Mkira, inaonekana huelewi maana ya ukabila na unachangaya ukabila na watu wa kabila moja kushikiriana na kufanya mambo fulani kwa pamoja au kutunza mila za kabila lao. Ukabila si kuzungumza lugha ya kabila lako au kula chakula cha kikwenu. Na zaidi ya yote ukabila si kuwa ofisi moja na mtu wa kabila lako! Nikiwakuta wafipa wanne kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa kule Rukwa, naweza kuita huo Ukabila? Je nikienda Songea kwenye uwanja wa Majimaji karibu na soko kuu pale na kukuta wengi waliojiriwa pale ni wangoni na wandendeule nitasema pana ukabila hapo? Au niende pale Makorola, au barabara ya 11 na kumi na mbili karibu na soko "Mjinga" na kukuta kuna wasambaa wengi wanafanya vibarua pale, wabondei na wazigua nitasema kuna ukabila?
Kwa vile umejifatutia ugumu usio wa lazima wa kutokuelewa ukabila ni nini, nimeamua basi kukusaidia kuweza kuona ni wapi umepotoka katika hoja.
Ukabila ni hisia isiyo na msingi katika ukweli (biased) ambayo inamfanya mtu au jamii ya watu kuamini na kukubali kuwa kabila lao ni bora zaidi, lenye kustahili zaidi, na lenye tunu iliyo ndani (intrinsic value) inayotofautisha kabila hilo na makabila mengine. Watu wenye hisia hizi huamini kuwa makabila mengine ni duni kiuwezo na kinafasi na pia makabila hayo mengine hayastahili nafasi zile ambazo mtu wa kabila hilo (linalojihisi bora) anazo. Kwa maneno mengine, Ukabila ni hisia ya ubaguzi utokanao na habari zisizokweli kuwa kabila fulani ni bora zaidi kuliko makabila mengine na hivyo linastahili zaidi katika jamii.
Mara nyingi msingi wa ubaguzi wa namna hii siyo tofauti kubwa ya kabila hilo na makabila mengine bali ni tofauti inayoonekana (perceived difference) ya watu wa kabila hilo na makabila mengine. Inaweza kuwa ni tofauti ya lugha, maumbile, na makazi. Hivyo unaweza kukuta watu wanaozungumza lugha moja wakibaguana kwa misingi ya nani anatoka familia au ukoo gani katika kabila hilo. Hata hivyo hapa tuzungumzie ukabila unaotokana haswa na tofauti ya lugha ya watu na tamaduni za watu ambao rangi yao ni moja (weusi).
Mtu mwenye ukabila wa aina hii hudharau watu wa makabila mengine kwa kuwaona duni na hivyo hujaribu kwa kila aina kukwepa kuhusiana nao na kuwapa nafasi. Je Tanzania kuna ukabila wa namna hii? Kwa ujumla si kweli kwani licha ya watu wa Tanzania kuoleana (wachagga wanaoana na wamasai, wapare), (wangoni wameoana na wasukuma, wahehe, wanyakyusa) n.k... Hivyo katika mahusiano ya watu wetu hakuna ukabila wa namna hiyo kwani tumeingiliana sana kiasi cha kwamba ukianza kumbagua mtu utajikuta unambagua shemeji yako!!
Sasa ni nini kinachotokea maofisini? Mwalimu aligundua tatizo lililoko maofisini ambalo watu wanalitafsiri kama ukabila. Kinachotokea maofisini na sehemu nyingi za kazi ambacho ni cha hatari zaidi kuliko ukabila hewa unaotajwa ni undugunization ambao unatokana na kujuanization. Wengi wanaopata nafasi za kazi, masomo, biashara n.k swali la kwanza ni "je namfahamu", "Je familia yake inafahamika"? Watu hawaulizi je "ni mhaya, mchagga, au mnyakyusa"?! sasa.. bahati mbaya ni kuwa tunafahamiana na kujuana na watu ambao tunatoka zaidi sehemu moja au shule moja n.k Hivyo, kiongozi mchagga yuko tayari kumpa nafasi mtoto wa rafiki yake mkurya kwa vile yeye na huyo baba wa kijana walikuwa wote Tabora Boys miaka ile!!! Sasa mchagga mwingine ambaye anawania nafasi ile ile kwa vile hajuani na huyo bosi.. usitarajie kuwa atapata nafasi!!
Sasa, kama alivyosema Mkandara kwa umahiri mkubwa watu wa kabila moja kuimba nyimbo za kikwao, kula chakula cha kikwao n.k siyo ukabila ama sivyo sisi watanzania tulioko nje ya nchi ambao tumeunganika katika jumuiya mbalimbali za Watanzania tunafanya ubaguzi kwa wale ambao si Watanzania! Watu wajumuiya moja wanaposhirikiana katika shughuli mbalimbali bila ya kujijengea hisia ya kuwa wao ni bora kuliko wote wa makundi mengine au wanastahili zaidi hao siyo wabaguzi. KKK ni wabaguzi kwa sababu wanashirikiana mambo yao nk lakini msingi wa ushirikiano huo ni chuki yao dhidi ya watu wengine. Watusi na Wahutu walipouana mwaka 1994 ni kwa sababu hiyo kuwa lile kabila jingine ni duni na lisilostahili!!
Katika Tanzania, ukabila wa namna hiyo haupo kwa watu wetu kama jumuiya. Hata hivyo, kuna watu ambao mmoja mmoja wanazo hisia hizo. Siku moja nilikuwa nazungumza na rafiki yangu ambaye katika kuzungumza akaamua kujisifia "unajua wachagga ndio most intelligent na smart tribe katika Tanzania, ndio maana wamesoma sana". Sasa, aliyesema maneno hayo binti wa miaka 18 tu na ni wazi hajui historia imetoka wapi, yeye akiona wachagga wamepata nafasi za uongozi hapa na pale anafikiri ni kwa sababu wachagga ndio smart kuliko watu wote! Of course, nilimsaidia kuona kosa la maoni yake na kuanzia wakati huo amekuwa akisahihisha mtazamo huo uliopotoka. Bila ya shaka wapo watu kwenye makabila au dini ambao kutokana na kutokuwa na habari sahihi wamefikia masuluhisho ya kujiona kuwa wao ni bora kuliko watu wa dini au makabila mengine. Watu wanamna hiyo ni lazima waoneshwe upotofu wa mawazo yao ili wajisahihishe! Wale wanaokataa na kung'ang'ania uduni wa watu wa makabila mengine, hao ndiyo wenye ukabila!