SoC02 Ukusanywaji wa tozo na mchango wake kwenye Uchumi wa Taifa

SoC02 Ukusanywaji wa tozo na mchango wake kwenye Uchumi wa Taifa

Stories of Change - 2022 Competition

Lameck Ezekiel

New Member
Joined
Sep 14, 2022
Posts
4
Reaction score
3
Uhai wa serikali yoyote unategemea mapato inayoyakusanya ili kuendesha mipango yake katika nchi. Na nguzo kuu ya mapato hayo huwa ni wananchi waliyoipatia dhamana serikali hiyo hasa kwa njia ya kodi. Lakini nakumbuka kanuni za ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kodi zilizotolewa na mwanafalisafa mmoja Adam smith, ambaye pamoja na mambo mengine alisema kuwa, kodi inayokusanywa kwa wananchi lazima izingatie usawa, uhalali na isiwe ile inayotengeza usumbufu kwa mlipa kodi.

Kumeshuhudiwa kutokuzingatiwa kwa baadhi ya kanuni hizi nchini mwetu hasa kwenye kipindi cha uanzishwaji wa kodi mpya zilizobatizwa kwa jina la tozo. Na hili limedhihirishwa na kelele zilizokithiri za wananchi kupinga kodi hizi tofauti na kodi zingine zilizokuwepo awali.

Ebu tujiulize kwamba, je ni kweli serikali imekosa njia mbadala za kujipatia mapato tofauti na njia hii ya tozo inayopigiwa kelele kila kona? Na je, ni kweli ukusanyaji wa tozo unaleta matunda tarajiwa ya serikali bila kusababisha athari zingine kwenye mfumo wa uchumi?

Binafsi ninaona uwepo wa tozo umeongeza ugumu wa maisha ukilinganisha kwamba zinakusanywa kipindi cha mfumuko wa bei za bidhaa unaotokana na vita vya Urusi na Ukraine. Na mbaya zaidi zinakusanywa hasa kutoka kwa watu wa tabaka la chini, tena kwa wingi mno (kwa maana kwamba kuna utitiri wa tozo) kila kukicha.

Pia, tozo hizi zinaathathiri mfumo wa uchumi kwa kiasi kikubwa sana. Kwa mfano, mtu anaweza akajiuliza kwamba,kama tozo za miamala ya simu zimepelekea kupungua kwa watu wanaotumia huduma hiyo kwa zaidi ya asilimia 20, kiasi ambacho kimepelekea makampuni ya simu kupata hasara, je serikali haioni kwamba tozo za miamala ya kibenki pia zitapunguza utumiaji wa huduma za kibenki kwa wananchi?

Jambo hili kwa upande wa pili linaelekea kuwa ugonjwa mkubwa kwenye uchumi wa taifa kwa sababu mzunguko wa kifedha kwenye mabenki ndio unaonesha dira ya uchumi wa tiafa. Hili pia litapunguza uwezo wa serikali kufanya tathimini na kufanya mipango yake ya kiuchumi. Matokeo ya haya ni kwamba, wananchi wanaenda kurudi kwenye utamaduni wa zamani wa kutunza fedha zao majumabani, na ndipo tutaanza tena kushuhudia matukio ya uvamizi na mauaji ambayo taifa lilikuwa limeyapunguza kwa kiasi fulani.

Aidha tozo hususani zile za miamala ya simu zimedhoofisha uwekezaji wa wananchi wa uchumi wa chini na hivyo kupelekea kuongozeka kwa kasi ya umasikini. Hii ina maana kuwa akiba ya mtu wa chini anayowekeza ili baadae imuinue, inapunguzwa na makato kitu amabacho baadae kinafanya mavuno ya uwekezaji wake kupungua na hivyo kufanya mzunguko wa pesa uwe mgumu.


NI UPI UNAWEZA UKAWA MBADALA WA HAYA?

Kelele za wananchi juu ya tozo kimsingi hazikutakiwa kutolewa kwenye taifa lililojariwa utajiri na neema ya kila namna kama Tanzania. Cha kufanya ni serikali yetu iongeze usismamizi wa utajiri ambao mwenyezi Mungu katujaria.

Hili linadhihirishwa na kauli ya rais wa Rwanda Paul Kagame aliyoitoa akisema kwamba,yeye angeweza kuendesha nchi yake kupitia mapato yanayopatikana kwenye bandari ya Dar es salaam peke yake. Mfano,nchi yetu ni moja ya nchi zenye vivuko na bandari nyingi barani afrika ambazo zikisimamiwa vizuri tunaweza tukapata ushuru wa kutosha kuiendesha nchi yetu.

Shida hapa kwetu ni usimamizi hafifu, kitu kinachowafanya viongozi wenye dhamana kuona tozo kama ndio njia rahisi ya kukusanya mapato.

Pia,kunatakiwa kuwe na usismamizi mzuri wa fedha za serikali. Mapato ambayo yalikuwa yanakusanywa na serikali kabla ya tozo yangetosha sana kama tu serikali ikiongeza usimamizi wa hayo mapato. Hii itawezekana kama maadili ya watumishi wa umma yataendelea kuimarishwa. Kwa mfanao, ni ajabu mpaka sasa taifa kuwa na ubadhirifu wa fedha kama ule uliogunduliwa na waziri mkuu Kassim Majariwa kule Uyui mkoani Tabora kwenye shughuli za ujenzi wa chuo cha VETA ambapo nyumba tu ya mlinzi ilionekana kutumia zaidi ya milioni kumi.

Aidha serikali iongeze uaminifu na uwazi kwa wananchi. kimsingi kelele za tozo zinasababishwa na mkanganyiko na sintofahamu ambayo serikali inatengeneza kwa wananchi. Kwa mfano, watu wanachanganywa wanaposikia kwamba fedha za kupambana na korona zimetumika kujenga shule na miundombinu mingine, wakati huohuo fedha za tozo zikisemwa kutumika kwa matumizi yaleyale.

Lakini pia tumeshuhudia viongozi wakubwa na wenye dhamana wakisimama hadharani na kusema juu ya wananchi kukubaliana na tozo jambo ambalo sio kweli kabisa na uhalisia. Hili lilionekana kwa mfano kwa mweshimiwa raisi Samia Suluhu Hassan akihojiwa na BBC, na pia kwa waziri Mwigulu Nchemba akihojiwa ITV. Kitu hiki mbali na mambo mengine kinawafanaya wananchi kukosa imani na serikali yao.

Kwa kuongezea, serikali iweke vipaumbele chanya kwa manufaa ya wananchi, kwa kuzingatia vipaumbele amabavyo wananchi watanufaika navyo moja kwa moja. Tumeshuhudia serikali ikiwa na bajeti ya ununuzi kwa mfano wa magari ya serikali pamoja na mpango wa royal tour ambavyo japo vinaweza kuwa na manufaa kwa wananchi lakini ni kwa mgongo wa nyuma.

Kwa kuhitimisha, suala la kuanzishwa kwa ukusanywaji wa tozo halileti ile picha na uhalisia unaodaiwa na serikali, badala yake limegeuka kuwa mzigo kwa wananchi hasa wale wa tabaka la chini. Swali ni je, Kama serikali ya awamu ya tano ambayo ilikuwa imesheheni watendakazi wale wale wa awamu hii ya sita na iliweza kutufikisha kwenye uchumi wa kati bila kutumia njia hii ya tozo, kwa nini sasa isiwezekane? Pia,tozo zimefikia hatua sasa zinaleta picha mbaya kwa serikali Kiasi kwamba inawafanya wananchi waamini serikali yao imejaa wale wanaoitwa na vijana wa leo kama ‘’wapigaji’’.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom