ADOLPH EMMANUEL
Member
- Sep 22, 2020
- 7
- 1
Andiko hili linaelezea suala la ukombozi wa kifikra kwa Watanzania na Waafrika kwa ujumla kama nyenzo ya kujikomboa kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.
Jamii ya watu wasiojiamini, wenye akili iliyofungwa, wenye kuwategemea watu wengine wawaletee maendeleo, wasioweza kufikria hatima yao na vizazi vyao, wanaowaabudu binadamu wenzao na kuwaona kama miungu, kamwe: Hawawezi kuendelea na watabakia masikini na tegemezi siku zote.
Fikra ni mawazo au mafikilio ya mtu juu ya kitu fulani. Haya mawazo ndio hutengeneza msimamo wa kiutendaji ndani ya mtu. Uwezo wa kufikria hutofautiana kutoka kwa mtu mmoja na mwingine. Baadhi ya watu wana uwezo mkubwa wa kufikria (huwaza mambo makubwa) na wengine wana uwezo mdogo wa kufikria (huwaza mambo madogo).
Kuto-komboka kifikra kwa Waafrika wengi kumezifanya nchi nyingi za Afrika zibakie masikini japo zimeishapata uhuru. Inawezekana Waafrika wana uwezo mzuri wa kufikria lakini je! Wanakiweka katika matendo kitu wanachokiwaza au kukifikria? Je! Wana uhuru wa kukifanya hicho wanachokifikria?
Ukweli ni kwamba, Waafrika wengi hawajakomboka kifikra. Hili linadhibitishwa kwa kutazama jinsi ambavyo Afrika inaishi kwenye kivuli cha wazungu (nchi za ughaibuni). Wao ndio huamua ni kitu gani kifanyike au kisifanyike barani Afrika. Jambo lisiloweza kupingika ni kwamba, Waafrika wengi hawako tayari kuukubali ukweli huu, wao hujiona wamekomboka kifikra na huona wako huru...
Baadhi ya Waafrika wanaoukubali ukweli huu ni wale waliokata tamaa, ambao huamini wazungu wamebarikiwa, na nchi za Kiafrika haziwezi kuendelea kama zilivyo nchi nyingi za wazungu pamoja na watu wenye rangi (coloured people). Wengine kwa kutumia imani za dini zao, husema kwamba, "Afrika ni uzao wa Ham, ambao ulilaaniwa". Wakiwa na maana kwamba, ngozi nyeusi imelaaniwa.
Chimbuko la nadharia zote ambazo zinamfanya Mwafrika ajione dhaifu mbele ya watu wengine hasa watu weupe (Wazungu na watu wenye rangi) ni ukoloni. Madhara makubwa ya ukoloni ambayo yanazidi kulizoofisha bara la Afrika ni kuiaribu saikolojia ya Mwafrika, kumfanya Mwafrika ajione dhaifu na mnyonge mbele ya mzungu. Kwavile kipindi kile cha ukoloni, Mwafrika alitakiwa kunyenyekea mbele ya mzungu au mtu mwenye rangi na nadharia hiyo imeendelea mpaka leo.
Kudhibitisha hili, jiulize kwanini ukienda kwenye ofisi yoyote hapa nchini Tanzania, wakati ukisubiri kuhudumiwa, akija mzungu anaudumiwa wa kwanza? Kuna mtu atasema Watanzania ni wakarimu, hivyo huo ni ukarimu kwa wageni. Je! Watanzania wanaoneshwa ukarimu wakiwa ughaibuni? Mbona watu weusi kutoka mataifa jirani hawaoneshwi huo ukarimu? Kwanini baadhi ya sheria kwenye baadhi ya maeneo, zinawabana Waafrika tu na sio Wazungu? Kuna baadhi ya hoteli na taasis za kielimu hapa nchini, mwanaume hawezi kuingia akiwa amevaa bukta lakini mzungu anaingia nayo. Kwanini sheria zisiwabane wote? Mwafrika akiingia kwenye baadhi ya taasis za utarii hasa hoteli na vivutio vya utarii, huwa hachangamkiwi kama anavyochangamkiwa mzungu labda huyo mtu mweusi awe maarufu. Watu husema eti, "Hii ni kwasababu Waafrika huwa hawatoi tips (to improve proper services) na "keep change" kwa wahudumu.
Jambo jingine la kujiuliza, viongozi wa Kiafrika wana nguvu ya kufanya maamuzi? Kama jibu ni ndiyo, mara ngapi wamekuwa wakikosolewa na mataifa yaliyoendelea na kutishiwa kuondolewa madarakani? Watu watasema kukosolewa ni kawaida, je! nchi za Kiafrika zina uwezo au mamlaka ya kuyakosoa mataifa yaliyoendelea na yenyewe yakazisikiliza?
Mataifa yaliyoendelea yanapozikosoa nchi za Kiafrika, huwa yanawaaminisha Waafrika kuwa viongozi hao wana makosa na hawafai na Waafrika huamini. Unaweza kupinga hili jambo, chukulia mfano wa aliyekuwa rais wa Libya, Mh. Muammar Muhammad Abu Minyar al-Gaddafi, mataifa yaliyoendelea yaliwaaminisha Waafrika kuwa ni mtu mbaya na wengi wakaamini, mwishowe akaondolewa madarakani lakini mpaka sasa imepita miaka kumi Libya haijapata amani.
Inasikitisha sana kumuona mtu anasema eti, "Bora ningezaliwa mbwa Marekani kuliko kuzaliwa mwanadamu hapa bongo". Mtu akiisema hii kauli, huwa naumia kwani huwa inanidhihirishia kuwa baadhi ya Waafrika ni watumwa wa akili. Hii kauli haisemwi tu na watu ambao hawajaenda shule bali na wenye elimu ya juu. Wanao itumia hii kauli hawatambui thamani yao kama binadamu ndio maana hujilinganisha na mbwa. Hii ni sawa na kusema, huwezi kujiongoza na kujiendesha kimaisha mpaka uongozwe na kuendeshwa na mtu mwingine. Kauli kama hii inaposemwa na mtu mzima mbele ya watoto, huwafanya hata wao waamini kuwa mtu mweusi hana thamani.
Wazungu ndio waliosema na wanaoendelea kusema kwamba, "Afrika haikuwa na utamaduni wala historia". Wanadai kwamba, wakati wanafika barani Afrika, watu hawakuwa na utamaduni, lugha, uongozi, elimu wala hawakuwa wamestaarabika. Wanadai kuwa, historia ya Afrika imeanza mara tu ya wao kufika barani Afrika na kwamba wao ndio walioleta ustaarabu barani Afrika.
Umasikini uliopo barani Afrika ni kwasababu ya utumwa wa akili uliopo miongoni mwa Waafrika. Kwahiyo, kama tunataka kujikomboa kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa, lazima tujikomboe kifikra kwanza. Lazima tufikrie hatima ya taifa letu kwa miaka ijayo, lazima kila mmoja kwa nafasi yake, ajione ana jukumu la kulikomboa taifa na si kuwaachia viongozi. Taadhari; Kama tusipoamua na kujiwekea malengo juu ya hatima ya taifa (bara) letu basi kizazi kijacho kitazidi kuumia mbele ya mataifa yaliyoendelea.
Kila mmoja ajiulize swali, ni urithi gani anaenda kuiachia nchi ya Tanzania? Amelifanyia nini taifa? Tunawakumbuka waasis wa taifa (bara) letu kwasababu walifanya makubwa kuhakikisha wanaleta uhuru. Basi na sisi tuandae urithi wa kuwaachia watoto wetu na wajukuu zetu.
Kama tunataka kujikomboa juu ya nadharia mbaya juu ya mtu mweusi ni lazima tuanze sasa na si kusubiri wakati ujao ambao hatuna uhakika nao. Yafuatayo yanaweza kufanyika ili tuweze kujikomboa na kuleta maendeleo kwenye taifa letu.
Iundwe tume au timu ya kuendesha mchakato huu. Watu wanaounda timu hii, lazima wawe na uelewa mzuri juu ya umuhimu wa kujikomboa kifikra. Lazima wote wawe na imani moja au imani chanya juu ya faida za elimu hii. Ni vyema timu hii, ikaundwa na watu wa rika na jinsia zote bila kubagua. Timu hii ndiyo itakuwa na jukumu la kuielimisha jamii, kuandaa mwongozo wa kutolea elimu hii pamoja na kuangalia namna bora kabisa ya kufanikisha mchakato huu. Sheria huanzia nyumbani, hivyo lazima timu nzima iwe na uelewa mzuri katika suala la ukombozi wa kifikra.
Kuwafundisha na kuwaaminisha watoto juu ya thamani ya mtu mweusi. Ukweli ni kwamba, nadharia potofu iliyojengeka miongoni mwa Waafrika wengi kuwa Mwafrika si lolote na si chochote mbele ya watu weupe ni ngumu sana kuibadilisha kwenye akili ya watu wazima. Ni vigumu kukibadilisha kizazi cha sasa hivyo ni vyema kukiangalia kizazi kijacho. Kwahiyo, tuandae mazingira mazuri kwaajili ya kuwafundisha watoto juu ya thamani ya Mwafrika. Mtoto akue akiamini kuwa binadamu wote ni sawa na wote wanaweza kufanya mambo makubwa. Hii itamsaidia mtoto kuwa na uhuru wa kufikiria kufanya mambo makubwa kwa maslahi ya taifa bila ya kuwa na hofu kwamba Waafrika hawawezi. Mtoto atengenezewe mazingira ya kujiamini mbele ya watu wa rangi zote. Tulifanye hili sio kwa manufaa ya kizazi kilichopo bali kijacho. Wengi watasema ni vigumu kufanya ili jambo lakini tukumbuke, Roma haikujengwa kwa siku moja, pia Wazngu hawakutumia siku moja kuibadilisha imani ya Mwafrika, iliwachukua muda. Hili lifanyike kwa moyo mmoja kwa manufaa ya kizazi kijacho.
Kuwashirikisha na kuwaelimisha walimu katika mchakato huu. Miongoni mwa watu wanaokaa karibu na watoto ni walimu, hivyo ni vyema kuwaelimisha kuhusu mchakato wa kuibadilia nadharia potofu juu ya mtu mweusi. Walimu wapatiwe mwongozo watakao hutumia kuwafundishia wanafunzi juu ya ukombozi wa kifikra. Isiwe kwa walimu wa shule za msingi tu, bali ngazi zote za elimu nchini. Isije kusaulika kwamba, hata walimu nao waelimishwe kwanza juu ya mchakato huu kwani ukombozi wa kifikra unahitajika kwa watu wote.
Kuwashirikisha na kuwaelimisha wazazi juu ya mchakato huu. Inawezekana likaonekana jambo gumu sana kuwaelimisha wazazi juu ya ukombozi wa kifikra, lakini lazima waelimishwe hata kama hawatoelewa wote wachache wataelewa. Ikumbukwe kwamba, wazazi ndio huanza kuwaaminisha watoto kwamba, "Mzungu ni Mungu mtu". Huongezea kwamba, “Mzungu alitengeneza yote hila alishindwa moyo tu”. Kauli kama hizi huwafanya watoto wakue wakiamini kuwa mzungu ni bora kuliko Mwafrika na anatakiwa kuabudiwa kwani kila kitu kipo chini ya matakwa yake. Hivyo basi, huwa ni rahisi sana watoto kuamini, kukua na kuishi katika ulimwengu wanaotengenezewa na wazazi wao pamoja na watu wanao wazunguka.
Kuvishirikisha vyombo vya habari. Huu ni ulimwengu wa tehama ambao vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuielimisha na kuibadirisha jamii. Ili kuweza kuufanikisha mchakato huu, ni vyema vyombo vya habari viusishwe. Waandishi na watangazaji waelimishwe ili waweze kutoa taarifa sahihi juu ya elimu hii kwa umma. Vilevile, wataalam watakaokuwa wameandaliwa kwaajili ya kuendesha mchakato huu, wapewe nafasi kwenye vyombo vya habari ili kufundisha na kuuelimisha umma juu ya ukombozi wa kifikra.
Yaandaliwe makongamano mbalimbali yenye lengo la kutoa elimu hii. Kwavile mchakato huu lazima uendeshwe na timu fulani inayokuwa imetengenezwa, hivyo makongamano mbalimbali yanaweza kuandaliwa ambayo yataendeshwa na timu hii. Makongamano hayo, yawausishe watu wote, muda mwingine yanaweza kuandaliwa yakilenga kikundi fulani cha watu.
Kwahiyo, umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu, hivyo hatuna budi Watanzania (Waafrika) wote kushirikiana ili kufanikisha mchakato huu. Kwa mtu aliyeridhika na hali hii ya Mwafrika kuishi kama tegemezi kwa mzungu, hawezi kuunga mkono mchakato huu. Kwa yule ambaye anaona kila kizazi kife kivyake, pia hawezi kukubaliana na mchakato huu. Yule ambaye anaona yote sawa, pia hawezi kusaidia maendeleo ya mchakato huu. Inawezekana tumeishachelewa, kwamba mchakato ulitakiwa uanze mapema lakini hatujachelewa kwani bora kuchelewa kuliko kukosa kabisa. Ukiingalia Tanzania (Afrika) bila elimu hii unaiona wapi ndani ya malengo ya millennia? Je! Kwa elimu hii ndani ya malengo ya millennia? Angalizo, mchakato huu unahitaji gharama, muda na uvumilivu kwani wengi wataupiga vita usifanikiwe.
Andiko hili limeandaliwa na…
Adolph Emmanuel
Upvote
1