Ukosefu wa vyoo shuleni unavyoathiri afya, taaluma

Ukosefu wa vyoo shuleni unavyoathiri afya, taaluma

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
choo.jpg

Mwalimu akionyesha mfano wa choo unavyoonekana katika moja ya shule za msingi nchini

KWA UFUPI
Wanafunzi hao ni kati ya wengine maelfu nchini ambao kila siku wanalazimika kupanga foleni, kwa ajili ya kupata huduma hiyo katika vyoo ambavyo siyo tu havina matundu yanayokidhi haja ya idadi ya wanafunzi, pia havina huduma kama vile maji na mifumo ya majitaka.


WAKATI wa mapumziko katika shule mojawapo ya msingi Jijini Dar es Salaam, wanafunzi wamepanga foleni wakiingia kwa zamu katika choo chenye tundu moja pekee linalotumiwa na wanafunzi zaidi ya 200 wa shule hiyo.

Wanafunzi hao ni kati ya wengine maelfu nchini ambao kila siku wanalazimika kupanga foleni, kwa ajili ya kupata huduma hiyo katika vyoo ambavyo siyo tu havina matundu yanayokidhi haja ya idadi ya wanafunzi, pia havina huduma kama vile maji na mifumo ya majitaka.

Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), katika shule za wilaya 16 nchini, zaidi ya wanafunzi 200 wamebainika kutumia shimo moja, zaidi ya asilimia 80 ya wanafunzi hao hawakuwa na sehemu ya kunawa mikono baada ya kujisaidia.

Aidha, utafiti huo unabainisha kuwa asilimia 96 ya vyoo vya wavulana havikuwa na milango na asilimia 96 ya shule hazikuwa na vyoo kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu, hali ambayo imekuwa na athari za kitaaluma na kiafya kwa wanafunzi.

"Hali ni mbaya zaidi katika maeneo yenye msongamano wa watu kama vile Dar es Salaam, hasa Temeke" inasema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza kuwa wilaya hiyo inahitaji hatua za makusudi ili kukabili hali hiyo ambayo ina athari kubwa za kitaaluma na kiafya kwa watoto.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mpango wa Maji, Usafi wa Mazingira na Mazingira Mazuri ya Afya (WASH), ni asilimia 11 tu ya shule zilizofanyiwa utafiti zimekidhi viwango vya Sera ya Elimu ya mwaka 2005 ambayo inataka kila shimo la choo kutumiwa na wanafunzi wa kike 20 na wa kiume 25.

Ukosefu wa vifaa vya kunawia na sabuni ni changamoto nyingine inayozikabili shule za msingi nchini, na utafiti zaidi unaonyesha kuwa ni asilimia moja pekee ya shule hizo ndizo ambazo zina sabuni kwa ajili ya kunawia mikono na asilimia nane hazina kabisa vifaa hivyo.

Hali ni mbaya zaidi kwa wanafunzi wenye ulemavu, kwani ni shule asilimia nne pekee ndizo ambazo zina sehemu za kunawia mikono kwa watoto wa namna hiyo, hali hiyo inatajwa kuchangia matatizo ya kiafya kwa wanafunzi na vifo vinavyotokana na maradhi kama vile homa ya matumbo, kuhara na kipindupindu.

Sambamba na hilo, utafiti unabainisha kuwa mazingira ya namna hiyo yanasababisha pia baadhi ya wanafunzi ‘kukacha' masomo, tatizo ambalo takwimu za kiulimwengu zinabainisha kuwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwemo Tanzania zina idadi kubwa ya wanafunzi wanaoacha shule kuliko maeneo mengine.

Tafiti zaidi zinabainisha kuwa tatizo la ukosefu wa vyoo na maji ya uhakika shuleni limekuwa na athari mbaya zaidi kwa watoto wa kike kuliko wa kiume na inaelezwa kuwa asilimia 10 ya wasichana wamekuwa wakikatisha masomo wanapokuwa katika siku zao za hedhi.

Wanafanya hivyo kutokana na mazingira wanayokutana nayo shuleni ambayo si rafiki kutokana na hali wanazokua nazo wakati huo, na hali hiyo inaelezwa kuwa huwafanya wafadhaike, hivyo wengine kuamua kubaki nyumbani na kushindwa kurudi shule hata baada ya kumalizika kwa kipindi hicho.

Katika kile kinachoonekana kukabiliana na hali hiyo, hivi karibuni Unicef, liliingia mkataba wenye thamani ya Sh150 milioni na benki ya Stanbic kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Mpango wa Maji, Usafi wa Mazingira na Afya (WASH) kwa shule za msingi Wilaya ya Temeke.



Mwakilishi wa Unicef nchini, Dk Jama Gulaid anasema mradi umedhamiria kuwakomboa watoto nchini kwa kupambana na matatizo ya uhaba wa majisafi na mazingira katika shule mbalimbali za msingi nchini na mradi huo ni wa kwanza wa ubia tangu shirika hilo lifungue ofisi zake nchini miaka ya 1960.

"Wilaya ya Temeke ni moja ya wilaya nchini zinazohitaji sehemu za usafi, kwa sababu ni moja ya maeneo yaliyopo mjini yenye idadi kubwa ya wanafunzi au kuwa na shule nyingi zilizopo jirani katika eneo moja," anasema na kuongeza kuwa benki hiyo na Unicef watajihusisha na mradi huo kwa miaka mitatu.

Anasema magonjwa yanayoweza kuzuilika kama vile kipindupindu, kuhara na ugonjwa wa matumbo, yameenea sana nchini Tanzania na kwa muda mrefu yamekuwa ni chanzo kikubwa cha vifo kwa wananchi hasa wanawake, watoto wanaosoma shule na wale wenye umri chini ya miaka mitano.

"Magonjwa haya yamekuwa yakihusishwa na ukosefu wa maji na mazingira machafu. Takwimu zinaonyesha kwamba watu milioni 1.7 nchini Tanzania huugua ugonjwa wa kuhara, ambao unawaathiri sana watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambao 200 hupoteza maisha kabla ya kufikisha miaka mitano kati ya 1,000 wanaozaliwa," anasema.

Mmoja wa walimu katika Shule ya Msingi Wailes ya wilayani Temeke, anabainisha kuwa hali siyo nzuri katika shule nyingi kutokana na ukosefu wa maji na uhaba wa mashimo ya choo, huku michango ya wazazi na harambee nyingine zikishindwa kubadili mambo kutokana na urasimu na shule nyingi kutumia kiasi cha fedha katika masuala ya utawala badala ya mradi husika.

Kutokana na hali hiyo ni wazi kuwa jitihada zaidi zinahitajika kukabili hali hiyo na kupanua zaidi wigo wa utekelezaji wa mradi huo kutoka shule za Temeke hadi katika shule nyingine za wilaya zote 16 zilizofanyiwa utafiti. Ukosefu wa vyoo shuleni unavyoathiri afya, taaluma - Makala - mwananchi.co.tz
 
Back
Top Bottom