Mahakama ya Uingereza imemhukumu mwanaume wa Kizimbabwe Guy Mukendi (39) kifungo cha miaka 4 na miezi 3 jela kwa kosa la 'kuhadaa' baada ya kutoa kondomu bila ridhaa ya mwenzake wakati wakifanya ngono.
Guy Mukendi (39) kutoka jiji la Brixton alihukumiwa Alhamisi katika mahakama ya ndani ya London kwa kosa la kumbaka mwanamke mwaka jana.
Uondoaji wa kondomu bila kibali huainishwa kama kubaka chini ya sheria zinazotumika katika mataifa ya Uingereza.
Kulingana na chombo cha habari cha The Guardian, mwanamke huyo alikuwa amekubali kulala na Mukendi kwa sharti la kutumia kondomu lakini aliiondoa bila ridhaa yake.
Maafisa wa polisi wa mji mkuu walifanya kazi na mwathiriwa kupata picha za skrini (screenshots) za ujumbe kutoka kwa Mukendi ambapo aliomba radhi kwa kuivua kondomu akieleza ni kwa sababu alikuwa hajashiriki ngono kwa muda mrefu kisha akafuta ujumbe huo.
Maafisa pia walikusanya ushahidi wa kimahakama kwa usaidizi wa mwathiriwa ambao ulisaidia kupata hatia ya Mukendi ambaye alipatikana na hatia na mahakama tarehe 2 Aprili, 2024.