Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
TAARIFA KWA UMMA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI
IMETOLEWA JIJINI DAR ES SALAAM
JANUARI 22, 2020
TAKUKURU YAFANYIA KAZI RIPOTI YA UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA: YABAINI KASORO NA KUFANIKIWA KUREJESHA FEDHA JUMLA YA SHILINGI BILIONI 4 KUTOKA KWA WATUHUMIWA
IMETOLEWA JIJINI DAR ES SALAAM
JANUARI 22, 2020
TAKUKURU YAFANYIA KAZI RIPOTI YA UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA: YABAINI KASORO NA KUFANIKIWA KUREJESHA FEDHA JUMLA YA SHILINGI BILIONI 4 KUTOKA KWA WATUHUMIWA
Ndugu Waandishi wa Habari,
Awali ya yote ninawatakia ninyi nyote HERI YA MWAKA MPYA wa 2020.
Nimewaita kwa mara nyingine tena ili kupitia kwenu, tuujulishe umma kazi ya uchunguzi iliyofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU kuhusu RIPOTI YA UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA YA MWAKA 2018/2019, iliyotolewa na Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga - Novemba 26, 2019 na kupewa TAKUKURU, kuchunguza ubadhirifu na Rushwa katika matumizi ya fedha za ushirika nchini Tanzania.
Sisi sote tunafahamu kuwa VITA dhidi ya ubadhilifu wa fedha, mali pamoja na rushwa ni moja ya kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Dkt John Pombe Joseph Magufuli – rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo basi, leo hii tunayo furaha kuujulisha umma moja ya mafanikio ambayo TAKUKURU imeweza kuyafikia katika kufuatilia ubadhilifu wa fedha, mali pamoja na rushwa katika Vyama vya Ushirika nchini.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Mtakumbuka kwamba, takriban mwezi mmoja na nusu uliopita (Novemba 26, 2019) – Jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga alinikabidhi mbele ya waandishi wa habari, MUHTASARI WA UCHAMBUZI WA UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA uliofanywa na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (Co-operative Audit and Supervision Corporation – COASCO) kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019.
Kwa kuwakumbusha tu ni kwamba:
Katika mwaka wa fedha wa 2018/19 Serikali ilitoa maagizo kwa Shirika la COASCO kukagua taarifa za Vyama vyote vya Ushirika nchini.
Kama tunavyofahamu, Vyama vya Ushirika vina jukumu la kuwasaidia wakulima kupata masoko ya mazao yao kwa lengo la kuwaendeleza kiuchumi na kijamii.
Kupitia vyama hivi, wakulima hupaswa kupata utalaam, pembejeo pamoja na mikopo mbalimbali ili kuboresha na kuimarisha kilimo pamoja na masoko ya mazao ya wakulima.
Katika ukaguzi wao, COASCO walibaini kwamba:
• Hadi kufikia Juni 30, 2019 Vyama vya Ushirika vilivyosajiliwa vilikuwa 11,410.
• Kati ya Vyama hivyo, Vyama hai ni 6,463;
• Vyama Sinzia ni 2,844 na
• Vyama ambavyo havipatikani au havijulikani vilipo ni 2,103.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Akinikabidhi taarifa hii, Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga alisema kuwa pamoja na kwamba kuna baadhi ya vyama vilipata HATI SAFI, vilikuwepo vyama vilivyopata HATI CHAFU zilizohusishwa na hoja zenye viashiria vya ubadhirifu wa fedha na mali pamoja na Rushwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi, Vyama vilivyofanyiwa ukaguzi vilikuwa ni 4, 413 kwa mchanganuo ufuatao:
| S/N | AINA YA VYAMA | IDADI YA VYAMA VILIVYOKAGULIWA |
| 1. | Vyama Vikuu (UNION) | 38 |
| 2. | Vyama vya Mazao (AMCOS) | 2,710 |
| 3. | Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) | 1,448 |
| 4. | Vyama vinginevyo | 217 |
| JUMLA | 4,413 |
Kwa mujibu wa Muhtasari wa taarifa iliyokabidhiwa TAKUKURU jumla ya fedha ambayo ilikuwa na viashiria vya ubadhirifu wa fedha na mali pamoja na Rushwa ni zaidi ya shilingi Bilioni 124 (124,053,250,874.00). Hata hivyo, uchunguzi wa Awamu ya Kwanza uliofanywa na TAKUKURU mpaka sasa umefanikiwa kuchunguza kiasi cha Shilingi Bilioni 51 (51,794,221,683.09); Wakati uchunguzi wa Bilioni 72,259,029,190.91 unaendelea.
Katika ufuatiliaji huo, TAKUKURU imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi Bilioni 4 (4,066,162,092.38), ambazo fedha hizo baadhi zimesharejeshwa kwa wakulima na Vyama vya Ushirika ama kutunzwa katika akaunti maalumu zilizofunguliwa kwa ushauri wa Warajisi wa Vyama vya Ushirika na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa ajili ya kuzirejesha kwenye vyama vya ushirika ama wakulima.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Naomba kutumia fursa hii kuishukuru Serikali inayoongozwa na Jemadari wa Mapambano dhidi ya Rushwa nchini – Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutupatia fedha kwa ajili ya kuendesha operesheni hii muhimu ya kurejesha fedha za ushirika na wakulima.
Hivyo tunatoa rai kwa wanaushirika wote nchini, wakiwemo viongozi wa Vyama vya Ushirika na Wafanya Biashara - waliofanya biashara ya kununua mazao ya wakulima au mtu yeyote atakayekuwa ana fedha za ushirika, arejeshe fedha hizo mara moja.
Katika awamu inayofuata ya ufuatiliaji wa fedha hizo – TAKUKURU haitakuwa na HURUMA na mtu yeyote aliye fisadi au aliyetumia rushwa kujipatia faida au aliyeshindwa kulipa fedha yoyote ya ushirika. ATAKAMATWA na kuwekwa ndani, kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka; Akaunti zitasimamishwa na ama kutaifishwa mali zao.
Maagizo haya yametolewa kwenye ofisi zetu zote za Wilaya na Mikoa, kuchukua hatua hizo bila woga kwa mtu yeyote awaye kuanzia leo.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kupitia Operesheni hii maalum, mpaka sasa tayari TAKUKURU imefanikiwa kufanya yafuatayo katika Awamu ya Kwanza iliyochunguza Shilingi Bilioni 51.7 ambazo kati ya hizo- Bilioni 4 zimeshaokolewa katika mikoa yote nchini kama ifuatavyo:
JEDWALI:
PROGRESS REPORT KUHUSIANA NA CHUNGUZI ZA UBADHILIFU WA FEDHA ZA |
VYAMA VYA USHIRIKA NA SACCOS |
NO | MKOA | KIASI CHA FEDHA KINACHOCHUNGUZWA | KIASI CHA FEDHA KILICHOOKOLEWA | KIASI CHA FEDHA KINACHODAIWA |
1 | RUVUMA | 1,027,815,498.00 | 9,968,000.00 | 1,017,847,498.00 |
2 | KILIMANJARO | 3,191,075,967.78 | 38,075,967.78 | 3,153,000,000.00 |
3 | MANYARA | 90,025,324.00 | 9,856,800.00 | 80,168,524.00 |
4 | KINONDONI | 5,509,490,727.00 | - | 5,509,490,727.00 |
5 | KATAVI | 239,090,000.00 | 49,000,000.00 | 190,090,000.00 |
6 | PWANI | 1,097,378,992.53 | 291,400,000.00 | 805,978,992.53 |
7 | MBEYA | 2,585,139,879.04 | 50,701,900.00 | 2,534,437,979.04 |
8 | IRINGA | 2,350,690,451.00 | 133,801,317.00 | 2,216,889,134.00 |
9 | SINGIDA | 132,599,880.00 | - | 132,599,880.00 |
10 | SIMIYU | 132,599,880.00 | 57,178,000.00 | 75,421,880.00 |
11 | ILALA | 3,752,744,920.00 | - | 3,752,744,920.00 |
12 | ARUSHA | 1,137,537,016.25 | 1,256,000.00 | 1,136,281,016.25 |
13 | KIGOMA | 208,803,214.99 | - | 208,803,214.99 |
14 | LINDI | 1,240,305,402.00 | 1,042,362,754.00 | 197,942,648.00 |
15 | NJOMBE | 4,473,574,087.00 | 1,021,472,480.00 | 3,452,101,607.00 |
16 | TANGA | 332,993,600.00 | 10,842,480.00 | 322,151,120.00 |
17 | TABORA | 99,941,274.60 | 69,492,274.60 | 30,449,000.00 |
18 | SHINYANGA | 1,478,633,215.00 | - | 1,478,633,215.00 |
19 | MARA | 646,172,800.00 | 242,982,800.00 | 403,190,000.00 |
20 | TEMEKE | 5,737,141,541.00 | 2,120,000.00 | 5,735,021,541.00 |
21 | MWANZA | 4,613,127,930.00 | - | 4,613,127,930.00 |
22 | KAGERA | 6,449,183,695.00 | - | 6,449,183,695.00 |
23 | GEITA | 26,291,447.00 | - | 26,291,447.00 |
24 | SONGWE | 1,115,916,074.00 | 354,374,673.00 | 761,541,401.00 |
25 | RUKWA | 595,321,710.00 | - | 595,321,710.00 |
26 | MOROGORO | 198,600,359.00 | - | 198,600,359.00 |
27 | DODOMA | 1,854,301,158.00 | - | 1,854,301,158.00 |
28 | MTWARA | 1,477,725,639.90 | 681,276,646.00 | 796,448,993.90 |
51,794,221,683.09 | 4,066,162,092.38 | 47,728,059,590.71 |
Ndugu Waandishi wa habari,
Awamu ya Pili ya uchunguzi wa TAKUKURU utajielekeza katika kuchunguza kiasi cha fedha kilichobakia ambacho ni shilingi Bilioni 72, 259,029,190.91. Kiwango hiki ni sehemu ya Shilingi Bilioni 124 kilichobainishwa na taarifa ya Mhe. Waziri wa Kilimo ikilinganishwa na kiasi cha fedha ambacho tayari TAKUKURU imeshakifikia katika Awamu ya Kwanza ya Operesheni hii.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Fedha zote zilizookolewa na TAKUKURU kwa sasa kama nilivyoeleza zimehifadhiwa katika Akaunti maalum zilizofunguliwa kwa kushirikiana na Warajisi wa Vyama vya Ushirika, Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na TAKUKURU kwa ajili ya kurejesha kwa wanaostahili kurejeshewa fedha hizo.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Naomba kurudia.
Watu wote waliojihusisha katika kufanya ubadhirifu, rushwa au wizi wa fedha za ushirika, wahakikishe wanazirejesha haraka sana kuanzia sasa taarifa hii inapotolewa.
Tunapenda wananchi wafahamu kwamba, TAKUKURU ipo imara kuwafuatilia wale wote waliojihusisha na ubadhirifu huu ili warejeshe fedha walizochukua.
Hatua kali dhidi ya wote ambao watakaidi agizo la kurejesha fedha walizochukua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali za watuhumiwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka.
Ndugu Waandishi wa Habari,
TAKUKURU inaendelea kuwasihi wananchi popote pale walipo, waendelee kutupatia taarifa za wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa ili tuhakikishe kwamba hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wale wote wasiolitakia mema Taifa letu.
TAKUKURU imeendelea kuboresha miundombinu ya kuwawezesha wananchi kuwasiliana nasi na kutupatia taarifa ambapo pamoja na kuwa namba za simu ya Dharura 113 ambayo ni BURE – TAKUKURU imeanzisha TAKUKURU APPLICATION ambayo inamwezesha mwananchi kuwasilisha taarifa za wanaojihusisha na rushwa kupitia Simu ya kiganjani.
Kupitia TAKUKURU APPLICATION, Mwananchi anaweza kutuma Picha mnato za matukio; Anaweza kutuma sauti na pia anaweza kutuma ujumbe mfupi wa maneno.
Taarifa hizo zitakazotumwa zitapokelewa moja kwa moja TAKUKURU katika ofisi maalumu ambayo maafisa wake wanafanya kazi saa 24.
Mbali na kutumia njia hizo, Mwananchi anaweza kufika katika ofisi zetu zilizoko katika kila mkoa, kila Wilaya na hata katika Vituo Maalum ambavyo vina mkusanyiko wa shughuli nyingi za kuichumi.
Ndugu Watanzania wenzangu,
RUSHWA NI ADUI ANAYEWEZA KUTUCHELEWESHEA MAENDELEO AMBAYO RAIS WETU – MHE. DKT JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI – RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AMEKUWA AKIYAPIGANIA USIKU NA MCHANA.
HAYA SHIME, KILA MMOJA WETU AJIVISHE JUKUMU HILI LA KUWAFICHUA WALA RUSHWA NA MAFISADI ILI KWA PAMOJA TUWATOKOMEZE. TULETEENI TAARIFA NASI TUTAZIFANYIA KAZI KWA WAKATI NA KUWAPA MREJESHO.
AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.
IMETOLEWA NA:
BRIG. JEN. JOHN J. MBUNGO
KAIMU MKURUGENZI MKUU
TAKUKURU