Ukame kupandisha tena bei za vyakula nchini

Ukame kupandisha tena bei za vyakula nchini

BARD AI

JF-Expert Member
Joined
Jul 24, 2018
Posts
3,591
Reaction score
8,826
Wakati mfumuko wa bei ya bidhaa za chakula ukiripotiwa sehemu mbalimbali nchini, hofu ya bei hizo kuendelea kupanda imeibuka baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutangaza uwezekano wa kuwepo upungufu wa mvua za vuli katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua.

Hofu ya bei ya vyakula, hasa nafaka jamii ya kunde kuendelea kupanda inachagizwa na taarifa ya TMA iliyotolewa juzi Ijumaa Septemba 2, 2022 na Mkurugenzi Mkuu, Dk. Agnes Kijazi inayoonyesha upungufu wa mvua za vuli kati ya Oktoba hadi Desemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, upungufu huo wa mvua utapunguza unyevunyevu katika udongo, hivyo kusabababisha athari mbalimbali, ikiwemo vipindi virefu vya ukame.

Alisema upo uwezekano kutokea kwa mvua kubwa katika baadhi ya maeneo, upungufu wa chakula, malisho na maji kwa ajili ya mifugo na milipuko ya magonjwa kutokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.

Licha ya Dk. Kijazi kushauri wananchi kuhifadhi na kutumia vema akiba ya chakula, uchunguzi wa gazeti hili katika baadhi ya mikoa nchini umebaini bei ya bidhaa sokoni hasa mchele, mahindi na viazi mviringo imeanza kupanda ndani ya kipindi cha miezi miwili.

Mfano, bei ya kipimo cha mchele ndoo yenye ujazo wa kilo 20 katika Soko la Sido Jijini Mbeya imepanda kutoka sh. 35,000 hadi sh. 48,000, huku mahindi yakipanda kutoka Sh10,000 hadi sh. 15,000 kwa kipimo hicho hicho na viazi mviringo vilivyokuwa vikiuzwa kwa sh. 7,000 sasa vinauzwa sh. 12,000.

Mfumuko wa bei pia umeshuhudiwa mkoani Iringa katika kipindi hiki cha mavuno ambacho bei zilitarajiwa kushuka na gunia la mahindi lenye ujazo wa kilo 100 lililokuwa linauzwa kwa sh. 88,000 limepanda hadi sh. 89,000, gunia la mchele limepanda hadi sh. 210,000 kutoka bei iliyotarajiwa ya sh. 209,000, huku viazi mviringo bei ikipanda kwa sh. 200 kutoka bei tarajiwa ya sh. 82,000 hadi sh. 82,200.

Ushauri wa TMA
Akitoa taarifa kuhusu mwelekeo wa mvua za vuli kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2022, Dk. Kijazi alishauri matumizi mazuri ya chakula na kwa uangalifu kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa, huku wafugaji na wakulima wakishauriwa kuwa na mpango mzuri wa matumizi ya malisho kuzuia migogoro kati yao.

“Wananchi ambao maeneo yao yatakuwa makavu wanashauriwa kuacha kuotesha mazao mpaka pale mvua zitakapoanza. “Upungufu wa unyevunyevu kwenye udongo utasababisha kujitokeza kwa visumbufu vingi, ikiwemo mchwa, viwavi jeshi, panya na nzige. Ni vizuri kupanda mazao kwa wakati na yanayostahimili ukame, ikiwemo viazi, mihogo, mtama, viazi vitamu, mtama na jamii ya mikunde,” alisema.

Pamoja na kupanda mazao yanayostahimili ukame, Dk. Kijazi pia alishauri matumizi ya mbinu na teknolojia ya kilimo inayohifadhi unyevunyevu kwenye udongo.

NFRA yaondoa hofu
Kutokana na hali hiyo, mwananchi lilizungumza kwa simu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Milton Lupa aliyewaondoa hofu watanzania kuhusu uwezekano wa kutokea njaa, akisema taifa lina akiba ya kutosha ya chakula.

“Tuna chakula cha kutosha. Kiwango tulichohifadhi ni kikubwa na hakifikiwa kwa miaka mitano iliyopita. Siwezi kutaja ni tani ngapi kwa sababu takwimu hizo zinapatikana Wizara ya Kilimo, lakini tuna akiba ya kutosheleza kwa miezi mitatu ikiwa hakuna chakula kingine na Watanzania wote watakula ugali pekee,” alisema Lupa. Juhudi za kumpata Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe na Naibu wake, Anthony Mavunde kufahamu kiwango cha chakula kilichopo NFRA hazikufanikiwa jana, baada ya simu zao za kiganjani kuita bila kupokelewa.

NFRA ina maghala ya kuhifadhi chakula katika kanda nane nchini, ikiwemo katika mikoa inayoongoza kwa uzalishaji ya Mbeya, Rukwa, Njombe, Ruvuma na Songwe. Maghala mengine yako Shinyanga, Dodoma na Dar Es Salaam.

Kwa mujibu wa Lupa, kazi inayofanyika sasa baada ya kununua chakula kutoka mikoa na maeneo yenye kiwango kikubwa cha uzalishaji ni kukihamishia chakula hicho kwenye mikoa na maeneo yenye uzalishaji mdogo, lengo likiwa ni utayari kwa dharura yoyote.

Walichokisema wasomi
Baadhi ya wasomi katika fani ya uchumi na uhandisi walisisitiza matumizi ya teknolojia na kilimo cha umwagiliaji kuwezesha taifa si tu kuzalisha chakula cha kutosha, bali pia ziada ya kuuza nje.

“Tanzania inapata mvua za kutosha hata pale panapokuwepo mvua chache, tujikite katika teknolojia ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji badala ya kilimo cha kutegemea misimu ya mvua,” alisema Amani Golugwa, mchumi na mtaalamu wa hesabu mkazi wa Arusha.

Akitaja mataifa ya Misri, Libya na Syria yanayojitosheleza kwa chakula kupitia umwagiliaji, licha ya kuwa kwenye ukanda wa jangwa, Golugwa alisema tangazo la uwezekano wa ukame na njaa linaweza kutumiwa na baadhi ya wakulima wakubwa na wafanyabiashara wa nafaka kuficha bidhaa hiyo, ili kusababisha mahitaji na hatimaye bei kubwa sokoni.

Hoja ya kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji pia ilitolewa na Mhadhiri Mstaafu wa vyuo vikuu vya Dar Es Salaam (UDSM), Ardhi na Saut, Dk. Kamugisha Byabato aliyeishauri serikali na wadau wengine wa sekta ya kilimo kuwekeza rasilimali fedha, ujuzi na nguvu kwenye kuvuna, kuhifadhi na kusambaza maji shambani.

“Tuna ardhi kubwa na yenye rutuba inayofaa kwa kilimo, tuwekeze kwenye kuvuna maji ya mvua na tutumie teknolojia ya kuyatunza, kuyasafirisha na kuyasambaza shambani kuondokana na tishio la njaa,” alisema.
 
Back
Top Bottom