Ukoo wa Yesu
Wakristo wanasema wananukuu... Qur’an inasema Mariamu aliyemzaa Isa ni binti Imrani (3:35 na 66:12).Ewe wa kizazi cha Harun, aliye kuwa Nabii Mchamngu Mahashumu! Vipi umefanya uliyo yafanya na baba yako hakuwa na tabia mbovu, wala mama yako hakuwa kahaba!
Maelezo ya Aya: ("Ewe dada wa Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu, wala mama yako hakuwa kahaba." Imeandikwa katika Encyclopaedia Britannica kuwa Qur'ani imekosea kosa la kihistoria ilipo mwita Maryamu "Dada wa Harun," ilihali baina ya Maryamu huyu na Harun nduguye Musa ni karne nyingi. Wamesahau hawa kuwa Udugu ulio zungumziwa hapa ni wa kushabihiana. Makusudio ya hapa ni kushabihiana kwa wema na uchaMungu, yaani ewe uliye mshabihi Harun kwa wema na uchamngu, nini kilicho kugeuza hali yako njema ukawa hivyo? Wala baba yako hakuwa mtu muovu wa kutenda mabaya, wala mama yako kufanya uchafu. (Kadhaalika Maryamu ni ukoo wa Harun, na pengine huitwa "Binti wa Imran", na Imran ni baba yake Harun.)
quranitukufu.net
Pia inaongeza kuwa Mariamu alikuwa dada ya Haruni (19:28). Biblia inasema dada ya Haruni ni Miriamu wala siyo Mariamu. (Kutoka 15:20). ... Biblia bado inaeleza kuwa Miriamu dada yake Haruni hajawahi kuzaa maisha yake yote. Mwisho wa kunukuu.
Ni kweli Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndani ya Qur’an Tukufu amewanukuu Wayahudi kumuita Bi. Mariamu kuwa ni dada ya Harun. Pamoja na hivyo, "udada" unaokusudiwa hapo ni wa Kiukoo kwa kuwa Bi. Mariamu na Haruna wote wanatoka katika ukoo wa Lawi. Ushahidi wa hili tunaupata katika Injili ya Luka 1:36 inayoeleza uhusiano wa Mariamu na Elizabeti (mama yake Nabii Yohana Mbatizaji) ambaye ni mmojawapo wa uzao wa Haruni wa ukoo wa Lawi (Luka 1:5).
Kiutumishi wa kazi za Mungu, kwa kuwa Bi. Mariamu na Haruna wote walikuwa ni watumishi wa Mungu hasa kwa vile ukoo wao (Walawi) ndivyo Mungu alivyokwisha mteua maalum kwa kazi hiyo (Kutoka 40:12-16 na Luka 1:38).
Kiucha Mungu: Kwa kuwa Bi. Mariamu alikuwa ni mcha Mungu neema aliyopewa na Mungu (Luka 1:30) kama vile Haruna pia. Na hii inafanana na ile kauli ya Bwana Yesu au Nabii Isa (a.s.) aliyosema:
"Kwa maana yeyote atakayefanya mapenzi ya Baba yangu aliye Mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, umbu langu na mama yangu". (Mathayo 12:50).
Hapa haina maana kwamba eti kwa vile Mkristo ataamua kufanya mapenzi ya Mungu basi ndio atakuwa ndugu ya Yesu wa kuzaliwa. Hapana! Lakini atakuwa ni ndugu yake kiimani (kiucha Mungu) tu.
Kwa mantiki hiyo, maelezo ya Qur’an Tukufu juu ya "udada" wa Mariamu kwa Nabii Haruna bado haujatofautisha Yesu na Isa. Lakini maana yake ni yule yule mmoja, Bikira Mariamu anayetajwa na Qur’an na Biblia kama tulivyoona hapo juu.