Kifo cha Pepe Kale
Ilikuwa majira ya mchana, tarehe 29 November mwaka 1998 ndipo radio za kimataifa zilitangaza kifo cha Pepe Kale. Mwamba, mwanaume aliyekuwa na kilo zake nyingi tu na urefu kama unaotajwa katika Biblia alifariki kwa ugonjwa wa moyo katika Hospitali ya Ngaliema huko Kinshasa.
Wakati dunia inatangaziwa kwamba Pepe Kale, amefariki kwa ugonjwa wa moyo, huko Congo kulikuwa na habari nyingine kwenye vijiwe vya kahawa na vilabu vya pombe. Wacongo kama walivyo waafrika wengine, walikuwa wanasema ushirikina na ndagu ndio ilikuwa chanzo cha kifo cha Pepe Kale.
Pepe Kale alifariki akiwa na umri wa miaka 46 tu, mwili wake ulionekana wa kizee lakini umri alikuwa bado kabisa. Huko Congo ilikuwa inasemwa kwamba Pepe Kale alikuwa amepewa masharti na mganga wake. Kila alipokuwa anataka kutoa albamu yake mpya alikuwa anajifungia bafuni kwa muda wa siku tatu. Huko bafuni alikuwa anakuwa kama mtu aliyekufa na kuoza, funza na mende wanamjaa kwenye mwili. Baada ya hizo siku 3 alikuwa anaamka tena na kwenda kuachia albamu yake. Na hiyo album ilikuwa moto na kuvuma dunia nzima. Hayo ndio yalikuwa masharti ya mganga. Sasa, wakongo wanaendelea kusema katika vijiwe vya kahawa, kwamba mwaka huo Pepe Kale alikuwa anajiandaa tena kutoa albamu yake. Akawa ameenda bafuni tena, bahati mbaya mfanyakazi wake wa ndani alikuwa hajui masharti hayo. Siku hiyo mfanyakazi akaenda kufanya usafi bafuni. Alipofika akamkuta Pepe Kale akiwa kama mtu aliyeoza, funza zimejaa mwilini, ndipo yule binti alipopiga kelele kuomba msaada. Na hiyo ndiyo ikawa imesababisha kifo cha Pepe Kale.
Afrika watu wengi ambao huwa wanafanikiwa hata kama wanafanya kazi kwa juhudi na maarifa bado mafanikio yao huwa hayaachwi kuambatanishwa na uchawi na ushirikina. Pepe Kale alifikia mafanikio kutokana na kujituma na kuandaa mziki mzuri. Kwa mtu mwenye uzito kama aliokuwa nao Pepe Kale, sio ajabu kwamba kifo huwa kinatokea katika umri mdogo kutokana na mishipa ya moyo kujaa mafuta. Licha ya hayo yanasemwa lakini historia imeandikwa Pepe Kale alipata mshtuko wa moyo tarehe 28 Novemba akiwa nyumbani kwake na kukimbizwa kwenye Hospitali ya Ngaliema huko Kinshasa ambako usiku wa tarehe 29 aliaga dunia.