Umewahi kujiambia ‘sina cha kuficha hata wakiniibia sina cha kuogopa’?

Umewahi kujiambia ‘sina cha kuficha hata wakiniibia sina cha kuogopa’?

OleWako

Member
Joined
Sep 7, 2021
Posts
25
Reaction score
73
Tujifunze kuhusu Umuhimu wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi Kutoka kwa Historia ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani

mfszaigfo753bild-0003mast-scaled.jpg


Wanaojua historia miongoni mwenu watakuwa wanajua kwamba baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Ujerumani iligawanywa katika maeneo manne ya uvamizi chini ya Allies na USSR, na baadaye kuwa mataifa mawili – Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani.
Lakini hayo yanahusiana vipi na taarifa zako binafsi, unaweza kujiuliza?

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani (GDR) iliweka moja ya mifumo ya upelelezi na ufuatiliaji iliyoingilia maisha ya watu zaidi katika historia, kwa lengo la kudhibiti wanaoitwa wapinzani wa serikali, watetezi wa haki za binadamu, wakosoaji wa serikali, raia waliopanga kukimbia nchi, na wengine wengi. Mamlaka hiyo iliitwa Staatssicherheit (Usalama wa Taifa), kwa kifupi Stasi. Idara hiyo iliunda mfumo wa upelelezi uliopenya kila tabaka la jamii: simu zilirekodiwa, barua zilifunguliwa na kufungwa tena, taarifa za afya na elimu zilifikika, nyumba na ofisi ziliwekewa vipaza sauti, na watu waliolengwa walifuatiliwa na majasusi wa kitaalamu au raia walionunulika na kukubali kushirikiana na mamlaka.

Katika idadi ya watu milioni 16 wa GDR, kulikuwa na majasusi 90,000 wa kitaalamu na hadi 200,000 waliokuwa ‘majasusi raia’ waliovutwa kushiriki – yaani jasusi mmoja kwa kila raia 55. Miongoni mwa waliovutwa walikuwa wake, waume, marafiki wa karibu na hata ndugu wa damu wa waliolengwa.

Kwa njia hiyo, Stasi walikusanya takriban kilomita 111 za mafaili, picha milioni 2, video 2,900, na rekodi za sauti 23,000 kuhusu watu wapatao milioni 5.6. Miongoni mwa mafaili hayo kulikuwa na rekodi za mazungumzo ya karibu kati ya wanandoa, barua kati ya marafiki, na maandiko ya mikutano ya siri au binafsi ya vikundi mbalimbali.

180704-magazin-im-bstu-mulders-dsc00329-2000px.jpg


Na taarifa hizo hazikuhifadhiwa tu kwenye akiba fulani zikioza. Zilitumika kimkakati katika mpango uliokuwa ukijulikana kama ‘Zersetzung’ (yaani, kuvunjavunja au kuvuruga), ambao uliwalenga ‘maadui wa serikali’ kwa njia ya mateso ya kisaikolojia:

Wapenzi wa kulipwa walitumika kujaribu kuvuruga ndoa kwa kujaribu kuwahadaa wenza wa walengwa; sehemu za kazi zilibanwa kutoajiri walengwa; nyumba zao ziliingiliwa kwa siri na fanicha pamoja na mali kubadilishwa mahali au kuharibiwa; na mbinu nyingine nyingi zilizotambuliwa kama udhaifu wa mlengwa kutokana na taarifa binafsi zilizokusanywa juu yake.

Waathirika walipata madhara makubwa ya kisaikolojia kutokana na mateso hayo, ambayo yaliendelea hata baada ya kuanguka kwa GDR — wengine hata walijitoa uhai kwa sababu ya mateso hayo.

Lakini kwa nini nilete historia ya kabla ya intaneti kuzungumzia ulinzi wa taarifa binafsi?

Kwa sababu mfano huu unaonyesha nguvu ya taarifa binafsi katika kudhibiti jamii, na hamu ya tawala za kiimla (iwe ni za kijamaa, kibepari au kifashisti) kukusanya taarifa hizo na kuzitumia dhidi ya raia wao wenyewe.

Na hilo lina umuhimu zaidi leo kuliko wakati wowote wa nyuma katika historia. Majasusi hawahitaji tena kufunga vipaza sauti au kamera ndani ya nyumba zetu – kwa sababu tunazileta sisi wenyewe kupitia simu zetu. Hata hawahitaji mtu wa kukufuatilia kujua uko wapi, iwapo una laini ya simu iliyo hai na imesajiliwa kwa jina lako. Kusikiliza simu zako, kusoma ujumbe wako mfupi, kufikia picha na video zako – yote yanawezekana.

Tunataniana tukisema simu zetu zinatujua kuliko tunavyojijua wenyewe – inachekesha, sivyo?

Katika kiwango cha teknolojia cha leo, taasisi yenye nia ya kudhibiti taifa kupitia ufuatiliaji haitahitaji tena majasusi 300,000. Tunaiona AI (Akili Unde) kama kifaa kidogo cha kutusaidia kuandika barua pepe, ripoti au kazi za shule. Lakini tusijidanganye. Sababu kuu ya msukumo wa maendeleo ya AI ni fursa kubwa katika uchakataji wa taarifa. Hii, kwa kiwango kikubwa, inapunguza rasilimali zinazohitajika kuendesha mfumo wa ujasusi.

Kwa nini tusimuulize rafiki yetu ChatGPT yenyewe:

Wangehitajika watu wangapi leo kuiendesha mfumo wa upelelezi ya taifa lenye ukubwa kama wa Tanzania?
ChatGPT: “Kwa kuzingatia ukubwa na idadi ya watu ya Tanzania, kwa mfumo mzuri wa ufuatiliaji wa kitaifa wenye ‘coverage’ ya wastani na baadhi ya maeneo kuendeshwa kiotomatiki, idadi halisi ya wafanyakazi inaweza kuwa kati ya maelfu machache (kama watu 2,000–5,000).
Kwa ‘coverage’
ya kiwango cha juu (ikiwa ni pamoja na maeneo ya vijijini, saa 24, wingi mkubwa wa vifaa), inaweza kufikia makumi ya maelfu (kwa mfano 20,000–40,000+).”

Tuchukue idadi ya juu – 20,000 – hiyo ni jasusi mmoja kwa kila watu 3,500 (unakumbuka nyuma nchi ya GDR ilitumia 1 kwa kila watu 55?). Kwa kulinganisha, inakadiriwa kuwa serikali ya Tanzania inaajiri takriban watu 850,000 – hao ni wale waliopo rasmi. Kwa hivyo, watu 20,000 kwa kumfikia kila mtu (‘total coverage’) au hata 2,000 kwa ‘coverage’ lengwa si idadi kubwa.

Hivyo basi, si swali la uwezo tena, bali ni swali la nia ya kuweka mfumo kama huo.
Na swali la kwamba nia hiyo ipo wapi katika nchi yetu, naliachia kwenu ndugu zangu.


Kwa hiyo, kizuizi cha mwisho dhidi ya ufuatiliaji ni mfumo wa kisheria unaolinda taarifa zetu binafsi na uaminifu wa makampuni.
Uamuzi juu ya uimara wa kizuizi hicho, naliachia tena kwenu ndugu zangu.

Madai hizi si za kubahatisha tu. Kwa taarifa ya Sauti Kubwa, serikali ya Tanzania ilinunua programu ya kijasusi kutoka Israel iitwayo Pegasus mwaka 2017, na kuitumia kudukua vifaa vya waandishi wa habari, viongozi wa dini, watetezi wa haki za binadamu, na mawakili — na kufuatilia mawasiliano yao pamoja na walipo. Zaidi ya hayo, unakumbuka kesi ambayo Tundu Lissu aliifungua dhidi ya kampuni ya Tigo, akidai kuwa mtoa huduma huyo alishirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa zake binafsi pamoja na mahali alipo?
Kesi hiyo iliishia wapi?

Ukiunganisha vidoti – mifano ambayo historia imetupa, na ishara tunazoziona nchini mwetu – bado unadhani huna cha kuficha, kwa hiyo huna cha kuogopa?
Je, hakuna kitu ulishawahi kusema katika mazungumzo ya faragha na rafiki wa karibu au kitandani na mwenza wako au mpenzi?
Hakuna ujumbe au maoni uliyowahi kucomment au kutext yaliyoweza kukuletea shida kwa engo fulani? Simu yako haijui udhaifu wako unaoweza kutumiwa dhidi yako? Gallery yako haina picha au video zinazoweza kukuaibisha?

Tuna haki ya kuficha mambo yetu binafsi kama inavyoainishwa katika Ibara ya 16 ya Katiba, na haki ya kujieleza kama ilivyo katika Ibara ya 18.
Lakini inaonekana ukiukwaji wa katiba yetu kupitia marekebisho ya kisheria na matumizi ya nguvu ya mamlaka umekuwa kama burudani ya kitaifa. Hili tunahitaji kulibadilisha.
Tunahitaji kuwawajibisha viongozi na serikali kwa kulinda haki za msingi za taifa letu, ikiwemo ulinzi wa taarifa zetu binafsi.


Mpaka wakati mwingine:

Wapenzi wa tamthilia za uhalifu wanajua kauli maarufu wakati mtuhumiwa anakamatwa na afisa wa polisi:
“Everything you say can and will be used against you”

Kama hatutahakikisha taarifa zetu zinalindwa, kila tunachosema, tunachoandika, tunachotoa maoni, tunachopiga picha au video, na vile tunavyofikiria kwa sauti halafu simu yetu ikavisikia na kuvirekodi – unaweza kuongeza vingine kwenye orodha hii kadri utakavyo – vyote vinaweza na vitatumika dhidi yako.

Tujilinde.
 
Back
Top Bottom