Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amesifia mafanikio ya serikali yake katika sekta ya elimu kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Akiwa katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma kwa ajili ya kampeni, aliwaeleza wananchi kuwa ingawa kuna watu wanapita wakiibeza serikali kuwa haijaafanya kitu, dunia imetambua mchango wa serikali katika kuandikisha wanafunzi wengi wa shule za msingi na wameamua kuipatia tuzo.
Rais Kikwete alisema hatua ya serikali kufanikiwa kuandikisha wanafunzi kwa asilimia 99 ndiko kumeifanya dunia kutambua mchango huo mkubwa na hatimaye kuamua kuipa serikali tuzo.
Watu wanatubeza, lakini dunia imetutambua kuwa sisi ni kiboko, tukiahidi tunatimiza, sisi ni waaminifu, tuliahidi kuandikisha shule za msingi kwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule na tumefanya hivyo, huwezi
kutulinganisha na vyama vingine, alisema. Kikwete alisema kuwa wakoloni hawakujenga shule na kwamba serikali mara baada ya Uhuru ndiyo ilianza harakati za kujenga shule na yaliyoonekana hayawezekani kwa miaka yote yamewezekana.
Alisema safari ya kila mtoto kuwa na kitabu chake imekaribia na kwamba baada ya muda mfupi, wanafunzi hawatakuwa wakichangia vitabu.
Alisema serikali ya Marekani imeshasaidia vitabu 800,000 na mwakani itatoa vitabu vingine milioni 2.4 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na aliyekuwa Rais wa Marekani, George W. Bush.
Alisema serikali imejitahidi kukarabati hospitali ya Wilaya ya Kongwa na itaendelea kuiboresha pamoja na kununua magari zaidi ya kubebea wagonjwa ili kurahisisha ubebaji wa wagonjwa wakati wa dharura.
Wakati huo huo, Kikwete leo anatarajia kuanza kunguruma katika visiwa vya Unguja na Pemba katika harakati zake za kusaka kura kwa ajili ya kuingia Ikulu kwa awamu ya pili.
CHANZO: NIPASHE