na maji Magufuli angekuwepo!
Katika miaka ya Magufuli mambo mengi yalitokea. Muda ulikuwa unasogea haraka, hujui nini kitatokea kesho sio serikalini tu bali hata ndani ya CCM. Mara sauti zimevuja za viongozi waandamizi wa chama wakimsema vibaya Magufuli, mara kiongozi wa upinzani kapigwa risasi, mara kiongozi mwingine kaharabiwa shamba lake, mara gazeti limefutwa … alimradi maisha yalichangamka.
Ila mwamba lazima tumsifu kwa uamuzi wake wa kukaa nchini isipokuwa kwa safari chache alizoenda nchi za jirani kwani aliokoa fedha nyingi. Magufuli alitengeneza vimagufuli vingine vidogovidogo (Sabayas) na hivi sasa vinapata shida kuendana na mfumo, huku baadhi waking’ang’aniwa mahakamani kwa uhalifu walioufanya wakilindwa na marehemu.
Samia Suluhu Hassan
Rais wa kwanza mwanamke. Mwanzo wengi hawakumuamini kuwa anaweza lakini amefanikiwa kubadili mawazo ya watu wengi. Kumbe si mwepesi kama wengi walivyokuwa wakidhani.
Mama, vijana wanasema, kaupiga mwingi katika miezi hii takriban saba ya utawala wake, ingawa watu wanasema pia kuwa anapokea maelekezo kutoka Msoga. Kama Kikwete, mama naye anasafiri lakini aghlabu huwa ana cha kuonesha kutokana na safari zake ikiwemo ongezeko la wawekezaji na misaada mbalimnbali. Kwa ujumla, mama ni mchakarikaji.
Hata hivyo, mashtaka ya ugaidi yanayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Freeman Mbowe, yanatia doa utawala wake, ingawa amekuwa akijaribu kupunguza athari katika diplomasia yake kwa kuchukua hatua nyingine zinazoonesha nia njema.
Hivi majuzi tu Mkurugenzi wa Mashtaja alitangaza kumfutia mashtaka Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema ambaye amekuwa akiishi nje kwa muda mrefu baada ya kupona majeraha ya risasi alizomiminiwa kule Dodoma katika kipindi cha utawala wa awamu ya tano.
Hata hivyo, kwa sasa tunachoweza kufanya ni kumpa muda Rais Samia tuone wapi atatufikisha huku tukiendelea kumkumbusha juu ya matakwa ya wananchi katika mambo kama Katiba Mpya, Tume Huru ya Uchaguzi na kadhalika.